Hii Blog ya Mtanzania Mzalendo ambaye anatumia fikra zake kuangalia mustakabali wa kimaendeleo wa taifa lake na watu wake, lengo likiwa ni kuisaidia nchi yake na yeye mwenyewe kuondokana na umaskini uliokithiri. Lakini pia lengo jingine ni kuwasaidia viongozi wetu kuongoza kwa kujali maslahi halisi ya taifa na si matumbo yao.
Thursday, October 27, 2011
Hizi ni dalili za kifo cha CCM
September 2010

Na Absalom Kibanda

TAIFA limeingia katika wiki ya saba ya kampeni za urais, ubunge na udiwani ambazo wagombea wake wamesambaa katika maeneo mbalimbali nchini wakijinadi kwa wananchi huku wakitumia kila aina ya mbinu za ushawishi; halali na batili.

Kwa jinsi mambo yanavyokwenda, kwa mara ya kwanza katika historia ya chaguzi kuu za vyama vingi, wagombea wengi wanaosaka nafasi za uwakilishi kutoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi zote tatu za urais, ubunge na udiwani wanaonekana wakikabiliwa na upinzani mkali ambao kwa kiwango kikubwa unatishia fursa zao za ushindi.

Ingawa katika nchi zilizoendelea na kupiga hatua kubwa katika ushindani wa demokrasia ya vyama vingi ni jambo la kawaida kutarajia mabadiliko ya uongozi kila unapofanyika uchaguzi mkuu, kwa nchi changa kama zetu, matarajio ya kimazoea huyaona matukio ya namna hiyo kuwa ni mambo yasiyoweza kutokea kirahisi.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana katika mataifa makubwa kama Marekani baadhi ya marais wa aina ya Jimmy Carter, George Bush (mkubwa) pamoja na kuwa na mafanikio kadha wa kadha wakati wa tawala zao, waliangushwa wakati walipojaribu kutetea nafasi zao katika muhula wao wa pili wa madaraka.

Hali kama hiyo ilimpata pia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown ambaye hata baada ya kuingia madarakani akipita katika mgongo wa Tony Blair pasipo kufanyika kwa uchaguzi mkuu, alijikuta akishindwa katika uchaguzi na mpinzani wake mkubwa, David Cameron.

Ni jambo la kushangaza sana kwamba, wakati matukio ya namna hiyo ya viongozi walio madarakani kukubali kushindwa katika chaguzi huru na za haki yakitokea katika nchi ambazo kutoka kwao tumeiga mfumo wa ushindani wa vyama vingi, kwenye nchi kama Tanzania, walio madarakani (viongozi na vyama vyao) wanaliona jambo hilo kuwa lisilokubalika na lisilopaswa kutokea.

Dalili za wazi za viongozi walio madarakani kukataa katakata kushindwa hata katika sanduku la kura, zimekuwa zikionekana kutokea kila zinapofika nyakati kama hizi za kampeni za kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana leo hii wakati upepo ukionekana dhahiri kuvuma dhidi ya CCM katika ngazi ya urais kwa upande wa Zanzibar ambako mgombea kwa tiketi Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anaonekana kuwa na nguvu kubwa na ushawishi unaojitosheleza dhidi ya mshindani wake wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein bado mazingira yanaendelea kubainisha kuwa watawala wanazidi kuliona tukio hilo kuwa lisilopaswa kutokea.

Hali hii ya mambo imeanza kujionyesha hata kwa upande wa serikali ya muungano ambako katika mazingira ambayo si rahisi kuyaeleza kwa haraka haraka, mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Dk. Willibrod Slaa anaonekana kila kukicha akizidi kuvuta ushawishi unaoonekana kutishia urais wa Kikwete.

Kuongezeka kwa mbwembwe na kujiamini kwa Chadema na Dk. Slaa kwa kiwango cha kulifanya tishio lao hilo kuchukua picha inayoanza kuonekana kuwa ni ya kweli na dhahiri, kumesababisha kuibuka kwa matukio na mambo ya kushangaza ambayo yumkini kwa sababu moja au nyingine yanazidi kukiweka chama tawala katika taswira mbaya.

Kwa namna hiyo hiyo, kustawi na kuzidi kung’ara kwa nyota ya Maalim Seif na CUF yake katika mchuano wa urais Zanzibar kwa kiwango cha kuiweka njia panda CCM, nako kunaonekana kupokewa kwa njia ambazo ni dhahiri zinaanza kujenga mazingira ya kutaka kuchafua hali ya hewa ya kisiasa na dalili njema za ustawi mpya wa ustahimilivu.

Ili kuweza kuwazuia Dk. Slaa kwa Tanzania na Maalim Seif kwa Zanzibar, CCM na mawakala wake kwa ustadi mkubwa wameamua kuendelea kuvitumia vyombo vya habari kujenga taswira ambayo hakuna shaka hata kidogo lengo lake ni kuhakikisha wapinzani hao wawili na vyama vyao hawafanikiwi kuendelea kupenya mioyo ya wapiga kura walio wengi.

Kupitia vyombo kadha wa kadha vya habari, kwa makusudi na kwa nia ya kupotosha au kukuza mambo, kumeibuka taarifa za ajabu ama dhidi ya Maalim Seif na CUF yake kwa upande wa Zanzibar au Dk. Slaa na Chadema yake kwa upande wa serikali ya muungano.

Wakati kwa upande wa Zanzibar mawakala wa CCM wameanza kupenyeza makala za kumpaka matope Maalim Seif kuwa ni mwanasiasa mwenye lengo la kuvunja muungano na kuvitenga visiwa vya Unguja na Pemba, Dk. Slaa na Chadema yake sasa wameanza kuhusishwa na siasa za kutishia amani ya nchi na mshikamano wa kitaifa.

Kama hiyo haitoshi, mawakala hao wa CCM ambao hakuna shaka wamekuwa wakitumia mbinu za namna hiyo hiyo kila zinapofika nyakati za uchaguzi kama hizi wamefikia hatua ya kuandika habari za kupindisha ukweli zinazoonyesha eti Maalim Seif ameshakubali kushindwa urais wa Zanzibar hata kufikia hatua ya kujisalimisha chini ya Dk. Shein akiomba dua aambulie umakamu wa rais katika serikali ya umoja wa kitaifa inayotarajiwa kuundwa baada ya matokeo kutangazwa.

Ni wazi kwamba, Maalim Seif mwenyewe, mmoja wa viongozi adhimu na wa mfano ambao taifa hili limepata kuwa nao atakuwa ameshang’amua janja hiyo ya CCM na mawakala wake na hivyo atalazimika kuendelea kupiga kampeni pasipo kulitaja tena jina la Dk. Shein.

Wakati Maalim Seif na CUF wakionekana kung’amua janja ya CCM na mawakala wake inayolenga kuwaondoa katika mstari wa kuendelea kunadi sera na mwelekeo wao wa kiuongozi, hali inaonekana kuwa tofauti kwa Chadema na kwa Dk. Slaa ambao kwa kutojua au kwa makusudi wamejikuta wakijizatiti kujibu kila aina ya mashambulizi yanayoelekezwa kwao.

Tamko lililotolewa na vikosi vya ulinzi na usalama na kusomwa mbele ya wanahabari na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo mwishoni mwa wiki iliyopita ni kielelezo kimoja cha kishindo na nguvu ya upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wakati katika uchaguzi mkuu uliopita, tamko kubwa la vikosi vya ulinzi lilitolewa na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Omar Mahita aliyefikia hatua ya kukihusisha CUF kwa namna ya uzushi wa wazi na jaribio la kuvuruga amani kwa kuingiza nchini visu vyenye rangi ya bendera za chama hicho, mwaka huu hali inaonekana kuwa mbaya kwa kiwango cha kuhusisha vikosi takriban vyote vya ulinzi.

Tamko la mwaka huu mbali ya kutoa kila aina ya mwelekeo kuwa lilikuwa likikilenga Chadema ambacho viongozi wake walikuwa wamekaririwa wakisema walikuwa hawako tayari kuona matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani yakichezewa kwa maslahi ya kuibeba CCM, kwa upande mwingine lilikuwa likionyesha kuwapo kwa hofu ndani ya dola kwamba chama hicho tawala kilikuwa katika hatua ngumu zaidi ambayo haijapata kufikiwa wakati mwingine wowote kabla ya uchaguzi huu.

Akili za kawaida kabisa zinaonyesha kwamba, uzito wa nafasi ya Jenerali Shimbo ndani ya jeshi na ule wa matamshi aliyoyatoa mbele ya wana habari kwa namna yoyote ile yalikuwa yakibeba uzito wa ujumbe ambao ulikuwa nyuma ya matukio ambayo wanaamini yanaweza kutokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Ni wazi kwamba, Jenerali Shimbo na vikosi vingine vya ulinzi na usalama wa taifa vilifikia hatua ya kutoa tamko lile si kwa sababu tu ya kutishwa na kombati zinazovaliwa na makamanda wa kisiasa wa Chadema au maneno makali ya akina Freeman Mbowe na Dk. Slaa bali uzito wa kile ambacho kilikuwa kikitarajiwa baada ya uchaguzi mkuu.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, iwapo vikosi vyetu vingekuwa vikishtushwa na kauli za ama uchochezi au zile zenye mwelekeo wa kutishia amani ya nchi, basi tungepata kuwasikia majenerali wa kabla ya Shimbo wakitoa matamshi ya namna hiyo dhidi ya kauli ambazo kuanzia mwaka 1995 zilikuwa zikitolewa na wanasiasa wa aina ya Christopher Mtikila.

Kwa sababu hiyo basi, kwangu mimi kwa viongozi wa upinzani, wagombea wao na kwa wapiga kura, kauli kama zile za Jenerali Shimbo zilipaswa kujibiwa kwa kuandaa mikakati ya kujizatiti kushinda kwa kujenga ushawishi zaidi na kwa njia ya kulinda kura kwa namna ambayo haitakuwa rahisi kuibiwa.

Ili kufanikisha hilo, akina Dk. Slaa, Mbowe na wenzao wengine wa ndani ya Chadema walipaswa na kimsingi wanapaswa kuendelea kukifanya sasa ni kuwashawishi wananchi sababu za kuwachagua wao na kuwaweka kando akina Kikwete na wagombea wa CCM badala ya kuendelea kuzozana na majenerali ambao kwao siasa si eneo lao la kujidai.

Ni wazi kwamba, iwapo vyama vya CUF (Zanzibar) na Chadema (Tanzania Bara) vitakuwa na mikakati imara na endelevu ya kisera, kifedha, kimtandao na kioganaizesheni basi safari ya CCM kuendelea kubakia madarakani inaweza ikawa imeanza kukoma mwaka huu kwa upande mmoja wa muungano au kwa pande zote mbili.

Ingawa hilo linaweza likaonekana kuwa ni ndoto ya alinacha kwa baadhi ya watu, hususan wale walio na maslahi ndani ya CCM, ukweli wa kimazingira umeanza kuonyesha kwamba silaha pekee ambazo chama hicho tawala kimebakiza na ambazo sasa inazitumia kama turufu yake ya ushindi ni nguvu ya fedha (si sera), mtandao na historia yake ambayo inawafanya hata wale ambao walipaswa kuwa wameshakihama chama hicho waendelee kubakia humo humo. Hizi ni dalili za mwanzo za kifo cha CCM.

Mwisho
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 2:34 AM | Webu Unganishi |


0 Comments: