Tanzania Daima Jumatano, 29 julai 2009
Absalom Kibanda
MZIMU wa Richmond umerudi tena bungeni, ikiwa ni mwaka mmoja na ushei tangu ulipotua na kusababisha kuondoka kwa mawaziri wawili, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Februari mwaka jana.
Kurejea kwa Richmond ndani ya Bunge kunatokana na serikali kutoa tamko ambalo hatimaye linaweza kusababisha kazi kubwa iliyofanywa na iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato mzima wa mkataba ulioipa ushindi Kampuni ya Richmond kuzalisha umeme wa dharura wakati wa kipindi kigumu cha ukame cha kati ya mwaka 2006 na 2007 kuwa isiyo na maana kubwa.
Kwa hakika tamko la serikali lililotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, William Ngeleja likieleza namna serikali ilivyotekeleza maazimio 23 ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond, tayari limesababisha Bunge na pengine taifa kugawanyika.
Hata hivyo, ni wazi kwamba taarifa hiyo ya serikali ambayo hatimaye imewasafisha kutoka katika tuhuma viongozi wakuu wawili wa serikali; Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah imetoka ikiacha wazi matamshi yaliyopata kutolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika moja ya vikao vya Bunge.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Agosti 28 mwaka jana, Pinda akizungumza bungeni kuhusu hatima ya viongozi hao wawili ndani ya Bunge, alisema suala lao lilikuwa limefikishwa Ikulu kwa ajili ya kufanyiwa kazi, hasa ikizingatiwa kwamba wao ni wateule wa rais.
Kwa maneno yake mwenyewe Pinda alisema: ‘‘Kutokana na nafasi yake kikatiba, mamlaka yake ya nidhamu ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
‘‘Kwa hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji wakuu watatu waliokuwa wanaishauri serikali, suala lake la kuhusishwa kwake katika mchakato mzima wa mkataba huo, linashughulikiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu.” Mwisho wa kunukuu.
Pinda hakuishia hapo, bali alikwenda mbele na kusema azimio namba saba la Bunge lililokuwa likitaka watumishi walioshiriki katika kamati ya serikali ya majadiliano wawajibishwe, lilikuwa limeangaliwa kwa namna ya kuwapa nafasi watuhumiwa kujitetea.
Miongoni mwa watu ambao Pinda alisema walikuwa wameandikiwa barua ya kujitetea ni pamoja na Hoseah ambaye alikuwa ameandikiwa na Katibu Mkuu Kiongozi ili aeleze namna alivyoshiriki katika mchakato huo.
“Ili kutekeleza azimio hili, Mkurugenzi TAKUKURU amepelekewa barua ya kutakiwa kujieleza na mamlaka yake ya nidhamu ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi.
“Vilevile, wasaidizi walio chini yake walioshiriki katika zoezi la uchunguzi, nao wametakiwa kutoa maelezo yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambaye ndiye mamlaka yao ya nidhamu.
‘‘Hii ni kwa kuzingatia misingi ile ile ya kanuni asilia ya haki ya kusikilizwa kwanza,” alisema Pinda akitoa kauli ambayo inafanana kimantiki na ile aliyotoa Lowassa bungeni siku alipotangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu, Februari mwaka jana.
Hata hivyo, katika kuonyesha namna serikali ilivyokuwa imedhamiria kuchukua tahadhari katika suala hili zima, Pinda alisema halitakuwa jambo rahisi kwa Rais Jakaya Kikwete, kuwastaafisha au kuwafukuza kazi watuhumiwa hao bila kufuata taratibu zinazotakiwa, kwani akifanya hivyo, kuna hatari kwa serikali kuwalipa fedha nyingi iwapo watakwenda mahakamani na kushinda kesi zao.
Kwa haraka haraka, maneno hayo ya Pinda aliyotoa mwaka jana na hitimisho lililotolewa na serikali bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita, ni ushahidi wa wazi wa namna serikali ilivyokuwa imeamua kwa dhati kuitupa kwa heshima ripoti ya Kamati Teule ya Bunge.
Huku ikijua kile ilichokuwa ikikifanya, serikali kwa namna ya kuweza kulifunga mdomo Bunge kwa kutumia kanuni zake lenyewe, ikaamua kutekeleza baadhi ya maazimio ya Bunge ambayo hayakuwa na athari za moja kwa moja kwa watu wazito.
Kwanza, ikaanzisha utaratibu wa kufuta usajili wa Kampuni ya Richmond kutoka katika vitabu vya Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) na kabla ya kumfikisha kortini mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo ambayo hakuna shaka usajili wake ulikuwa na utata na mashaka makubwa.
Kama hiyo haitoshi, huku ikijua hisia za kishabiki za baadhi ya wabunge, hususan wale waliojitoa mhanga kupambana na ‘mafisadi’ kisiasa, serikali ikaenda mbele na kuliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) kuvunja mkataba wake na Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd ambayo ilikuwa imeununua mkataba wenye utata kutoka Richmond.
Matokeo ya serikali kuvunja mkataba na Dowans kwa sababu tu ya kujaribu kupoza hasira za wazalendo wa Kitanzania wanaotoka katika makundi mbalimbali ya kijamii, waliojitwisha ufahari wa uanazuoni katika masuala yanayohusu nishati ya umeme, yalikuwa makali zaidi pale serikali hiyo hiyo ilipojaribu kuinunua mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 na ushei za umeme kwa mlango wa nyuma.
Wakati mzozo kuhusu ama kununua au kutonunua mitambo hiyo ya Dowans ukiendelea kulitikisa taifa, Rais Kikwete ambaye ndiye aliyepaswa kutoa mwongozo wa nini kifanyike kwa maslahi ya taifa, naye akaingia katika mtego rahisi wa kukiogopa kile ambacho yeye mwenyewe alikiita ‘alama za nyakati’.
Tukio hili la Rais Kikwete kuwatosa wateule wake wawili, Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid kwa lugha nyepesi isiyopaswa kutumiwa na kiongozi mkuu wa nchi ya ‘kusoma alama za nyakati’ ndiyo ambayo leo hii imelifikisha taifa hapa tulipo.
Ukitafakari kwa makini sakata zima la Richmond kwa kuangalia mlolongo mzima wa matukio, hasa yale ya baada ya kusomwa kwa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe na ambayo yamehitimishwa na tamko la serikali la majuzi, unaweza ukajikuta ukilazimika kuurejea ujumbe uliopuuzwa uliotolewa bungeni na Lowassa siku alipotangaza kujiuzulu.
Pengine kabla sijahitimisha hoja yangu nichote sehemu tu ya maneno aliyosema mwanasiasa huyu siku hiyo ambayo kwa bahati mbaya yaliachwa yakapita pasipo kujadiliwa mbali ya kujibiwa kwa maneno makali na Mwakyembe mwenyewe.
“Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunifanya msemaji wa kwanza katika hoja hii.
Lakini la pili, nimpongeze Dk. Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Kamati Teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli. (Makofi).
Kwa kazi nzuri kwa maoni yao, wamewasilisha vizuri. Lakini nimesimama kuweka kwenye kumbukumbu kutoridhika kwangu na jinsi kazi hiyo ilivyofanywa.
Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe ni mwanasheria, tena daktari, alikuwa anafundisha wanafunzi chuo kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa anafundisha ni “Natural Justice”.
Mheshimiwa Spika, wewe pia ni mwanasheria unafahamu suala la “Natural Justice”. Kwamba Kamati Teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong’ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja katika watuhumiwa mle hawakunihoji hata siku moja.
Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu (Dar es Salaam) hata wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari kufanya hivyo.
Hawa ni watu makini sana siwezi kuamini kwamba wanaweza wakafanya ‘oversight’ kama hiyo.
Kwa sababu katika kila hoja walizojenga wamesema Waziri Mkuu ilikuwa hivi. Kulikuwa na shida gani kuja kuniuliza Waziri Mkuu wanasema ulitoa dokezo hili ni sawa sawa ni kweli? Kulikuwa na shida gani kwa mfano kufuata utaratibu wa Westmister kuthibitisha hapo unaposema mwenye Richmond ni fulani uka – lay on the table records na ushahidi kuwa ni fulani.
Mheshimiwa Spika, taifa letu ni taifa changa, lakini chombo hiki ndiyo mahali pa demokrasia pakubwa katika nchi pote, hapa ndipo penyewe.
Kama katika chombo hiki hakitaonekana kutendeka haki nchi yetu haitakwenda vizuri. Hapa ndipo tunategemea tuwaonyeshe umakini wetu, umahiri wetu katika mambo ya demokrasia.
Kwa hiyo, nilichofanyiwa napenda kuweka kumbukumbu sawa kwamba, naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.
Maana zimechukuliwa tuhuma zikaja zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijaulizwa. Kulikuwa na shida gani ya kuniuliza, kwa nini muamini minong’ono ya mitaani kuliko maelezo yangu?
Sisi wote hapa ni wanasiasa, tukianza kuamini minong’ono ya mitaani niambieni mwanasiasa atakayesimama. Hatuwezi, tume imepewa muda wa kutosha lakini inashindwa kumuona mtu ambaye wanamtuhumu na wanamsema kwa kirefu sana.
Mheshimiwa Spika, lakini hata pale uliponinong’oneza ukaniambia una ushahidi wowote? Nilikuwa ushahidi huo wa maandishi.
Katika taarifa yao hakuna hata moja ya ushahidi ambao umetoka Waziri Mkuu. Kile kitabu cha majedwali kimejaa majedwali mengi pamoja na magazeti mpaka ya udaku lakini maelezo ya Waziri Mkuu hakuna hata moja. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, naamini ingekuwa ni heshima wangeiweka halafu wakasema tunakataa kitambulisho hiki kwa sababu hii na hii na hii, hiyo ndiyo imejengwa hoja.
Lakini kujenga hoja na kuja hapa bungeni tunahutubia nchi nzima na kusema Waziri Mkuu amefanya hiki, amefanya hiki bila ya kumsikiliza nachelea kuuliza hivi mtu wa chini itakuwaje?
Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi hasa kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni?
Mimi nadhani there is a wish which I am going to grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.
Mheshimiwa Spika, nimetafakari sana kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya serikali yangu nimeamua kumwandikia rais barua ya kumwomba niachie ngazi.
Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji lakini na kutokukubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya Bunge wa kumsingizia mtu.” Mwisho wa kunukuu.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, Bunge lililojaa watu makini na wachambuzi hodari wa mambo, kwa sababu tu ya kuelemewa na ushawishi wa kishabiki na woga uliojengwa katika misingi ile ile ya Kikwete ya kuzihofia alama za nyakati, lilishindwa kuzijadili kwa kina hoja za Lowassa ambaye kwa wengi habari, makala za kichambuzi tulielekeza mashambulizi kwake (Tuendako ikiwamo), na tahariri mbalimbali za magazetini.
Leo hii ukitafakari kwa utulivu, unaweza kushangaa ni kwa nini Lowassa, yule mwanasiasa jeuri aingie katika mtego ule ule rahisi wa kutishwa na kishindo cha alama za nyakati hata kuamua ‘kuachia ngazi’ badala ya kuliomba Bunge liipe serikali muda wa kutosha kujibu hoja za Kamati ya Mwakyembe.
Ukiliacha hilo, ni jambo la ajabu sana kwamba, katika hali ile, wabunge wale wale ambao leo ni hodari kusimama kwa kujiamini wakitaka muongozo wa Spika, walishindwa kumwomba Spika, amtake Lowassa athibitishe matamshi yake mazito dhidi ya kamati teule kwamba ilisema uongo ndani ya Bunge.
Kwa hakika, leo hii serikali inapotoa taarifa ya kuwasafisha viongozi takriban wote waliotuhumiwa katika Kamati Teule ya Mwakyembe, huku jina la Lowassa likiachwa pasipo kuguswa, ni rahisi kabisa watu kuamini na kuaminishwa kwamba kumbe kweli tatizo lilikuwa ni uwaziri mkuu.
Kama hiyo haitoshi, tunapomsikia Waziri Mkuu Pinda akisema serikali ilikuwa imewapa muda maofisa wake wote waliotuhumiwa na Bunge kutoa utetezi wao kwa mamlaka zilizowatetea, uamuzi huo, moja kwa moja unayafanya maneno ya Lowassa aliyelalamika ndani ya Bunge kuwa hakutendewa haki kwa kutopewa nafasi ya kujitetea kuwa na nguvu kubwa.
Tunapofikishana hapa tulipo leo, kama taifa tunao wajibu wa kujitafakari upya na kukiri ukweli mchungu kwamba, ukianza na Rais Kikwete, Lowassa, Kamati ya Mwakyembe, wabunge, wanahabari na wananchi kwa ujumla, tulilishughulikia ndivyo sivyo suala zima lililohusu kashfa hii ya Richmond, kwa namna ya sote kubebwa na kile tulichokitengeneza sisi wenyewe na kukipa jina zito; ‘alama za nyakati.’
Kama wasemavyo wana historia, kila mara tunao wajibu wa kujifunza kutokana na makosa tuliyotenda nyuma, ili kujenga mustakabali mwema leo hii, tayari kwa kujiandalia mazingira bora huko TUENDAKO.
Mwisho
