Hii Blog ya Mtanzania Mzalendo ambaye anatumia fikra zake kuangalia mustakabali wa kimaendeleo wa taifa lake na watu wake, lengo likiwa ni kuisaidia nchi yake na yeye mwenyewe kuondokana na umaskini uliokithiri. Lakini pia lengo jingine ni kuwasaidia viongozi wetu kuongoza kwa kujali maslahi halisi ya taifa na si matumbo yao.
Wednesday, December 10, 2008
Tunaongozwa na kizazi cha watu wala watu
Na Absalom Kibanda


NCHI hii haiishi vituko. Kila siku inayokwenda kuna jambo jipya linaloibuka katika nchi hii na kufunika lile lililotangulia au lililotokea siku, wiki, miezi au miaka kadhaa iliyopita.

Katika siku za hivi karibuni, Watanzania tumeshuhudia kuibuka kwa mambo kadha wa kadha mazito yanayogusa mwenendo wa mambo kitaifa na pengine kuathiri kwa namna njema au mbaya mustakabali wetu kama nchi leo hii na katika siku zijazo.

Jambo la kwanza ambalo nimekuwa nikilitazamia katika hayo yote ninayofikiria ni lile linalogusa kesi zinazowakabili baadhi ya watuhumiwa wa wizi wa mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania katika kipindi cha mwaka 2005.

Kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa 20, wote wakijimuishwa katika tuhuma mbalimbali ndani ya mtungi mmoja huo huo wa EPA wakiwamo wafanyabiashara wenye majina makubwa wa kiwango wa ‘Jeetu Patel’ kulifungua ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya ufisadi, tatizo ambalo hakuna shaka limekuwa kitovu cha ulaji usiostahili kwa miaka mingi sasa.

Matukio ya kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hawa yaliyozingira hisia na mwenendo wa mambo nchini kwa takriban wiki mbili, kulianza kuonekana kuwa ni mwanzo wa kikweli kweli wa mafanikio ya vita dhidi ya ufisadi iliyoanzishwa katika kipindi cha karibu mwaka mmoja na ushee uliopita.

Hata hivyo kama ilivyo ada, tukio hili la kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao, lilionekana kuligawa taifa katika makundi mengi kwa kiwango cha kusababisha kila kundi kuibua hoja zinazokinzana.

Kundi moja la wanaharakati wenye msimamo mkali kuhusu ufisadi, lilikataa na kimsingi limeendelea kukataa kukiona kitendo cha kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao 20 wa EPA kuwa hatua ya kwanza ya mafanikio ya serikali, Rais Jakaya Kikwete, wao wenyewe na vyombo vya habari ambavyo kwa pamoja vimekuwa vikipambana na vitendo vya ufisadi.

Kwa waumini wa kundi hili, mafanikio ya kweli kweli katika sakata hili la EPA yangeonekana iwapo tu, serikali na hususan Rais Jakaya Kikwete wangefumba macho na kuyafikisha mahakamani makampuni yote ambayo kwa namna mmoja au nyingine yalishiriki katika uchotaji wa shilingi bilioni 90 na ushee kati ya zile bilioni 133 zilizoibwa kutoka akaunti nzima ya EPA.

Kwa sababu hiyo basi, wanaharakati wa kundi hili walikuwa wakiamini kwamba, Rais Kikwete na serikali yake walikuwa hawana sababu hata moja ya kuwatenga wezi wa EPA katika makundi mawili ya wale waliorudisha fedha na wale ambao hawakurudisha na badala yake wote walikuwa wakipaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kuiacha korti iamue hatima yao.

Kwa watu wa kundi hili, hatua ya serikali kutangaza msimamo wa kuwasamehe wale wote waliorejesha fedha, ilikuwa ina maana moja tu kwao; ‘usaliti katika mapambano dhidi ya ufisadi.’

Wafuatiliaji wasiopendelea upande wowote katika mapambano haya ya ufisadi ni mashahidi wazuri kwamba, uamuzi huu wa serikali kuwasamehe wale wote waliolipa fedha hizo ulizidi kuonekana usiofaa hasa baada ya taarifa kuanza kuvuja kwamba kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ilikuwa miongoni mwa makampuni yaliyokuwa yamefanikiwa kurejesha fedha zote kiasi cha shilingi bilioni 40 ilichochota EPA.

Taarifa kwamba Kagoda ilikuwa imefanikiwa kukwepa kitanzi na hatari ya kufikishwa kortini, ilikuwa ni habari mbaya kwa wanaharakati ambao kwao, kampuni hiyo ndiyo iliyokuwa ikistahili kubebeshwa mzigo takriban wote wa EPA pengine kabla ya mtuhumiwa mwingine wowote.

Joto la mtazamo wa wanahaerakati hao na mashabiki zao ndiyo ambayo imesababisha baadhi yao hadi leo hii kuendelea kuziona kesi zilizofunguliwa dhidi ya watuhumiwa wa EPA kuwa ni kiini macho na mchezo wa kuigizwa usio na lengo la kuikomboa nchi hii katika tatizo sugu la ufisadi.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wanaharakati wa kundi hili wanaitaka serikali, Rais Kikwete na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuchukua hatua za kuifikisha Kagoda mahakamani huku wakisahau ukweli wa wazi kabisa kwamba, kampuni hiyo ambayo usajili, mahali ilipo, wamiliki wake na namna ilivyochota fedha ni mambo yenye utata mkubwa inaonekana kuwa na uhusiano wa moja kwa moja wa siri na wa wazi na watu wenye mamlaka au waliopata kushika madaraka makubwa kabisa kidola.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wanaharakati hawa wa ufisadi ambao kimsingi nayaunga mkono mapambano waliyoyaanzisha, wanasahau kabisa kile ambacho mwanazuoni wa siku nyingi na mwanasheria aliyebobea, Profesa Issa Shivji alipata kukisema kuhusu uhalali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuongoza nchi kikiwa katika taswira yake ya sasa ya chama dola.

Nasema hivi kwa sababu utafiti wangu binafsi kama mwanahabari na mtu ambaye katika kipindi cha miaka takriban 10 ya kazi yangu hii nimepata kukutana na kuzungumza na watu kadha wa kadha wakiwamo wale wanaohusishwa na Kagoda umenithibitishia pasipo shaka kwamba kampuni hii inayotajwa, ilianzishwa kwa utaratibu haramu ulioratibiwa na dola na kusimamiwa na baadhi ya viongozi wa juu serikalini na makada wenye nguvu ndani ya CCM.

Ni kwa sababu hiyo basi, ushahidi wa mazingira unaonyesha pasipo shaka kwamba, Kagoda ni jinamizi ambalo mizizi yake ilijengwa na uharamu uliokipa chama tawala uhalali wa kuendelea kuongoza nchi hii, kikiwa na sura yake ile ile ya CCM iliyostawi katika mizingira ya kidikteta yaliyorithiwa na vyama vya kisoshalisti na kikomunisti duniani zama za vita baridi.

Hakuna shaka kwamba, Kagoda katika maelezo ya kisomi, ni mfano wa taasisi za kifisadi, iliyojengwa ikihusisha dola na chama tawala ambavyo uhalali wa ubia wao uliwashirikisha wafanyabiashara marafiki na makada wakubwa wa CCM.

Mahusiano haya ndiyo ambayo kwa kiwango kikubwa yalisababisha serikali kushikwa na kigugumizi mapema kabisa sakata hili la EPA lilipoanza hata kufanya jitihada za kununua muda kwa kuhalalisha makampuni makubwa mawili ya kimataifa ya ukaguzi wa mahesabu, kwanza Delloite & Touche na kisha Ernst & Young kuyapitia mahesabu ya BoT na EPA na kisha kuwasilisha taarifa zake serikalini.

Ni jambo la ajabu kwamba, hata baada ya Delloite & Touche kupitia mahesabu na kubaini wizi uliofanywa na Kagoda na makampuni mengine na serikali kuamua kuipa kampuni nyingine kazi ile ile, wanaharakati hawa wenye msimamo mkali walihadaika na kuipa dola nafasi nyingine ya kujipanga na kutafuta majibu ya namna ya kujinusuru.

Ni jambo la ajabu kwamba, wanaharakati hawa hawa, walikaa kimya na wakashindwa kutambua nini maana ya yote hayo ilhhali katika kumbukumbu zao wakiwa na barua mbili zenye kupingana zilizoandikwa katika kipindi kisichozidi wiki moja na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Zakia Meghji kuhusu sakata hilo hilo la EPA.

Ni ukweli rahisi kabisa kwamba, iwapo wanaharakati wangekuwa wakiunganishwa na chombo chenye sauti moja kuhusu jambo hili, wangebaini mapema kabisa kwamba, Meghji aliingizwa katika mtego wa barua mbili zinazokinzana si kwa sababu ya udhaifu wake, bali kutokana na shinikizo la kidola ambalo lilikuwa likimtaka yeye kama Waziri wa Fedha kufanya lolote lililokuwa likiwezekana kuinusuru serikali, chama chake na baadhi ya watu wenye mamlaka ambao kwa namna moja au nyingine walitumia madaraka yao vibaya kuihalalishia CCM ushindi mwaka 2005.

Leo hii wanapoibuka kwa ujasiri mkubwa, akina Reginald Mengi, Dk. Willibrod Slaa, Zitto Kabwe, M.M Mwanakijiji, Mpayukaji, wanaharakati na wanasiasa wengine wengi makini wakitaka siri ya Kagoda ifichuke, kwa hakika hoja zao zinazidi kuongeza mtihani kwa serikali ambayo imenunua muda mwingi na kutumia kila aina ya mbinu kuinusuru kampuni hii.

Unapoziangalia juhudi zote hizi za serikali za kuinusuru Kagoda, kwani wakifanya siri taarifa zote za ukaguzi wa mahesabu ya BoT, hata baada ya nyingine kuonekana zimevuja, pili wakitumia kamati ya Mwanyika ambayo hadi leo hii matokeo yake ni kitendawili na tatu wakijaribu kujificha nyuma ya madaraka makubwa ya kisheria ya DPP, ndipo siri na nini hasa kinachofichwa kinapojulikana.

Kwa hakika leo hii angetokea Mengi, Slaa, Mwanakijiji na Mpayukaji wakaniuliza ni jambo gani bora unalodhani linatupasa Watanzania tulifanye ili kujua kwa uhakika siri iliyojificha ndani ya Kagoda, sintapita na kuanza kutaja orodha ya wamiliki wa kampuni hiyo tata bali jicho langu na akili yangu nitaielekeza CCM moja kwa moja.

Nasema hivi kwa sababu naamini tena kwa dhati kabisa kwamba, Kagoda ni mchezo mchafu wa CCM ambao ulitumika kukirejesha madarakani isivyo halali chama hicho tawala mwaka 2005 kikinunua mioyo ya watu kwa fedha haramu hata kuwapa udiwani, ubunge na urais.

Kwa sababu hiyo basi, kwangu mimi Kagoda si mtu mmoja, wawili watatu au wanne, bali ni mkakati wa miaka mingi, wa CCM na serikali yake wa kufuja matrilioni ya fedha ambazo malengo yake ya msingi ni kuwahudumia wananchi wanaoishi maisha yaliyozongwa na tabu ambazo kimsingi hawastahili.

Kwa sababu hiyo basi, jibu langu kwa Mengi lingekuwa mdudu Kagoda anayetafuta jibu lake ni tunda la uasi lililostawishwa kikatiba na kuipa CCM mamlaka ya dola ambayo yamkini mafisadi wachache wanaopewa baraka na dola wamekuwa wakiyatumia kufuja na kuimaliza nchi hii.

Kwa hakika staili iliyotumiwa na CCM na serikali yake kuhalalisha wizi BoT mwaka 2005 ndiyo ambayo ilitumika wakati serikali ilipoliingiza taifa katika mradi tata wa Richmond ambao uligharimu madaraka ya watu wachache sana serikalini ambao mpaka kesho naendelea kuamini walitolewa kafara ili kukinusuru chama hicho na fedhaha ya kuanguka kizima kizima.

Watanzania tunapaswa kutambua kwamba, staili hii ya CCM ya kujivua gamba nusunusu na kuwatoa kafara wachache miongoni mwa mafisadi wengi walio ndani ya chama na serikali yake, ndiyo ambayo imekuwa ikikijengea uhalali wa kuendelea kuwahadaa wananchi wenye mapenzi ya kweli na taifa lao.
Ni kwa sababu ya kuifahamu CCM kwa jicho hilo ndiyo maana hadi leo hii nimekuwa ni mtu wa mwisho kushangilia kuanza kusikilizwa kwa kesi za EPA, kufikishwa mahakamani kwa Basil Mramba na Daniel Yona mahakamani na kabla ya hapo kulazimishwa kujiuzulu kwa Edward Lowassa, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na.

Kwangu mimi mafanikio ya kweli ya vita dhidi ya ufisadi yataanza wakati Watanzania watakaposimama na kuacha kushangilia siasa za msimu na kuzika madhambi za wana CCM kulana wenyewe kwa wenyewe (Political Cannibalism) ama kwa kulazimishana kujiuzulu, kusutana, kunyosheana vidole, kutishana na kuburuzana mahakamani ilhali chama kinachotoa baraka za wizi huo kuendelea kikiendelea kubakia madarakani kikiwa na sura za watu wale wale wanaohamishana kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Huko ndiko tunakopaswa kwenda.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 2:01 AM | Webu Unganishi | Maoni 1
Monday, November 17, 2008

Nikiwa Mwenyekiti wa Kongamano la Ukosefu wa Uongozi Tanzania, nikitoa maelezo mafupi kabla ya kongamano hilo kufunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (katikati). Aliyeketi kulia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:41 AM | Webu Unganishi | Maoni 1


Hapa nikimpa mkono wa pongezi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mara baada ya kutoa hutuba wakati wa kongamano la Ukosefu wa Uongozi Tanzania (The Vacuum of Leadership in Tanzania) lililofanyika Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. Mimi ndiye niliyekuwa mwenyekiti wa kongamano hilo la kihistoria.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:33 AM | Webu Unganishi | Maoni 1

Hapa nikiwaonyesha wanafunzi wa chuo kimoja cha uandishi wa habari gazeti letu la michezo na burudani la Sayari ambalo huchapwa kila siku ya Jumatatu na Ijumaa


 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 7:07 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Reginald Mengi na wahariri
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 5:25 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Tarime: Ushahidi wa kupoteza mwelekeo
Na Absalom Kibanda

MAMBO yanayotokea Tarime hivi sasa na yale ambayo yamekuwa yakitokea katika miezi ya hivi karibuni yamesababisha nitafakari upya na nirejee kile ambacho nimepata kukiandika siku zilizopita.

Nimepata kusema na leo ninasema tena kwamba, nimekuwa miongoni mwa Watanzania ambao nimekuwa nikivutiwa na kuguswa na namna Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kilivyosheheni watu wenye upeo mkubwa wa kuona mambo.

Na hali hiyo kwa kiwango kikubwa ndiyo ambayo imekuwa ikikifanya chama hicho tawala ambacho sala zangu kila siku zimekuwa zikitaka kukiona kikimeguka kiendelee kubakia hai hata katika mazingira ambayo aghalab kingepaswa kusambaratika kama ilivyo hali leo hii.

Hakuna asiyejua kwamba, kwa miaka mingi, hata baada ya kupoteza dira kwa maana ya kuwa na falsafa moja inayokiunganisha, chama hicho kimebakiza jeuri moja kubwa ya kuwa na makada wasomi wazuri wa kariba ya maprofesa na madaktari wa falsafa ambao ama kwa shuruti au kwa mapenzi yao ni wabunge au mawaziri katika serikali ya CCM.

Mbali ya hao chama hicho pia kwa kutumia nguvu kubwa za kiserikali kimejijengea uhalali unaokipa mamlaka ya kuwafanya wafanyabiashara wakubwa takriban wote walio na majina makubwa kuwa ama wafadhili au makada wa kuheshimika kama si kuogopwa ndani ya chama hicho.

Hata hivyo ni ukweli ulio wazi kwamba, kundi la kwanza la wasomi wanaounda timu muhimu ya ushindi kwa chama hicho, wengi wao wamekuwa wakijiunga au kukiunga mkono chama hicho si kwa sababu ya kuvutiwa na changamoto za kifikra au mwelekeo sahihi wa kifalsafa bali, tamaa ya kupata madaraka na kuwa karibu na watawala.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, wengi miongoni mwa wasomi hao ambao chimbuko lao ni taasisi za elimu ya juu nchini, na ambao kuingia kwao katika siasa limekuwa ni moja ya mambo yanayoibua maswali mengi miongoni mwa wanazuoni wenzao, wamejiunga katika chama hicho tawala si kwa mapenzi yao ya kiitikadi, kimkakati na kivisheni ya chama hicho tawala, bali kiu yao ya kupata fursa ya kuteuliwa kuwa mawaziri na wakati mwingine kupata fursa ya kuwafikia wakubwa walio na madaraka makubwa.

Nimepata kulisema hilo huko nyuma na likaungwa mkono na wadau wengine wengi kwamba, idadi kubwa ya wasomi wanaoingia katika siasa katika Tanzania wamechochewa zaidi na kushamiri kwa aina ya kipekee ya rushwa inayostawishwa na madaraka ya kidola (state sponsered corruption) inayoshika nafasi kubwa pengine kuliko aina nyingine yoyote ya ufisadi katika zama hizi.

Ushahidi wa hili haupatikani mbali, kwani unaweza kujionyesha waziwazi unapoangalia aina ya maisha wanayoishi leo hii wasomi wetu hao, walioingia katika siasa na ‘wakabahatika’ kuvuna madaraka ya kiuteuzi yawe ndani ya Kamati za Bunge au ukatibu mkuu, ubalozi na hata katika Baraza la Mawaziri.

Ufahari na utamu wa maisha ya kimadaraka wanayokutana nayo wanazuoni hao waliogeuka kuwa wasomi, ni mambo yaliyosababisha wafikie hatua ya kupoteza hulka za kawaida za kisomi za kujenga fikra kinzani (critical thinking), kuibua mijadala, kuanzisha mada na wakati mwingine, kuainisha na kutumia njia za kisomi kutatua matatizo ya kisiasa, kiuchumi, kitekinolojia na hata kijamii.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana hata leo hii, wakati taiofa likipita katika tanuri la moto mkali wa siasa za kupakana matope, kuzushiana na kuchafuliana majina, kundi la wasomi walio katika siasa na pengine hata wale walio nje, nalo limejikuta likipoteza mwelekeo wa kimsingi wa zama zile za umarxist na uleninist wa miaka ya 1970 na 1980.

Kupoteza huko kwa mwelekeo kwa wasomi wetu ndiko ambako kumesababisha leo hii, ndani ya CCM kwa mfano kuibuka na kushamiri kwa majibu ya kishabiki na yasiyo na tija kila linapotokea tatizo la msingi.

Leo hii kwa mfano Watanzania wamejikuta wakiendelea kulishwa upumbavu wa kishirikina na kipuuzi unaozingira mazingira ya ajali iliyopoteza maisha ya aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe.

Mazingira ya ajali hii ambayo hadi sasa hakuna taasisi yoyote ya dola au ya kisomi imeonekana kufanya kazi yake sawasawa na kutoa majibu yanayoridhisha, yamesababisha kuibuka kwa nadharia za kizushi ambazo katika taifa linalotafuta siri ya maendeleo ni mwelekeo hatari na wa kimaskini.

Matokeo ya wasomi wetu, mmoja mmoja au kupitia katika taasisi zao za kitaaluma kuingilia kati na pengine kulifuatilia suala hilo ili kulinusuru taifa kuingia katika mtego wa hoja za kupikwa na za kufikirika za wanafamilia wa Wangwe, makada wa CCM na akina Mtikila zimesababisha taifa zima kuingia kidogo kidogo kulishwa uongo na kuanza kupoteza imani na watu au taasisi ambazo zinahusishwa na suala hilo.

Leo hii ikiwa ni miezi miwili kamili tangu kifo hicho kitokee, jeshi la polisi lililo na wanataaluma makini wa kuchunguza ajali, limekalia matokeo ya uchunguzi wake, ilihali likijua kwamba, mazingira ya kifo cha mbunge huyo yalikuwa yameshaanza kuibua maswali mengi.

Kama hiyo haitoshi, vyuo vya elimu ya juu nchini ambavyo navyo vinao watalaam katika fani mbalimbali wanaoweza kufuatilia ajali hiyo na kuja na maelezo yao ya kitaalam navyo vimewafungia masandukuni wanazuoni wake na kusababisha nao waingie katika kundi lile lile la kulishwa hadithi za kufikirika za akina Mtikila.

Udhaifu huu wa kitaasisi umesababisha kuibuka kwa mambo mengi na ya kutisha kuhusu ajali hiyo na katika siku za hivi karibuni, wanasiasa wa aina ya Mtikila wamesikika wakitoa ‘taarifa zao za uchunguzi’ ambazo ukizisikiliza unaweza ukajikuta ukishawishika kuamini kwamba, huenda msimuliaji alikuwa eneo la tukio au alikuwa shuhuda katika mpango mzima kabla ya mauti kumkuta Wangwe.

Ni jambo la ajabu kwamba, hata baada ya vyombo vya habari kuandika kila aina ya porojo kuhusu mazingira ya kifo hicho vikiwanukuu wabunifu wa hoja na mashabiki wa CCM wanaokihusisha Chadema na kifo hicho, hadi leo hii Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za dola nazo kwa namna moja au nyingine zimeingia katika mchezo huo huo wa siasa za kufumbia macho matokeo mabaya.

Katika kuthibitisha namna taasisi za dola katika nchi hii zilivyoingizwa katika mtego huu wa kupuuzi na kusababisha vishindwe kujua nini cha kufanya ili kuwaokoa Watanzania na hatari ya kuendelea kujazwa uongo katika bongo zao na kulishwa hadithi za alinacha hadi leo hii, si Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa, Zitto Kabwe au Christopher Mtikila waliohojiwa kuhusu kauli suala hili.

Lakini pengine kibaya zaidi ni kwamba, taasisi hizo za dola na hususan polisi, katika mazingira yanayoonyesha kusahau wajibu wao na kutojua athari za uzushi wa namna hii, limeshindwa kuchukua hatua zozote za maana na za wazi dhidi ya wazushi ambao kwa kutoshughulikiwa kwao na kuachwa waendelee kusema uongo kunasababisha watu wengi kuanza kukiamini kile wanachokisema.

Kuzorota huko kwa mambo kumebabisha kuendelea kwa hoja hizo za kufikirika na juzi katika kampeni za ubunge na udiwani huko Tarime, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe naye akaibua hoja mpya yenye mwelekeo ule ule unaoibua maswali.

Katika mazingira ambayo hayafai kupuuzwa hata kidogo, Zitto, mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa katika zama hizi, akaeleza kusikitishwa kwake na matamshi yanayotolewa na makada wa CCM, Mtikila na yale yaliyosemwa na mmoja wa wake wa marehemu Wangwe.

Kwa kujua au kutokujua, Zitto akafikia hatua ya kutaka mzizi wa fitina ukatwe kwa Spika wa Bunge kuunda tume huru kuchunguza mazingira ya kifo cha Wangwe na akaeleza kushangazwa na wale ambao wanaweza wakawa na mkono katika ajali hiyo kuwageuzia wengine madhambi yao.

Kwa staili ile ile ya kawaida ya polisi, kauli hii ya Zitto kama ilivyokuwa kwa kauli zile nyingine zilizotangulia nayo inaonekana kupuuzwa na kuachwa iwaingie Watanzania wengi na pengine kusababisha wachanganyikiwe kwa kiwango cha kuanza kushindwa kujua ni nani anasema kweli.

Lakini pengine jambo baya zaidi ni kwamba, hulka hii ya uzushi unaozingira kifo cha Wangwe imesababisha wakazi wa jimbo hilo wanaojiandaa kumsaka mbunge wao kujikuta wakiwa majeruhi wa siasa chafu na zilizokosa mwelekeo za zama hizi.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wakazi hao wa Tarime ambao wanakabiliwa na matatizo mengi ya kijamii na kiuchumi wamejikuta wakiwa majeruhi wa siasa hizo za fitina badala ya kula uhondo wa hoja zitakazoeleza mipango ya wagombea ya kuwaondoa katika hatari ya mapigano ya mara kwa mara ya koo, umaskini na kilimo cha bangi.

Kama hiyo haitoshi, kampeni hizo za Tarime ambazo leo hii zimethibitisha kwamba vyama viwili vya CCM na Chadema ndivyo vilivyo na ushindani mkuwa zimeweka kando kabisa namna ya kuiwezesha wilaya hiyo kuweza kutumia vyema na kwa manufaa yake fursa yake ya kupakana na Kenya kwa maslahi ya wana Tarime na Watanzania kwa ujumla.

Siasa hizi chafu zinazotungwa zikizingira jina la Wangwe zimesababisha wananchi wa Tarime wanyimwe fursa ya kuvisikia vyama na wagombea ubunge na udiwani wakieleza ni nini watakifanya kumaliza uhasama wa miaka mingi kati yao wakazi wa eneo hilo na kampuni ya uchimbaji madini ya North Mara.

Kwa hakika udhaifu huu wa mambo wa kuweka mbele siasa za majungu, uzushi, kufitiniana, kuchafuana na kupakana matope ndizo ambazo leo hii zimebabisha Tanzania kama taifa kupoteza mwelekeo na kujikuta tukishindwa kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoikabili dunia ya leo.

Siasa zenye mwelekeo huu ambazo kwa bahati mbaya zimekuwa zikishabikiwa kwa njia ya siri na ya wazi na viongozi wenye dhamana kubwa kabisa nchini, ndizo zilizozingira masuala makubwa makubwa takriban yote ya siku za hivi karibuni. Tunapaswa kutoka huko iwapo tunataka kupona.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 5:13 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Hii ni lala salama ya Kikwete
Na Absalom Kibanda


HALI ya hewa kisiasa imebadilika na inaendelea kubadilika kila kukicha hapa nchini kiasi cha kuifanya serikali na vyama vya siasa kuanza kukaa mguu sawa.

Mabadiliko hayo ya upepo wa kisiasa yamesababisha harakati za kuelekea katika hekaheka za uchaguzi mkuu miaka miwili baadaye kuanza mapema, pengine kwa namna na kwa njia tofauti na ambavyo imezoeleka kwa miaka mingi huko nyuma.

Dalili za wazi za kuanza kwa harakati hizo za kisiasa zimeanza kujionyesha na hivi sasa wanasiasa katika makundi na mitazamo tofauti wanaonekana kuanza kujijengea mazingira ya kujihalalishia ushindi wakati wa uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2010.

Matamshi yanayotolewa na wanasiasa hivi sasa yameanza kuchukua sura za wazi inayoonyesha kuanza kujipanga sambamba na kujaribu kuangalia mustakabali wao kwa siku zijazo.

Ukiyapima na kuyaangalia katika mizani sawia ya kisiasa matukio ya siku za hivi karibuni, unaweza ukashangazwa na namna wanasiasa wetu wanaopaswa kutambua uteke wa nchi hii kiuchumi wanavyopigana vikumbo kwa namna na kwa njia mbalimbali kujahalalishia ushindi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Matumizi makubwa ya fedha yaliyoshuhudiwa na wadau mbalimbali wa masuala ya siasa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Tarime ambako tulishuhudia wapigakura ‘wakinunuliwa’ kwa gharama kubwa, ni moja ya mifano hai ya namna mwaka 2010 unavyopewa mtazamo wa aina yake.

Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za ndani ya nchi wanaweza kukubaliana nami nikisema kwamba, juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tarime zililenga zaidi mwaka 2010 na si kuziba pengo la Chacha Wangwe aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Makada wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wao, Yussuf Makamba walikuwa wamepania kwa nguvu zote kufanya kile walichokifanya katika jimbo la Kiteto miezi kadhaa iliyopita, dhidi ya wapinzani ambao katika miezi ya hivi karibuni wamejipambanua kuwa majemedari wa ufisadi, vita ambayo hakuna shaka sumu yake imeanza kuwaingia kwa kasi kubwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Makamanda wa propaganda wa CCM, chama ambacho kimefanikiwa kupenya hadi katika mishipa ya watendaji wakuu wa vyombo vya dola, vikiwamo vile vya ulinzi na usalama kama jeshi la polisi, walilazimika kufanya kila linalowezekana kulitwa jimbo la Tarime wakijua kwamba kufanya hivyo kulikuwa na maana moja kubwa; kushindwa kwa vita wanayoiharamisha kwa nguvu zote ya ufisadi.

Ni bahati njema kwamba, upepo wa mambo haukwenda kama ilivyotarajiwa kwa CCM (walioungana na vyama vingine vichache mamluki) na ndiyo maana kwa namna ambayo si rahisi kuieleza, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikafanikiwa kupenya ukuta mgumu kabisa na kulirejesha jimbo hilo mikononi mwake.

Kwa hakika ushindi wa Chadema Tarime kwa namna ya kipekee ukabadili upepo na kuchukua sura tofauti ukiungwa mkono na watumishi wa taasisi za umma, watendaji wakuu serikalini, mawaziri na mwisho wa yote makada maarufu wengi wa CCM.

Kishindo hiki cha ushindi wa Chadema kwa kiwango kikubwa kikabadili kabisa ndoto za CCM za kukizorotesha chama hicho na kukifuta katika mioyo ya watu ambazo zilianza mapema tangu aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe akiwa hai.

Kwa hakika muanguko huo wa CCM ukawa pigo na funzo kubwa, dhidi ya hoja za kizushi na kuchuliana zilizoasisiwa na mabingwa wa fitina wa chama hicho tawala dhidi ya Chadema na hususan viongozi wake wakuu, Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa na Zitto Kabwe waliohusishwa katika ‘kutengeneza’ ajali na hatimaye umauti wa Wangwe.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa siasa hizo za kufitiana, zilizoanzishwa wakati Benjamin Mkapa akiwa rais, kwanza zikiwalenga wana CCM wa kariba ya akina, Hassy Kitine, Profesa Philemon Mbilinyi, Frederick Sumaye, Abdallah Kigoda, Wilson Masilingi, John Magufuli, Mark Mwandosya, Dk. Salim Ahmed Salim na wengine wengi zikagonga mwamba. Tarime ikaandika historia mpya.

Kwa watu wanaofuatilia mwenendo wa mambo ya kisiasa ndani ya CCM na pengine serikalini ni mashahidi kwamba, ushindi wa Chadema katika jimbo la Tarime, ukawa kielelezo kingine bayana kwamba, lile kundi la ‘mtandao masalia’ linalojaribu kujitutumua likilenga kuhujumu harakati za kuisafisha nchi likajikuta likiangushwa kwa kishindo.

Matukio haya ya kustaajabisha kisiasa yaliyoanza kuthibitika (na si kutokea) hapa nchini Februari mwaka huu, wakati Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe iliposoma hotuba yake bungeni yamepokewa kwa hisia tofauti na wafuatiliaji mbalimbali wa masuala ya siasa.

Kwangu mimi mambo haya yanathibitisha jambo moja la wazi kabisa kwamba, ardhi ya Tanzania na raslimali zake zote imefikia hatua ya kusema hapana na sasa imeanza kudai mabadiliko makubwa kabisa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayolenga kulinufaisha taifa zima na si kikundi kidogo cha wanyang’anyi waliofikia hatua ya kutaka kuibinafsisha CCM, kuiteka nyara serikali na kuiuza nchi.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, kikundi hiki cha watu wachache, wenye uwezo mkubwa kifedha na kiuchumi na ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia nguvu zao hizo kuendesha mambo, bado hawajakata tamaa na sasa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanabadili upepo wa kisiasa na kurejea tena katika ulingo wa kisiasa mwaka 2010.

Hata hivyo, kwa namna ya kushangaza kikundi hicho cha wanasiasa wenye nguvu kabisa na ambao wakati fulani walijitambulisha kama watu wasioshindwa na mtu yeyote katika lolote watakaloamua wamejikuta wakiendelea kubakia kuwa majeruhi wa siasa za zama hizi, wakichafuka hatua kwa hatua kiasi cha kuanza kuhatarisha uhuru wao katika kipindi kifupi tu kijacho, iwapo hawatakubali kushindwa.

Mfa maji haachi kutapatapa, kifo hiki cha kisiasa cha kikundi hiki kidogo cha watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa na ushawishi mkubwa, kimeamua kurejea katika mstari wake wa awali na sasa kimeamua kuchukua hatua mbadala, kikiamini kwa kufanya hivyo kitakuwa kimewafunga midomo watu wa aina ya akina Mbowe, Slaa, Zitto, Mnyika na wengine ambao upepo wa kisiasa wa siku za hivi karibuni unapunga upande wao.

Watu hawa kwa namna ya ajabu wameamua kupambana na vyombo vya habari binafsi ambavyo kwa mtazamo wao, wanaviona kuwa vimekuwa mstari wa mbele kuwaangusha, kuwaumbua na wakati mwingine wakisema vimekuwa vikiwazushia uongo mwingi.

Katika kufanikisha hilo, kikundi hiki cha wanasiasa kimeamua kuyarejesha mitaani baadhi ya magazeti ambayo kimekuwa kikiyatumia kupika propaganda zao za kizushi na kifitini kama njia ya kueneza sumu za kisiasa, lengo likiwa ni kuwahadaa Watanzania.

Sambamba na hilo, kwa malengo hay ohayo ya kujipanga upya, kikundi hiki cha wanamtandao masalia kimefikia hatua ya kuwarejesha katika ulingo wa habari baadhi ya wana habari wanaowaamini kwamba wanao uwezo mkubwa wa kutengeneza hoja nzito wakitumia kalamu zao kutengeneza habari kwa malengo ya kipropaganda (spinning) .

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wanasiasa wa kundi hili wanafanya hivyo leo wakisahau kwamba, baadhi ya wanahabari hao, tayari wameshaanza kutambua mchele ni upi na pumba ni zipi na hivyo kurejea kwao katika kipindi kifupi kijacho kunaweza kuwa tukio litakalowaumiza wao wenye zaidi kuliko kuwasaidia. Tusubiri tuone haya yakitokea.

Wakati wataalam hao wa fitina wakijipanga kuchukua hatua hizo wananchi waliosambaa katika maeneo mbalimbali nchini, nao wanaonekana kuguswa na upepo mkali wa mabadiliko na hivyo nao kujikuta wakiwa na kiu ya kufanya kile ambacho kimefanywa na wenzao wa Tarime.

Upepo huu wa mambo ambao sina shaka hata kidogo kuamini kwamba una nguvu kubwa zaidi kuliko ilivyo kwa mikakati ya kujipanga ya kundi hili jipya la mtandao masalia, unayo nafasi kubwa ya kutujengea taifa jipya, lenye matumaini mapya mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kujulikana.

Unabii wa kisiasa ninaouona katika hili ni kwamba, katika kipindi kifupi au kirefu huko tuendako, kabla ya mwaka 2010, Rais Kikwete ambaye hadi hivi sasa ameendelea kujaribu kutofungamana na kundi lolote kwa uwazi ndani ya CCM na serikalini atalazimika kuachana na hulka yake hii ya kutofungamana na upande wowote na kuungana na wananchi kwa maelfu wanaolilia mabadiliko na neema aliyowaahidi mwaka 2005.

Ni wazi kwamba kabla hajafikwa na maono hayo mapya, Kikwete atalazimika kuyakubali mabadiliko kwa kuanza kuitakasa ofisi yake ili ichukue sura halisi ya utakatifu wa ikulu uliopaswa kuwapo pale.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 5:09 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Tumefika pabaya, neema yaja
Tumefika pabaya, neema yaja


Na Absalom Kibanda



NAANDIKA makala hii leo hii wakati taifa likipita katika kipindi cha kukata tamaa kwa upande mmoja na wakati huo huo kukiwa na kufufuka kwa hali ya matumaini kwa upande mwingine hususan kwa makundi kadhaa ya watu wanaoamini wameanza kuzika ufu wa kitaifa uliolikabili taifa hili kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Matukio ya hivi karibuni kabisa, ya migomo ya walimu, kufungiwa kwa miezi mitatu kwa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI, serikali kukimbilia mahakamani kuwazuia walimu kugoma, ya wananchi wa Chunya kuurushia mawe msafara wa Rais Jakaya Kikwete na ushindi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Tarime ni mambo ambayo ama yanaeleza namna watu walivyokata tamaa au waliovyoanza kufufua matumaini yaliyoanza kutoweka.

Katika yote hayo jambo moja ni dhahiri nalo ni kwamba, tupende tusipende, tukubali au tukatae, ahadi na mbwembwe nyingi za viongozi wetu ambao wamekuwa wakitembea kifua mbele wakitamba kwamba, wamelifanyia mema mengi taifa hili, hata kustahili kuenziwa kwa maneno, kalamu na kura ni mambo ambayo yanafurahisha genge zaidi kuliko kujenga misingi ya kuondokana na umaskini ulioota mizizi.

Ushahidi wa hayo ni rahisi kabisa. Miaka 45 na ushee baada ya uhuru majigambo ya viongozi wetu kutamba kujenga kilomita nyingi tu za barabara za lami na za kokoto, kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu na sifa nyingi nyingine zinazofanana na hizo ni mambo ambayo yameshindwa kulinusuru taifa hili na fedheha ya ufukara uliokithiri, maradhi yasiyokoma na ujinga usiomithilika.

Mambo makuu matatu ambayo Serikali ya Kwanza ya Tanzania (1961-1985) iliyaainisha kuwa maadui wakuu watatu wa maendeleo; ujinga, maradhi na umaskini yameendelea kubakia vidonda ndugu kwa taifa hili.

Leo hii ninalazimika kuyakumbuka na kuyarejea mahojiano aliyofanya Rais Kikwete na jarida la NewAfrican (soma toleo la Juni mwaka jana) kuhusu dhamira ya serikali yake kufanikisha mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE) baada ya kubaini kuporomoka kwa maelezo yanayoonyesha kuwa suala hilo ni jipya sana hapa nchini.

Wakati Kikwete akisema UPE ya zama zake imeingiza masomoni asilimia 96 ya watoto wote wanaopaswa kuwa darasani, ukweli ni kwamba kiwango kama hicho au zaidi yake kilipata kufikiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwishoni mwa miaka ya 1970.

Ukiuweka kando ujinga, adui mwingine maradhi naye pia amekuwa tatizo kubwa kabisa linalokuwa. Ukiuweka kando ukimwi, maradhi kama kifua kikuu, malaria na kipindupindu ambayo leo hii yanaundiwa mikakati mipya na ya kila jina kukabiliana nayo, yamekuwa katika kuta za maandishi maeneo mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35 sasa pasipo kupatiwa ufumbuzi. Nani halijui hilo!

Wakati ukimwi ukiwa sababu mojawapo ya kurejea kwa kasi kwa kifua kikuu, ukweli wa kitakwimu unaonyesha kwamba, ugonjwa huo kama yalivyo hayo mengine (malaria na kipindupindu) yameendelea kuwa sugu yakichagizwa na umaskini mkubwa unaolikabili taifa hili.

Leo wakati viongozi wetu wakipiga mbinje kujivunia matunda ya utawala wao, kwa miaka hiyo yote baada ya kuambiwa kuwa tuko vitani tukikabiliana na umaskini, Watanzania tunaendelea kuwa miongoni mwa mataifa sita maskini zaidi duniani. Kwa maelezo yoyote yale hii ni aibu na fedheha.

Kwa bahati mbaya sana, wakati baadhi yetu tukitambua kuwa Watanzania, kuanzia kwa viongozi wao hadi kwetu wananchi wa kawaida, tunao wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya, baadhi ya wenzetu, kwa sababu wanazozijua wao wameamua kudhihaki juhudi hizo na sasa wanavinyoshea vyombo vya habari kidole eti vinaendekeza ufisadi kama vile hakuna masuala mengine ya muhimu. Kwao vita dhidi ya ufisadi ni wivu, majungu, chuki na hadaa, hawa ndiyo wale ambao wamefikia hatua ya kuipa rushwa jina zuri.

Uamuzi wa baadhi yetu kuwakosoa viongozi fulani wasio waadilifu, kufichua baadhi ya maovu yao hata kama hayana harufu nzuri katika pua zetu na sura nzuri macho yetu, kuwakumbusha wajibu wao, na kukemea inapobidi kwa lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora tukitumia kalamu zetu, unaonekana kuwa ni wa kipuuzi na usiolitakia mema taifa hili. Siku hizi wanasema tunataka nchi hii isitawalike.

Viongozi wa serikali wanaokosolewa kwa makali na uzito unaolingana na ukubwa wa makosa yao, wameanza kugeuka mbogo. Wanashambulia kila mmoja anayeonekana kujaribu kuhatarisha madaraka yao ambayo, badala ya kuyaona kuwa dhamana na wajibu wa kuwatumikia wananchi wameyageuza kuwa mtaji wa ulaji wa aina ile ambayo Augustine Mrema alipata kuuita ‘ya kula bila kunawa.’

Kile ambacho, mchambuzi mmoja maarufu wa masuala ya kisiasa alipata kukiandika akiwataja baadhi ya watu kuwa ni mamluki wa viongozi wa dola, ndicho kinachoonekana kutokea hivi sasa.

Maelfu ya Watanzania wanaosoma safu hii, wanapaswa kutambua kuwa, huko tuendako, kalamu kali dhidi ya ukiukwaji wa uongozi bora unaofanywa na baadhi ya watu wenye madaraka ndani ya CCM na katika serikali zake zinaweza kukabiliana na dhoruba kutoka kwa mamluki wanaojulikana na ambao wameamua ama kujibebesha au kubebeshwa ukibaraka wa kifikra. Tayari baadhi ya mamluki hao wameshaanza kujitutumia ingawa ni bahati mbaya sana kwamba Mungu amewapa kisogo. Wasome alama za nyakati.

Lakini pia, viongozi hao hao kwa kadri inavyoonekana, wameshaanza kujipanga tayari kukabiliana na jambo lolote lile linaloelekea kufanana na wimbi la upinzani kutoka kwa wazalendo wa kweli wa nchi hii na tukio la kufungiwa kwa MwanaHALISI ni moja ya mikakati ya namna hiyo.

Matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Tarime yaliyokipa ushindi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya ubia haramu uliokishirikisha CCM na vyama vingine viwili vya upinzani ni kielelezo cha namna Watanzania wanavyoanza kuonyesha waziwazi kuchoshwa na hadaa za kisiasa za watawala wetu.

Ni jambo la kheri kwamba, hayo yaliyotokea Tarime yamekuja wakati huu, tena katika kipindi ambacho viongozi wetu watatu wakuu wa kitaifa, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wakifanya ziara za kupishana ama angani au ardhini wakizunguka kutoka kona moja ya nchi kwenda nyingine huku mara kadhaa wakibebebeana majukumu ya kuwakilishana katika mikutano au ziara za kimataifa.

Waswahili husema, mwenye macho haambiwi tazama, leo hii ninapoandika makala hii, viongozi hao watatu kila mmoja yuko nje ya ofisi yake wakizunguka mikoani kufanya kile wanachojaribu kukifanya kionekane kuwa ni kuhamasisha shughuli za maendeleo ilihali wakijua fika kwamba, kwa uzito wa nafasi zao za kidola, ziara zao ni kitovu kikuu cha matumizi makubwa ya fedha yasiyo ya lazima.

Kwa hakika kabisa, ninaweza nikasema pasipo kutafuna maneno kwamba, mizunguko ya Rais Kikwete, Ali Mohammed Shein na Mizengo Pinda mikoani hivi sasa imesababisha viongozi wa ngazi za mikoa na wilaya wapoteze maana halisi ya kuwapo kwao.

Kwa kweli ni jambo la bahati mbaya kwamba, pamoja na mbwembwe nyingi za ving’ora vya wakuu hao, kauli mbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya imegeuka historia na sasa si yeye rais au wasaidi wake hao wawili wanaoonekana kuwa na ubavu wa kuipigania. Kwa wananchi kama ilivyotokea majuzi mkoani Mbeya, lugha imebakia moja tu; ufisadi, ufisadi ufisadi.

Kile ambacho Jenerali Ulimwengu amepata kukielezea na nikakikariri mara kadhaa kuhusu ‘urafiki wa hatari na uliovuka mipaka kati ya wanahabari na wanasiasa’ ndicho ambacho leo hii tusipokuwa macho, kinaweza kikaivuruga taaluma ya habari yenye wajibu wa kuongoza njia, iwapo tutabebwa na mkumbo wa mambo

Nilipata kuandika kwamba, Kwame Nkrumah angeamka leo hii kutoka kaburini na kufanya tathmini ya kile kinachoonekana kuwa mafanikio ya sera za soko huria na mfumo wa vyama vingi ninao uhakika jina la kitabu chake lisingelikuwa tena; ‘New Colonialism The Highest Stage of Imperialism’ (Ukoloni mambo leo ni hatua ya mwisho ya ubeberu).

Badala yake mwanasiasa na mwanazuoni huyo kwa namna yeyote ile Neo Colonialism ingebadilika na kuwa Neo Liberalism kwa maana ya Udikteta mambo leo ambao watawala wanaoshinda uchaguzi chini ya mfumo haramu wa vyama vingi uliojaa mizengwe iliyokithiri wanavyojaribu kutumia ushindi wao huo kuminya uhuru wa habari, uhuru wa vyama vingi, uhuru wa kufikiri na dhana nyingine za namna hiyo.

Sikuishia hapo nilikwenda mbali zaidi nikasema; Nkrumah angeshangaa kubaini kuwa ubeberu umebadilika. Angestaajabu kuona watawala wa wa Kiafrika wakiwa wamejenga mtandao wa mahusiano ya ajabu kabisa na mabeberu walioupa jina la utandawazi. Mahusiano haya ndiyo yaliyowapa jeuri watawala wetu hata kuwa na jeuri ya kutumia udikteta mambo leo.

Kwa hakika udikteta mambo leo wa watawala wengi wa Kiafrika, umefanikiwa kuihadaa dunia kuwa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa habari, soko huria la kishindani ni mambo yanayofanya kazi pasipo shida yoyote, ilhali hali ikiwa tofauti.

Siyo jambo la siri kwa Watanzania wachambuzi wa mambo kutambua kuwa, udikteta mambo leo wa watawala wetu wanaojivunia ushindi wa kishindo ni matokeo ya wazi ya kazi kubwa iliyofanywa ya kuwanyonga wapinzani kwa fitina za uzushi, sheria ngumu na kandamizi zikiwamo zile 40 ambazo Tume ya Jaji Nyalali ilipata kupendekeza zifutwe.

Ni ukweli unaojulikana wazi kwamba, ushindi wa asilimia 80 ni matokeo ya kazi batili itakayobakia kuwa historia ya nchi hii ambayo ilivigeuza vyombo vyetu vya habari na na baadhi ya sisi wanahabari (Watanzania watusamehe) kuwa taasisi mahususi za uenezi za CCM.

Ni jambo la ajabu kabisa kwamba, leo hii, ushindi huo wa kishindo wa asilimia 80 ambao badala ya kuwa mzigo na dhamana isiyobebeka ya wajibu wa kuwatumikia wapigakura umegeuka na kuwa jeuri ya kuwasakama na kuwazulia mambo wakosoaji wengi ninaoamini wanafanya hivyo kwa nia njema kabisa.

Ujinga wa sisi Watanzania tulio wengi kuendelea kuuona mfumo wa vyama vingi kuwa eti msingi wa kusambaratika kwa umoja wetu, na dalili mbaya za kutoweka kwa amani na utulivu, tukitahadharishwa kuwa makini tusije tukafikwa na yale yaliyowahi kuwafika wenzetu wa Rwanda, Burundi, Kongo, Sierra Leone na kwingineko una sehemu kubwa katika ushindi huo wa asilimia 80.

Hivi Watanzania tumesahau kwamba, asilimia 80 ya watu ambao walipiga kura ya maoni wakitaka mfumo wa chama kimoja uendelee mbele ya Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1991 na 1992 ndiyo matunda ya ushindi wa CCM leo hii ambayo viongozi wake wanapita kifua mbele wakiwakebehi wachambuzi wa mambo wanaoikosoa serikali leo hii kwa kuwapa majina mabaya na hata kuwatenga na mema mengine yote wanayostahili.

Kwa hakika viongozi wetu hao wanapaswa kutambua na kujilazimisha kukubalia ukweli mchungu kwamba, filimbi iliyolia Tarime hivi majuzi na matukio mengine ya fadhaa wanayokabiliana nayo mitaani ni ushahidi wa wazi wa ujio wa Tanzania yenye neema ambayo inaweza ikajengwa na wale ambao leo wanaonekana wasaliti, wapiga domo na watu wasio na maana. Huko ndiko tuendako.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 5:03 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Monday, October 13, 2008
Tuna chembechembe za udikteta wa Mugabe
jpkhxTunazo chembechembe
za udikteta wa Mugabe

Na Absalom Kibanda


NIMEGUSWA na mambo makubwa mawili au matatu hivi yaliyotokea katika siku za karibuni ndani na nje ya mipaka yetu.

Tukio la kwanza ni kauli rasmi ya serikali iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambayo aliielekeza kwa Rais wa Zimbabwe Robart Mugabe.

Katika tamko hilo, serikali ilieleza kuhusu kuwa kwake na mashaka juu ya hali ya kisiasa nchini Zimbabwe wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Membe katika tamko hilo la serikali alisema Tanzania ilikuwa ina wasiwasi mkubwa iwapo uchaguzi huo ungekuwa ni huru na wa haki, kutokana na matukio na vitendo vya ghasia vinavyoendelea pamoja na matamshi ya viongozi mbalimbali wa serikali.

Katika tamko hilo la serikali, Membe alimkariri Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa, pamoja na urafiki wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Zimbabwe, Tanzania imeshtushwa na yanayoendelea katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

“Rais Kikwete amesema Tanzania ni rafiki mkubwa wa Zimbabwe kihistoria. Na mwaka 1980 walipoanzisha mapambano ya kudai ardhi, tulisimama nao pamoja na dunia nzima inajua. Hivyo inapofika katika suala la ardhi Tanzania ipo pamoja nao, lakini inapofikia kwenye suala la uongozi inaleta shida,” alisema Membe.

Aliongeza kuwa, pamoja na urafiki huo, Tanzania imeshtushwa na ghasia zinazoendelea nchini Zimbabwe, hivyo Kamati ya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), iliamua kila nchi ililizungumze suala hilo kwa nchi yake.

Membe alisema kutokana na hali hiyo, Kikao cha Ushirikiano wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kilikutana Juni 17 mwaka huu, nchini Malawi na kuamua kupeleka waangalizi 380 wa uchaguzi nchini humo, ili kufuatilia uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Juni 28.

Kwa maelezo ya Waziri Membe, taarifa kuhusu mgogoro huo wa Zimbabwe walizipokea kutoka kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Tomaz Salomao, ambaye alitembelea nchi hiyo na kuelezea hali tete ya kisiasa, uchumi na usalama.

Tamko hilo la Membe lilifuatiwa na kuondoka kwa balozi wa Zimbabwe hapa nchini ambalo tayari limesababisha kuibuka kwa minong’ono ambayo juzi ilimfanya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aielezee hatua hiyo kuwa ni kuibuka kwa mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Zimbabwe. Hilo ndilo tukio la kwanza.

Siku chache tu baada ya kutokea kwa hali hiyo, nchini Zimbabwe, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Movement for Democratic Change (MDC), Morgan Tsvangirai alitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro cha urais akisema anafanya hivyo kutokana na kujiridhisha pasipo shaka kuwa, hali ya kisiasa nchini Zimbabwe ilikuwa mbaya kisiasa na kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki.

Uamuzi huo wa Tsvangirai mbali ya kuthibitisha wasiwasi uliokwishaelezwa na Tanzania umedhihirisha na kuweka bayana udikteta wa wazi wa Robert Mugabe ambaye kwa miaka mingi amekuwa akichukuliwa kuwa mwanapinduzi na mzalendo wa kweli wa nchi yake.

Kwa mara ya kwanza, mwenendo wa mambo ndani ya Zimbabwe katika kipindi cha mwaka huu, kimesababisha Mugabe ambaye alikuwa akiungwa mkono na mataifa kadhaa ya Kiafrika ikiwamo Tanzania kwa miaka mingi.

Baadhi yetu tungali tukikumbuka mahojiano aliyofanya Rais Jakaya Kikwete na gazeti la Financial Times la Uingereza na yakachapwa Oktoba 5 mwaka huo huo wa jana wakati akiwa katika jiji la Paris, nchini Ufaransa.

Katika mahojiano hayo, Kikwete alieleza bayana kumuunga mkono Rais Mugabe na akayataka mataifa makubwa duniani kuacha kumnyoshea kidole akisema kwamba, Tanzania ilikuwa ikiamini kwamba Wazimbabwe wenyewe ndiyo watakaokuwa na jukumu la kuamua kidemokrasia hatima ya taifa lao.

Kwa maneno yake mwenyewe Kikwete wa mwaka jana alisikika akisema kwa kimombo; "Tanzania is standing by the people of Zimbabwe, including President Mugabe…We subscribe to the idea of working with them to get a solution, because if you end up condemning and insulting [Mugabe] he will not listen to you. Mugabe is there. He is president; he has been elected. If Tanzania said, 'You are hopeless! A murderer! A violator of basic human rights!' does that remove Mugabe from office? It doesn't."

Kwa tafsiri rahisi Kikwete alikuwa akisema; "Tanzania iko pamoja na wananchi wa Zimbabwe, akiwamo Rais Mugabe. Tunaunga mkono jitihada za kufanya nao kazi ili kupata suluhisho kwani iwapo mtaishia kumlaumu na kumdhihaki Mugabe hataweza kuwasikiliza. Mugabe yupo pale.Ndiye rais aliyechaguliwa. Kama Tanzania itamwita mtu aliyepotea njia, muuaji, na mkiukaji wa haki za msingi za binadamu sidhani kwamba maneno hayo yataweza kumuondoa madarakani.”

Kimsingi msimamo huo wa Kikwete juu ya Mugabe ndiyo ule ule ambao ulikuwa ukichukuliwa kwa miaka yote na Benjamin Mkapa wakati huo akiwa Rais wa Tanzania katika kipindi chote cha miaka 10.

Mkapa anakumbukwa kama kiongozi mmoja wa Afrika aliyesimama bega kwa bega na Mugabe akimtetea kwa nguvu kubwa ndani ya Jumuiya ya Madola, katika makongamano ya kisiasa na kiuchumi ya kimataifa na hata alipokuwa akizungumza na wanahabari ndani na nje ya nchi.

Si hivyo tu, Mkapa alipata kuandika makala nzito akimuelezea Mugabe na kutoa msimamo kuhusu Tanzania kumuunga mkono Mugabe dhidi ya kile kilichokuwa kikionekana kuwa ni ubeberu wa mataifa makubwa ya magharibi dhidi ya ustaarabu wa Kiafrika na wa watu wa Zimbabwe.

Kwa Mkapa, kama ilivyokuwa kwa Mugabe, wapinzani wa MDC walikuwa si lolote bali vibaraka wa mataifa ya magharibi ambao wametumwa si kwa lengo jingine bali kuwarejesha wakoloni wa Kingereza katika ardhi ya Zimbabwe kupitia mlango wa nyuma. Msimamo huo ndiyo unaotumika leo kuhalalisha udikteta wa Mugabe dhidi ya upinzani nchini mwake.

Katika sehemu kadhaa za makala yake kwa kuhusu Mugabe na Zimbabwe Mkapa aliandika yafuatayo: kwanza aliyaonya mataifa makubwa kuhusu hatari ya wao kuwachagulia Waafrika marafiki na akasema pasipo kusita kwamba, Mugabe hakuwa tu rafiki wa Tanzania bali komredi yaani mwenzi katika harakati.

Hakuishia hapo alikwenda mbele zaidi na asema, Tanzania itaendelea kusimama pamoja na Mugabe akisisitiza kuwa, kama rafiki Watanzania watashikamana na Wazimbabwe wakati wa amani na wakati wa shida pia.

Leo hii maneno hayo ya Mkapa yanazidi kupoteza maana yake halisi. Mugabe anazidi kuwa dikteta kwa gharama kubwa za maisha ya wananchi wa taifa lake ambao hivi sasa wanakabiliwa na vitanzi vingi vya hali ngumu ya kiuchumi, kijamii na kiusalama.

Ni wazi kwamba Watanzania wengi ambao miaka mitatu au mine hivi walikuwa wakimuona Mugabe kuwa mwanamapinduzi wa kuigwa wa Afrika na mzalendo wa kweli wameanza kubadili mtazamo wao na kwa hakika Mkapa angepewa fursa ya kuandika makala leo hii kuhusu Zimbabwe huenda asingerejea yale aliyoyaandika wakati huo.

Mwenendo huo wa mambo ndiyo ambao sasa umezaa ajenda mpya na ya aina yake ndani ya Bunge la Zimbabwe, ikianzishwa na Zitto na kupewa baraka zake na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Katika hoja yake, Zitto anaeleza bayana kuguswa na hali ya mambo nchini Zimbabwe na hata kuitaka Tanzania ifikie mahali itoe tamko lake kuhusu mustakabali wa hali ya mambo nchini humo chini ya uongozi wa Mugabe.

Hata hivyo wakati Watanzania ambao wakati fulani tulipata kumuunga mkono na kumuona Mugabe kuwa shujaa wetu na mfano wa viongozi makini wa Afrika, leo hii tunapogeuka nyuma tunalazimika kabla ya kumnyoshea kidole mwenzetu kujiangalia wenyewe na kujipima iwapo kweli tunao ubavu wa kuwakemea wenzetu.

Ninapotafuta jibu la swali hili, ndipo ninapojikuta nikirejea kuliangalia tukio jingine lililotokea juzi jioni bungeni mjini Dodoma wakati Waziri Mkuu kivuli wa kambi ya upinzani bungeni, Dk. Willibrod Slaa alipokuwa akisoma hotuba yake kujibu hotuba ya bajeti iliyosomwa asubuhi ya siku hiyo hiyo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Katika hali isiyotarajiwa na ambayo ni kielelezo cha udikteta wa kimya kimya wenye malengo yanayofanana na yale ya Mugabe ya kuendelea kubakia madarakani kwa gharama zozote zile, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liliamua kutorusha moja kwa moja hotuba hiyo ya Dk. Slaa.

Tukio hilo la aibu kwa serikali na TBC limekuja wakati huu wakati shirika hilo likiongozwa na Mkurugenzi mwenye uzoefu wa kimataifa, Tido Mhando ambaye uteuzi wake unahusishwa moja kwa moja na uswahiba wake na Rais Jakaya Kikwete, rais aliyeingia madarakani akitajwa na kupambwa kuwa kipenzi cha vyombo vya habari.

Ni wazi kwamba, serikali na TBC viliogopa kishindo cha hoja za Slaa ambaye hotuba yake iligusa eneo nyeti la ufisadi katika maeneo takriban yote serikalini ambayo Februari mwaka huu ilimuondoa madarakani Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine kadhaa.

Udikteta wa juzi wa kuwanyima fursa Watanzania kumsikia Slaa akisoma hotuba yake ni kielelezo cha hofu ya Pinda kuelemewa na uzito wa hoja za wapinzani, ni kipimo cha kupwaya kwa serikali, ni dalili za Pinda kuogopa kuporomoka na kimsingi ni dalili za wazi za serikali hii inayojidai kumnyoshea kidole Mugabe leo kuwa na chembechembe zile zile za ukandamizaji, uonevu, unyanyasaji dhidi ya haki za msingi za raia kupata habari.

Tukio la juzi dhidi ya wapinzani linapaswa kuwa darasa muhimu kwa vyombo huru vya habari kuanza kujipanga upya kwa ajili ya kukabiliana na udikteta unaofanana na ule wa leo hii nchini Zimbabwe unaotumiwa na Mugabe kukandamiza uhuru wa habari nchini mwake.

Kwa hakika huko tuendako, akina Pinda na wenzao serikali watapaswa kukaa mguu sawa wakijiandaa kukabiliana na uamuzi wa pamoja wa wamiliki wa vyombo huru vya habari ambao siku moja isiyo na jina watakataa kuchapisha magazetini au kuripoti katika redio na televisheni matamko, maamuzi au hotuba rasmi zao rasmi. Mgomo huu uko njiani unakuja.

mwisho
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 8:35 AM | Webu Unganishi | Maoni 1
CCM imeiteka vita ya ufisadi
CCM imeiteka vita ya ufisadi

Na. Absalom Kibanda


UJUMBE wangu naouandika leo hii unakwenda kwa Watanzania wenzangu, hususan wale ambao ni waadilifu si kwa matendo yao tu bali hata fikra zao.

Hili ninaloliandika leo, linalenga kuwaeleza wananchi wenzangu namna ninavyowaangalia viongozi wanaotutawala leo hii ambao kwa bahati kabisa wamefanmikiwa kushika madaraka makubwa kabisa ya kidola ama kupitia katika serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilicho madarakani au Bunge.

Kimsingi uamuzi wa kuandika makala hii leo nimeufikia kwa tabu sana, kwani kwa mara ya kwanza imenifanya nikijuke nilikalizimika kujenga hoja yangu kwa kuwaangalia watu kama msingi wa kujenga hoja ili kufikisha ujumbe niliokusudia.

Siku zote pamoja na ukweli kwamba watu na hususan viongozi wamekuwa wakionekana kuchukua msingi wa hoja ninazojenga, ni dhahiri kwamba wao wamekuwa ni vyombo tu kama si madaraja ya kufikisha kile ninachokusudia.

Hata hivyo pamoja na kupata shida kubwa kufikia uamuzi huo, nimejikuta nikilazimika kuendelea na makala yangu, hasa baada ya kujiridhisha kwamba, watu hawa ninaotaka kuwajadili ni wazito katika taifa letu na kimsingi ni watu ambao kauli zao, uongozi wao na maamuzi wanayofikia yana nafasi kubwa ya kubadilisha mwenendo wa mambo kitaifa.

Kikubwa kilichosababisha nifikie uamuzi huo ni jeuri inayoanza kuonyeshwa na baadhi ya viongozi wa dola dhidi ya watu wengine kwa sababu tu ya kulewa sifa ambazo wakati mwingine huzibeba hata wasipostahili.

Leo hii, vita dhidi ya ufisadi ambayo imeshamirishwa kwa njia ya maandishi ya wanahabari hasa wa magazeti na wale wanaotumia mitandao ya intaneti, huku ikichombezwa na kuungwa mkono na wabunge wachache wa upinzani, imegeuka na kuwapa thawabu wasizostahili viongozi ama wa serikali, CCM na hata Bunge.

Miongoni mwa viongozi wanaobeba sifa hata wao kuanza kuonekana kuwa ndiyo mashujaa dhidi ya vita hivi vya ufisadi ni pamoja na Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa nchi..

Wa pili katika orodha yangu hiyo yuko, Samuel John Tegeza Sitta ambaye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, watu hawa wawili kwa nafasi zao za kimadaraka ndiyo ambao kwa namna moja au nyingine leo hii wameaanza na wanaendelea kuonekana kuwa vinara wa kweli wa vita hii takatifu.

Lakini mbali ya hilo, ni jambo la hatari kwamba, mmoja kati ya viongozi hao wawili, huku akijua kuwa anaungwa mkono na baadhi ya majemedari wa kweli wa vita dhidi ya ufisadi, ameanza kwa sababu tu ya hulka yake ya kibinafsi kuibinafsisha vita hii na kujibebesha sifa nyingi ambazo aghalab nyingine hastahili.

Kutoka nje ya mstari kwa kiongozi mmoja kati ya hawa wawili ndiko ambako leo hii kumesababisha nijikute nikilazimika kuwakumbusha Watanzania wenzangu, wazalendo wa kweli kuanza kukaa macho na kuufuatilia utekaji nyara huu wa ajenda kwa jicho la karibu na la tahadhari zaidi. Nitaanza na Sitta.

Samuel John Tegeza Sitta

Huyu ni mwanasiasa machachari ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mtu ambaye ninaweza kusema pasipo kusitasita kuwa, ameandika historia pekee tangu akiwa kiongozi wa juu wa Bunge.

Ni ukweli usiopingika kwamba, katika kipindi cha miaka miwili na nusu tangu awe Spika, Sitta amefanikiwa kulijengea heshima ya pekee Bunge kutokana na namna alivyoweza kusimamia kwa umakini mkubwa baadhi ya masuala mazito.

Kwanza Sitta anaweza akatajwa kuwa ni spika aliyesaidia sana kuliongezea meno na nguvu Bunge akiliweka katika mstari sahihi wa kimaamuzi na kulijengea taswira ambayo haikupata kuwapo siku zilizopita.

Uzito wa maamuzi kama lile la kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza utata katika mkataba wa Richmond ni ushahidi mmoja wa tu wa mafanikio ya uspika wa Sitta ambayo kwa kiwango kikubwa yalimjengea heshima ya pekee ndani na nje ya Bunge.

Matokeo ya Kamati hiyo teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe ambayo ni pamoja na kulazimishwa kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha yamemfanya Sitta aonekane shujaa wa kipekee ndani ya Bunge.

Richmond kwa upande mwingine imemfanya Sitta aonekane na achukue sura ya kuwa mpambanaji dhidi ya vitendo vya kifisadi ndani ya chama chake na pengine serikalini. Huu ni ukweli unaopaswa kuheshimiwa.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, ushujaa huu wa Samuel Sitta umefikia hatua ya kumvimbisha kichwa hata kumfanya aanze kutembea kifua mbele na kujiona kuwa ni mtu asiyetaka kuguswa.

Leo hii ni kosa kubwa na baya kabisa kumgusa au kumkosoa Sitta. Ushahidi wa maandishi unaonyesha bayana kabisa kuwa, wanahabari waliopata kumgusa mwanasiasa huyo tangu alipojitwalia ushujaa katika Kashfa ya Richmond wamejikuta wakipewa majina mabaya kabisa na wakati mwingine wakihusishwa na kundi la mafisadi.

Hivi karibuni, mwandishi mmoja wa habari wa Tanzania Daima Jumapili; Charles Mullinda alifanya ‘kosa’ kwa kujua au kutojua, kwa makusudi au kwa bahati mbaya akamgusa Sitta sehemu mbaya kwa kuandika makala moja dhidi yake.

Kwa namna ya ajabu kabisa, ukosoaji huo dhidi ya Sitta umechukua sura ya pekee. Wabunge na waandishi kadhaa wa habari wamesikika wakieleza namna Sitta alivyoshtushwa na makala hiyo hata kuiunganisha na kile alichopata kukielezea kuwa ni ‘siasa za majitaka’.

Kwa namna ile ile alivyopata kufanya wakati zilipoandikwa taarifa kuhusu tuhuma za kutumia isivyofaa fedha na mali nyingine za Bunge, Sitta amesikika safari hii chini chini akihusisha upinzani huo wa hoja dhidi yake na ajenda ya mafisadi kumchafua. Huu ni upuuzi.

Leo hii Sitta kwa sababu ya kile kinachoweza kuonekana kuwa ni jeuri inayotokana na matokeo ya vita dhidi ya ufisadi amegeuka na kuwa mtu anayeweza kusema lolote baya dhidi ya watu wengine na akaaminika na hata kuonekana kuwa ni msema kweli. Hali hii lazima ifikie mwisho.

Hivi sasa kwa sababu ya jeuri hii, maofisa wa Bunge wanaomuona Sitta kuwa shujaa wao wa vita dhidi ya ufisadi ambayo Tanzania Daima ina kila sababu ya kutembea kifua mbele cha kupambana na tatizo hili kabla spika huyo hajatiwa ‘wakfu wa ushujaa zama za Kamati ya Mwakyembe’ wamefikia hatua ya kuwaogopesha wanahabari kutomgusa mkuu wao wa kazi.

Jakaya Mrisho Kikwete

Huyu ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Nchi. Ana madaraka makubwa kabisa ya kimaamuzi.

Yeye ndiye kiongozi ambaye kwa kujiamini alimteua Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu wakati akiingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2005 na kirahisi akakubali kung’oka akihusishwa na sakata la Richmond ambalo kitendawili chake Kikwete ameshindwa kukitegua.

Hakuna shaka kwamba, Richmond, mama wa tuhuma za ufisadi wa Serikali ya Awamu ya Nne kama ikiangaliwa kwa umakini inaweza ikazaa jibu la swali la miaka mingi la ni ubora gani akina Sitta, Lowassa, Rostam Aziz, Nazir Karamagi, Emmanuel Nchimbi na wengine wengi walikuwa wakitusadikisha juu ya Kikwete ambaye hakuna shaka alishindwa kuimudu sakata hii, miezi mingi kabla ya kuliyumbisha na kulitia hasara taifa.

Maneno ya majuto aliyoyatoa siku alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam akikiri kwa kinywa chake mwenyewe kwamba kulikuwa na uzembe wa kutochukuliwa kwa hatua za haraka kudhibiti mambo ni ushahidi kwamba, matokeo ya ufisadi wa Richmond yalimkuta akiwa usingizini.

Ukimya wa JK wakati majemedari wa mtandao wakiparurana wenyewe kwa wenyewe kulikoanza baada ya Lowassa kuangushwa ni ushahidi mwingine unaopaswa kutufanya wanahabari kwa upande mmoja na wanasiasa wa kambi ya upinzani kwa upande mwingine kutambua kuwa, vita dhidi ya ufisadi haijapata kuwa ajenda ya dhati ndani ya CCM na serikali yake.


Uamuzi huu wa Kikwete kuwa shabiki au mtazamaji katika vita dhidi ya ufisadi umesababisha wanamtandao wenzake waliosambaratrika kila mmoja kwa mtazamo na njia yake kuchukua mkondo anaoona unafaa.

Hulka hii ya JK kuacha maji yachukue mkondo wake, imemjengea heshima katika jumuiya ya kimataifa na miongoni mwa Watanzania wengine ambao wanakiona kitendo chake cha kukubali kuwaacha maswahiba wake akina Lowassa, Rostam, Karamagi, Msabaha, Andrew Chenge, Zakia Meghji wabebe wenyewe mizigo ya tuhuma mbalimbali za kimaamuzi, kifisadi au kiutendaji kuwa ni uungwana na ya kuheshimu matakwa ya kijamii ya wakati.

Aidha maamuzi yake kama yale ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, hayati Daudi Ballali, kuunda Kamati ya kufuatiliwa kashfa ya EPA, kuwatema katika Baraza la Mawaziri watu kama Meghji, Ngasongwa na wengine ni kipimo cha uwezo wake wa kuongoza katika misingi ya uadilifu na kutoyumba.

Kama hiyo haitoshi, uamuzi wake wa kuunda Kamati ya Kuchunguza Malalamiko ya Wananchi kuhusu Mikataba ya Madini wakati taifa likiwa katika kilele cha malalamiko tena akimjumuisha mwanasiasa wa upinzani Zitto Kabwe aliyeitikisa serikali kwa hoja ya Mkataba wa Buzwagi mwaka jana, ni sehemu nyingine iliyomjengea JK uhalali wa kuruka vikwazo vya ufisadi.

Sambamba na hilo, kauli nzito alizopata kuzitoa siku zilizopita kama zile za; ‘urais wangu hauna ubia’ na ile ya ‘kutenganisha biashara na siasa’ ni sehemu tu ya mambo ambayo yamepata kumjengea taswira ya kiongozi asiyekuwa tayari kufanya kazi katika dimbwi la uchafu hata kama uchafu huo unaofanywa na swahiba au ndugu yake wa karibu.

Ukiweka kando hayo, uamuzi wake au wa serikali anayoiongoza wa kuwaruhusu wapelelezi wa kimataifa wa SFO kutoka nchini Uingereza kuingia nchini na kuwahoji ikiwa ni pamoja na kuwachunguza baadhi ya viongozi ndani ya serikali yake, ni sehemu ya mambo ambayo imeifanya jumuiya ya kimataifa kumuona Kikwete kuwa askari nambari moja wa vita dhidi ya ufisadi.

Kwa maneno rahisi kabisa, maamuzi, kauli na baadhi ya matendo ya kimyakimya na ya wazi ya Kikwete ni mambo yaliyomfanya aweze kujihalalishia ujemedari katika vita dhidi ya ufisadi ambayo kimsingi haikuanzishwa moja kwa moja na serikali yake au yeye mwenyewe.

Hata hivyo, kushindwa kwake kujenga nidhamu ya kiwajibikaji ndani ya serikali, ikiwa ni pamoja na kutochukua kwake hatua za wazi dhidi ya watuhumiwa wa kweli wa ufisadi ni sehemu ya mambo ambayo kimsingi yanaanza kutoa ushahidi kwamba, vita dhidi ya ufisadi ilimkuta kwa bahati mbaya akiwa ofisini na yeye akaihalalisha kwa kufuata upepo wa wakati.

Mbali ya hayo yote, kukaa kwake kimya pasipo kueleza ukweli kuhusu kile anachokifahamu kwa undani juu ya Richmond, EPA, kauli za kitatanishi na viongozi kama Sitta na wengine ndani ya chama na serikali anayoiongoza ni sehemu ya mambo ambayo inawafanya Watanzania nikiwamo mimi kutilia shaka umadhubuti wake, kama Mwenyekiti wa CCM. Rais na Amiri Jeshi Mkuu.

Wanahabari ambao katika hili tunapaswa kutembea kifua mbele tunapaswa kutambua kuwa Kikwete akiwa rais mwenye mamlaka makubwa na jemedari mkuu ndani ya CCM ameshindwa kuonyesha kwa vitendo ni kifanyike na hatua gani za wazi zichuliliwe katika kuimarisha vita hii.

Kwa sababu hiyo basi, huko tuendako sisi wanahabari tutapaswa kuachana na siasa za majitaka za akina Sitta, Rostam, Lowassa, Kikwete na wengine za kila mmoja kujiona bora kuliko mwingine, wakati huu taifa linapopita katika kipindi kigumu kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kimsingi katika hili tunazo sababu za wazi za kutambua kuwa, vita hii dhidi ya mafisadi, ikiachwa ikaendeshwa na akina Kikwete na Sitta watu wenye malengo yao ya kimadaraka, basi itafanywa katika mtindo wa kutafutana ubaya kwa malengo ya kisiasa na wala si kwa nia ya kulinusuru taifa hili siku zijazo.

Kwa sababu hiyo basi, sisi wanahabari tunapaswa kutambua kwa dhati kabisa kuwa, neno ufisadi ndani ya CCM lina maana tofauti kabisa na ufisadi ambao Profesa Issa Shivji, Profesa Mwesiga Baregu, hayati Profesa Seth Chachege na wanazuoni wengine wanauzungumzia.

Leo hii wanasiasa wakongwe na maskini ndani ya CCM ambao kwa miaka nenda miaka rudi wamekuwa mabingwa wa kufuja fedha za umma kwa ulevi wa kupindukia, starehe za kukufuru, na kwa kuwahonga vimada wanaowatunza katika maeneo takriban yote nchini ndiyo ambao leo hii kwa sababu tu ya kuchanganyikiwa kiakili (frustration) wanakuwa mstari wa mbele kuwanyoshea vidole wenzao wa umri wao ndani ya chama hicho tawala waliotumia muda wao mwingi kujiimarisha kimapato na wakitumia vyema kila shilingi wanayopata kihalali au isivyo halali.

Katika hili, ukichunguza kwa makini utabaini kwamba ndani ya CCM wale wanaowanyoshea wenzao vidole vya ufisadi wanafanya hivyo si kwa sababu ya uadilifu wao bali kutokana na ufukara wao na wakati mwingine kwa sababu za magomvi binafsi.

Ni jambo la fedheha kwamba, wakati baadhi yetu tukiuona ufisadi kuwa vitendo vinavyohusisha matumizi mabaya ya madaraka, kufuja fedha na mali ya umma, rushwa za kisiasa na kimadaraka, wizi na ubadhirifu, kwa wana CCM wa leo, kitendo cha mtu kula ofisini kwake hata kama ni kwa rushwa, ni jambo halali na yeyote anayepingana na hilo ana wivu wa kijinga na roho ya kimaskini. Huko ndiko wanakotaka tuende.
Mwisho
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 8:12 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
CCM inahitaji ujasiri wa ANC
CCM inahitaji ujasiri wa
ANC kumweka sawa JK


Na Absalom Kibanda

WIKI iliyopita ilimalizika kwa matukio makubwa mawili ya kisiasa ambayo yote yalimgusa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ambaye kesho anahitimisha kipindi chake cha urais kilichokatishwa.

Tukio la kwanza lililomgusa kiongozi huyo wa moja ya mataifa makubwa ya Afrika likiwa na nguvu kubwa ya kiuchumi, ni lile la kuhitimishwa kwa mazungumzo magumu ya kutafuta suluhu ya kisiasa katika nchi ya Zimbabwe ambayo aliyasimamia na kuyaongoza katika mazingira ambayo kimsingi yalikuwa magumu na yenye mabonde na milima mingi.

Watu wanaofuatilia siasa za Zimbabwe ni mashahidi wazuri wa namna Mbeki alivyoweza kuhimili vishindo vya upinzani mkali ama kutoka kwa Rais Robert Mugabe au mpinzani wake Morgan Tsvangirai kwa nyakati tofauti.

Mbali ya kupata changamoto hizo kutoka kwa viongozi hao wawili, kwa kiwango kikubwa, Mbeki aliweza kuhimili vishindo vigumu kutoka kwa mataifa makubwa mawili duniani ya Uingereza na Marekani ambayo yalikuwa yakifuatilia kwa karibu mustakabali wa mambo ya ndani ya Zimbabwe wakati wote wa kipindi cha mazungumzo.

Kimsingi katika sura ya siasa za kimataifa na hususan za ukanda wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Mbeki aliweza kujipambanua kuwa kiongozi madhubuti na mtu aliyeweza kumaliza mgogoro ambao kwa kiwango kikubwa na kwa muda mrefu uliwagawa viongozi wengi wa Kiafrika wakiwamo marais wawili wa Tanzania, Benjamin Mkapa na baada yake Jakaya Kikwete.

Ni bahati mbaya sana kwamba, hata kabla wino wa furaha yake ya kufanikisha muafaka wa kisiasa wa Zimbabwe haujakauka, Mbeki akajikuta akiwa katika mazingira magumu ya kisiasa ndani ya nchi yake na hususan katika chama tawala anachokiongoza.

Kwa namna ambayo haikutarajiwa, Mbeki akajikuta akikamatwa na kile ambacho Baba wa Taifa Mwalimu Julus alipata kukisema wakati alipoamua kujiuzulu uenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuyakabidhi madaraka hayo kwa aliyekuwa rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi.

Katika hotuba yake aliyoitoa wakati huo, mwaka 1990, Nyerere alisema ni jambo la hatari kwa nafasi za urais wa nchi na ile ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama tawala kushikiliwa na watu wawili tofauti na mambo yakaenda sawasawa.

Kwa maneno yake mwenyewe, Baba wa Taifa alisema ili mambo yasiharibike katika mahusiano ya namna hii ni; ‘kuomba watu hao wawili wapatane.’

Alichokisema Mwalimu ndicho hasa kilichomkuta Mbeki Afrika Kusini hasa kutokana na ukweli kwamba, akiwa rais wa nchi, madaraka ya juu ya urais wa chama tawala cha African National Congress (ANC) yako mikononi mwa hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Jacob Zuma.

Kwa maelezo mengine na kwa kuzingatia utabiri wa kisiasa wa Mwalimu, kuanguka kwa Mbeki mwishoni mwa wiki iliyopita kulianza siku ile ile wanachama wa ANC walipomchagua kwa kura nyingi Zuma kuwa rais wa chama hicho.

Kulikuwa ni dalili za mwanzo za kuanguka kwa Mbeki hasa kutokana na ukweli kwamba, hadi wakati wakiingia katika mchuano huo wa madaraka ya juu ndani ya chama hicho tawala cha ukombozi nchini Afrika Kusini, wanasiasa hao tayari walishakuwa ni mahasimu wakubwa.

Kwa hakika kuanguka kwa Mbeki akilazimishwa kujiuzulu na chama chake mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kiwango kikubwa ni tukio la pili linalompeleka mwanasiasa huyo katika muanguko wake katika siasa za nchi yake baada ya kushindwa katika mchuano wa urais wa ANC.

Ni jambo la bahati mbaya kwa Mbeki kwamba, chama ambacho kilimpa tiketi ya kwenda ikulu kimekataa kuyatambua na kuyaenzi mafanikio aliyoyapata katika medani za diplomasia ya kimataifa, siku chache tu kabla ya tukio hilo.

Uamuzi wa ANC, chama ambacho kimekuwa kikijipambanua kama chama rafiki na CCM kwa miaka mingi tayari umeacha maswali na vigingi miongoni mwa makada wake kutokana na hali hiyo ya Mbeki kulazimishwa kujiuzulu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, (NEC).

Pamoja na mgogoro huo mpya ndani ya ANC ambayo baadhi ya wadadisi wa mambo wanaanza kuingiwa na hofu ya kutokea kwa mmegeko wa ndani kwa mfano wa ule uliotokea miaka ya 1960 na kuzaa chama cha PAC, bado ni ukweli kwamba, hali hiyo ya mambo imefungua ukurasa mpya wa siasa za kistaarabu ndani ya ANC yenyewe na nchini Afrika Kusini kwa ujumla.

Ustaarabu tunaouona hapa ambao wana CCM wanao wajibu wa kujifunza na kuukubali ni ukweli kwamba, hakuna mto yeyote ndani ya nchi, akiwamo rais aliye na mamlaka yanayozidi nguvu za chama chake na matakwa ya msingi ya watu walio wengi.

Sisi ambao siku zote na hususan kipindi hiki tumejikuta tukiwa mashabiki wa hoja inayohimiza kumeguka kwa CCM, tukio la mwishoni mwa wiki nchini Afrika Kusini ni kielelezo cha utayari wa viongozi wa chama tawala wa pande zinazopingana kuwa tayari kukabiliana na changamoto za kisiasa kwa kuweka mbele maslahi ya kitaifa kwanza badala ya kuyaangalia na kuyang’ang’ania yale ya kimataifa.

Leo hii kitendo cha wanachama na viongozi wa ANC kusimama kidete na kuyaweka kando mafanikio ya Mbeki katika diplomasia ya kimataifa yaliyomwezesha kuwaketisha chini Mugabe na Tsvangirai kwa sababu tu ya kuangalia kwanza mustakabali wa nchi yao, kinapaswa kuwa somo zuri kwa wana CCM ambao siku zote wamekuwa vinara wa kuyatumuia masuala ya kimataifa kama kinga yao ya msingi.

Ile hulka ya wanachama wa CCM, kumlinda Mkapa kwa hoja kwamba ameliletea sifa kubwa taifa letu katika masuala ya diplomasia ya kimataifa katika nyanja za kiuchumi, biashara na siasa haina budi kupewa uzito iwapo tu mafanikio hayo yanakwenda sambamba na uhalali wake katika masuala yanayogusa maslahi ya moja ya ndani ya nchi kwanza.

Wana CCM wanao wajibu wa kujifunza hilo pia hata kwa Rais Kikwete ambaye katika siku za hivi karibuni ametokea kutumia mafanikio yake katika masuala ya diplomasia ya kimataifa kama kivuli cha kuficha udhaifu wa kimaamuzi na kiutendaji ama wake binafsi na wakati mwingine serikali yake.

Tabia iliyojengeka ndani ya CCM ya kumpima Kikwete kwa kigezo cha namna alivyoweza kujenga ushawishi wa kumleta nchini na kumfanya aikubali Tanzania, Rais wa Marekani, George Bush haina budi kukomeshwa na tukio la hivi karibui la wana ANC, ambao wamekuwa wakijitambulisha kuwa marafiki wa karibu.

Ni wazi kwamba, wana CCM wa karne ya 21 wameendelea kuwa ni wale wale wa TANU na ASP wa kusifia na kushangalia hata masuala yanayojieleza waziwazi kuwa kielelezo cha udhaifu wa Rais Kikwete binafsi kwa namna ya kujenga propaganda za kusafisha kila aina ya uchafu wakitumia mafanikio Bandia ya diplomasia ya kimataifa.

Ni ajabu kwamba, wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambao wanaona waziwazi namna mwenyekiti wao na rais anavyoshindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kitaifa katika masuala mbalimbali muhimu kama yale yanayohusu mustakabali wa wafanyakazi, wanafunzi, wanasiasa wenzake ndani ya CCM na serikalini bado wao hao hao ndiyo wanaokuwa watu wa mwanzo kuandaa propaganda za kumsifu na kumpamba.

Leo hii wana CCM hao hao na tena si wale wa mitaani bali wajumbe wa CC na NEC za chama hicho tawala wamekuwa mabingwa wa kulalama chini kwa chini wakieleza kusikitishwa na kufadhaishwa na rais wao na serikali yao, ilhali ndani ya vikao vyao vya ndani wamekuwa mabingwa wa kufunga midomo na kutozungumza lolote.

Kumbukumbu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba, baadhi ya wana CCM tunaowaona kuwa ni mabingwa wa kujenga hoja kali dhidi ya serikali ndani ya Bunge na wakati mwingine wanapozungumza na wanahabari kwa siri au kwa uwazi hao hao ndiyo wamekuwa wa kwanza kufunga midomo yao wakati wa vikao ama vya CC au NEC.

Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa, na ulionekana waziwazi wakati wa kikao cha pamoja kati ya wabunge wa CCM na wajumbe wa NEC kilichofanyika Dodoma hivi karibuni chini ya uenyekiti wa Kikwete ikiwa ni miezi michache kabisa baada ya matukio ya bungeni ya Februari yaliyomuondosha madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Wakati wa kikao hicho, kile ambacho baadhi yetu tulikitarajia kukisikia kutoka kwa akina Samuel Sitta, Anne Kilango-Malecela, Christopher ole Sendeka na wabunge wengine ambao ndani ya Bunge wamejipambanua kuwa majemedari wa vita dhidi ya ufisadi hakikusikika wala kuonekana kumtikisa Kikwete aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Kama hiyo haitoshi, jeuri kama hiyo hiyo ya uwazi na ukweli ilishindwa kusikika kutoka kwa watu wa kariba ya Benjamin Mkapa, Edward Lowassa, Rostam Aziz na wana CCM wengine ambao ama wao wenyewe au watu wanaowaunga mkono wamekuwa wakisikika wakilalamika kuchezewa rafu kusingiziwa na kuzushiwa mambo ambayo wamekuwa wakipita kutuaminisha kuwa hayawahusu.

Aidha kati hali hiyo hiyo, hakuna mwanasiasa mmoja kutoka katika kundi lolote kati ya hayo ambayo hakuna shaka kwamba yako katika mvutano mkubwa aliyeweza kusimama na kutaka kusikia kwa uwazi kauli ya Kikwete mwenyewe ambaye kila siku minong’ono inayosikika kutoka kwa wapambe na wanasiasa wa makundi hayo imekuwa ikimuweka ama upande wa watuhumiwa wa ufisadi au ule mwingine wa majemedari wa vita dhidi ya uchafu huo.

Kwa hakika wana CCM na hususan viongozi wa kitaifa walikuwa na wajibu wa kuhakikisha wanaujua kwa uhakika kabisa msimamo wa rais kwa ufasaha kuhusu masuala yote makubwa yanayogusa mustakabali wa taifa kama yale ya Richmond, EPA, tuhuma dhidi ya Mkapa, Andrew Chenge na wengine wengi ambao aghalab ni makada muhimu wa kihistoria ndani ya chama hicho tawala.

Badala yake wana CCM wa leo tena wanaotokana na makundi tofauti kabisa kimtazamo ndiyo hao hao ambao wamekuwa tayari kwa gharama kubwa kuficha aibu zozote zile za serikali kwa njia ya kuandaa maandamano ya kupongezana hata katika masuala ambayo ushahidi unaonyesha waziwazi kupwaya kwa uongozi wa kitaifa.

Matokeo ya hali hii ndiyo ambayo yanamfanya Rais Kikwete leo hii atembee kifua mbele akiwa hana hofu yoyote ya kulazimishwa kujiuzulu kabla ya muhula wake, hata baada ya kuwapo kwa ushahidi kwamba, mtazamo wake kuhusu kile alichokiita mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar unapingana na ule wa wajumbe walio wengi wa NEC na pengine CC anayoiongoza.

Matokeo hayo ya unafiki wa kisiasa wa viongozi ndani ya CCM ndiyo ambao umewafanya wana mtandao wenzake ambao tunaambiwa wanakerwa na jinsi alivyoshughulikia suala kama lile la Richmond lililomlazimisha Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu kubakia wakipiga majungu ya chini chini na kumnyoshea jemedari wao vidole pasipo kuchukua hatua zozote za msingi na za wazi za kumsuta. Ni nani atawaamini?

Matokeo ya udhaifu huu wa kuishi katika propaganda ndiyo ambao kwa miaka mingi umeendelea kukifanya chama hicho tawala kifikie hatua ya kuwaaminisha Watanzania kwamba, rais aliyepo madarakani anapaswa kuendelea kutawala kwa miaka mitano ya kwanza na kisha akapewa miaka mingine mitano ya pili hata kama kiongozi huyo ameonyesha udhaifu na usanii wa aina ile unaoonekana nchini hivi sasa.

Matokeo ya ujinga huu wa viongozi wa ndani ya CCM wenye dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi, ndiyo ambao unawapa jeuri rais na mawaziri wake kusafiri na kushinda nje ya nchi wakijua kwamba, diplomasia ya kimataifa inayoliweka taifa hili katika ufukara wa kuishi kwa kuombaomba misaada, ndiyo kinga ya kimsingi ya kustawi na kudumu kwao.

Matokeo ya upofu huu ndiyo ambao leo hii unawapa jeuri wapambe na wasaidizi kadha wa kadha wa rais waliopo ikulu kuvitumia vyombo vya habari na wanahabari mamluki kumjengea rais heshima hata katika maeneo ambayo yeye mwenyewe amekuwa msingi wa kunyoshewa vidole na kukosolewa.

Matokeo ya ududumizi huu ndiyo ambao leo hii umewahalalishia viongozi wa CCM na wapambe wao kuwageukia akina Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe, Maalim Seif Sharif Hamad, Dk. Willibrod Slaa na wengine wengi na kuwaona kuwa ni tatizo dhidi ya ulaji wao kwa gharama za kuweka kando, kupuuzia na kujifanya hauoni udhaifu unaoonyeshwa na mamlaka kuu ya nchi iliyopewa dhamana ya kukaa ikulu bure.

Matokeo ya wana CCM kulemaa kwao na kuendelea kuamini kwamba ‘Kikwete ni Mwenzetu na ‘Zidumu Fikra Sahihi za Mwenyekiti’ hata katika masuala ya msingi ndiyo ambayo leo hii yamesababisha chama hicho kupoteza sura yake ya msingi ya chama cha wakulima na wafanyakazi. Kwa hakika huko tuendako CCM itapaswa kujifunza kutoka ANC.

Mwisho
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 7:59 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Friday, January 11, 2008
Kenya leo, Tanzania kesho



JUMATANO ya Desemba 19 mwaka jana, wiki tatu zilizopita, safu hii ilikuwa na makala iliyobeba kichwa cha habari kisemacho; ‘Ipo Siku Tutakesha’

Maneno hayo yalitokana na tafakuri ya kikaragosi cha msanii maarufu nchini, Masoud Kipanya ambaye aliyatumia kutoa tahadhari dhidi ya viongozi wanaopuuzia malalamiko ya wananchi hata katika masuala ya msingi.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, utabiri wa kikaragosi na makala hiyo ya ‘Ipo Siku Tutakesha’ umetimia katika nchi jirani ya Kenya kupitia katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Wananchi wa Kenya ambao miaka yote tangu uhuru wamekuwa wakiwapa ushindi marais walio madarakani, mwaka huu walikataa kasumba hiyo na kama si dhambi ya kupigania madaraka kwa gharama ya uhai wa watu, Mwai Kibaki angeandika historia mpya ya kisiasa nchini humo.

Kwa sababu anazozijua yeye na wale wanaomuunga mkono, Kibaki aliamua kutumia aina mpya ya udikteta, akaendesha mapinduzi ya chinichini na ya kumwaga damu za Wakenya ambao idadi yao ingali haijajulikana sawasawa akajitangaza kuwa Rais wa Kenya kwa kipindi kingine cha pili.

Huku akidhani kuwa kutumia madaraka yake ya urais kuapishwa haraka haraka kunaweza kukamnusuru, Kibaki akaamuru Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwasilisha haraka hati ya ushindi wake ambao haukuhakikiwa na kabla ya hapo akawa amemwita ikulu Jaji Mkuu na akajipa fursa ya kuapishwa, ili kujipatia uhalali.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, juhudi hizo za Kibaki za kujihalalisha kidikteta kuwa rais halali wa Kenya, akitumia vibaya mamlaka ya kikatiba hadi hivi sasa zinaonekana kuendelea kugonga mwamba.

Wananchi wengi wa Kenya ambao sasa wanaonekana dhahiri kuchoshwa na urithi mbaya wa ukabila na ulevi wa kuwakumbatia viongozi wezi wa kura, wameyakataa mapinduzi haya haramu ya Kibaki na wenzake kwa namna mbalimbali.

Huku wakiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, wananchi hao wa Kenya kwa sauti moja, wamefanikiwa kuiinua dunia ya wapenda haki ndani ya nchi hiyo, barani Afrika na kwingineko duniani kuukataa ushindi haramu wa Kibaki.

Nguvu ya umma iliyoshindwa kumnusuru Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF katika uchaguzi wa urais za Zanzibar mwaka 1995, 2000 na 2005 imejidhirisha nchini Kenya na kufanya kazi kuanzia huko.

Matokeo ya nguvu hiyo ya umma ya Wakenya, Kibaki amejikuta kila kukicha akilazimika kuchukua hatua moja mbele kusalimu amri na kutafuta kila aina ya njia ya kukubali yaishe kabla hayajamfika yale yaliyopata kuwafika madikteta wengine wengi Afrika wa kabla yake.

Kwa hakika, iwapo itathibitika kuwa Kibaki na kundi la wenzake wengine lilishiriki katika wizi wa kura ili kujihalalishia ushindi, basi kiongozi huyo na genge lake watakuwa na kila sababu ya kufikishwa katika kizimba cha aina ile ile ya akina Charles Taylor aliyekuwa Rais wa Liberia.

Zipo dalili zinazoonyesha kuwa, Kibaki ameanza kutambua kuwa yuko hatarini kufikishwa mahali pabaya kabisa kutokana na maamuzi yake au ya watu wake wa karibu kuzichezea kura ambazo matokeo yake yamemtia wasiwasi hata mwenyekiti wa tume ya uchaguzi aliyemtangaza yeye kuwa mshindi.

Kibaki analazimika kulikubali hilo kwani idadi ya wabunge wa chama chake cha PNU isiyofikia hata nusu ya wale wa chama cha mpinzani wake mkuu, Raila Odinga ni ushahidi na msingi mkuu wa urais bandia aliovishwa na kuhalalishwa na uapishwaji batili kuwa hatua itakayomfanya ashindwe kuitawala nchi hiyo.

Ni jambo la bahati njema kwetu (kwa maana ya kujifunza) kwamba, leo hii Wakenya kutoka makundi yote mawili yanayopingana wameamua kuja Tanzania na kumuomba Rais Jakaya Kikwete asaidie kuwasuluhisha wezi wanaoongozwa na Kibaki na wahujumiwa wanaomuunga mkono Raila.

Wakati Kikwete akiombwa kuwa msuluhishi, kazi iliyokwishaanza kufanywa kabla yake na akina Desmond Tutu na John Kuffor, yeye mwenyewe bado angali akikabiliwa na kishindo kingine cha namna hiyo hiyo cha hapa nyumbani, kilichoanzia Pemba.

Ingawa si rahisi kusema moja kwa moja ni kitu gani hasa kilichowaamsha Wakenya wa pande tofauti hata sasa waanze kumuona Kikwete (kiongozi waliyekuwa wakimpuuza awali) kuwa msuluhishi bora, ukweli ni kwamba uamuzi wake binafsi wa kukaa kimya na kutotangaza kumtambua Kibaki unamweka katika nafasi ya juu, kuliko ilivyo kwa rais mwingine wa Afrika Mashariki, Yoweri Museveni.

Kwangu mimi, usuluhishi wa Kikwete ninauona kuwa ni moja ya mambo ya msingi si kwa Wakenya bali kwetu Watanzania ambao katika mihula mitatu tofauti tumefanya uchaguzi mkuu wa vyama vingi kwa namna ile ile ya hao jirani zetu.

Ninaamini tena kwa dhati kabisa kwamba, Kikwete anaingia katika usuluhishi huo huku akijua kuwa, hata hapa nchini, kilio cha wizi wa kura kimekuwa kikipigwa na wapinzani na kupuuzwa na chama tawala kila kinapopigwa.

Ukiiweka kando Zanzibar ambako kwa viwango vya Wakenya shinikizo limekuwa ni hafifu, katika uchaguzi wa madiwani, wabunge na hata urais, matokeo ya kura yamekuwa yakitoa mwelekeo ule ule wa ushindi wa Kibaki katika maeneo mengi, hata kama si yote.

Tofauti pekee iliyopo ni kwamba, Wakenya wa mwaka 2007, tofauti na ilivyo kwa Watanzania, wameyakataa makosa yao ya 2002 yaliyowafanya wamwamini Kibaki kuwa mtu wa mabadiliko, aliyeaminika kuridhia kwa dhati makubaliano aliyofikiwa na wenzake akina Raila, Kalonzo Musyoka na wengine kabla ya kuundwa kwa NARC.

Rais wetu na sisi wananchi wake tunapaswa kujifunza kuwa, wenzetu Wakenya wa leo, wameukataa ukondoo wetu wa ‘hewala bwana yaishe’ kwa kutoheshimu tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na kutokubali kutishwa na uapishwaji wa haraka haraka wa Jaji Mkuu uliokuwa ukilenga kuzima jitihada zozote za ushindi wa wizi.

Kikwete anapaswa kutambua kuwa, wakati tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na uapishwaji wa haraka haraka wa Rais Amani Abeid Karume ulionekana kumaliza kila kitu mwaka 2005 na kabla ya hapo mwaka 2000, mbinu hizo zimeshindwa kufanya kazi Kenya.

Katika yote hayo, moja ya mambo ambayo Watanzania tuna kila sababu ya kujifunza kutoka Kenya ni kwamba, serikali inayoshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi kwa mfano wa Kibaki, haina budi kung’olewa kwa nguvu ya kura halali na linaposhindikana hilo kwa njia ya wizi, basi nguvu ya umma haina budi kutumika.

Mbali ya hilo, Watanzania wanapaswa kujifunza kuwa, nguvu ya kweli ya upinzani haina budi kutiwa nguvu na wanasiasa wenye nia ya dhati ya kuwatetea watu wa aina ya Raila walio tayari hata kupoteza madaraka yao ndani ya serikali iliyoshindwa, iliyo madarakani.

Katika hili Wakenya wamekuwa watu wa kwanza kutii unabii wa kisiasa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyetabiri kuwa upinzani wa kweli ungetokana na kumeguka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akina Raila, Musyoka na wenzao wamekuwa wana CCM wa kwanza wa Kenya kukiacha chama kilicho madarakani kilichokiuka ilani yake ya uchaguzi kikaitelekeza na kushindwa kuitekeleza kama kilivyoahidi.

Leo hii ndani ya CCM yetu, tunawaona na kuwafahamu kwa majina wanasiasa wakiwamo wale wanaounda Baraza la Mawaziri la Kikwete ambao haikubali visheni yake, wasiokubaliana na mwelekeo wa chama na serikali yao, wanaomkataa na kumpinga chinichini Waziri Mkuu Edward Lowassa ingawa bado wako ndani ya chama hicho hicho.

Wana CCM wa namna hii ambao wanaounda kundi kubwa lenye wanasiasa wakongwe wastaafu na walio madarakani kama wangekubali kukiasi chama hicho ambacho kimsingi kimepoteza mwelekeo wake wa msingi, wangewajengea wananchi matumaini makubwa ya ushindi.

Wanasiasa wa namna hii ndiyo ambao leo hii wanasababisha tushindwe kuwa na akina Raila, Musyoka, Charity Ngilu, Musalia Mudavadi, William Ruto, Profesa Peter Anyang’ Nyong’o na wengine wengi wa aina yao.

Unafiki wa wanasiasa kadhaa ndani ya CCM wenye tofauti za kimsingi za kiitikadi na kimwelekeo na chama hicho tawala, wengi wao wakiwa ni wale wa Tanzania Bara, ndiyo ambao leo hii unaigharimu demokrasia yetu na kuifanya isiyo ya ushindi kwa mfano ule wa Kenya tunayoshinda tukipiga soga kuishangilia na kujifunza kishabiki na si kimatendo.

Katika hili, mafanikio kidogo yamepatikana Zanzibar ambako mwaka 1988 baadhi ya waliokuwa wana CCM waliopata kushika nafasi za juu kabisa ndani ya chama hicho na serikalini, wakiongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Maalim Seif Sharif Hamad walitoa shinikizo zito lililoilazimisha CCM liwafukuze uanachama na kuwavua nyadhifa zao zote.

Kosa hilo la CCM kwa upande wa visiwani ambalo lilirudiwa na Kibaki miaka michache tu iliyopita, ndilo ambalo leo hii linazaa matunda tunayoyaona Zanzibar na haya tunayoyashabikia Kenya ambayo yote na kwa nyakati tofauti jukumu la usuluhishi wake analo Kikwete.

Watanzania kwa ujumla wetu tunapaswa kutambua na kukubali japo kwa uchungu kuwa, hali ya siasa ya leo hii nchini Kenya, ndiyo mtukio ya kesho hapa Tanzania.

Ubabe na udikteta wa siri siri wa baadhi ya viongozi wa juu ndani ya serikali ya CCM ambao umejengewa historia ya kufumbiwa macho ndiyo ambao kimsingi unatujengea mazingira bora yatakayotutengenezea akina Maalim Seif wengine na akina Raila wapya siku miaka michache ijayo.

Hulka za kulindana hata katika masuala yanayogusa maslahi na raslimali za taifa kwa namna ile aliyofanya Kibaki nchini Kenya leo hii, akifikiri kuwa ndiyo ustaarabu wa kisiasa, ndiyo ambazo zitaigharimu CCM hii ya Kikwete au ya mrithi wake miaka kadhaa ijayo. Huko ndiko tuendako.

Mwisho
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 9:49 AM | Webu Unganishi | Maoni 2
Thursday, November 29, 2007
Tumuenzi Kanyama Chiume

Tanzia kwa Mwana wa Afrika

Tujifunze kutoka kwa Kanyama Chiume


NI wiki moja kamili sasa tangu Afrika impoteze mmoja wa majemedari wake wa mwisho na mwasisi wa mapambano ya uhuru na umoja wa kweli wa Afrika, Mzee Kanyama Chiume akijulikana kabla ya hapo kama, Murray William Kanyama Chiume (78).

Mzee Chiume alifariki dunia Jumatano iliyopita akiwa New York Marekani, ambako alikuwa akiishi kwa miaka kadhaa na baadhi ya watoto wake walio huko kikazi.

Kwa hakika kifo cha shujaa huyu wa Malawi, Tanzania na Afrika nzima kinalifanya bara hili kuendelea kupoteza baba mmoja baada ya mwingine wa vita vya ukombozi na waasisi wa mapambano ya umoja wa Afrika.

Kabla ya kifo chake cha wiki iliyopita, Afrika ilikuwa imebakiwa na yeye na Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.

Bila ya kutafuna maneno, viatu vya Chiume vilikuwa vikiwatosha wanasiasa wa kariba yake; akina Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Jomo Kenyatta, Sekou Toure na wachache wengine ambao idadi yao haizidi wanafunzi 12 wa Yesu Kristo.

Wakati Baba wa Taifa alipokuwa ndiye kiongozi wa harakati za mapambano ya uhuru wa Tanganyika miaka ya mwanzoni mwa 1950, Chiume ndiye aliyekuwa kinara nchini Malawi, akiwa ndiye mwakilishi wa chama cha Nyasaland Congress Party kilichokuja kujulikana baadaye kama Malawi Congress Party.

Kupitia katika chama chake hiki, yeye ndiye aliyekiwakilisha katika mikutano ya kimataifa kule London, Accra Ghana na Tanzania.

Alishiriki kikamilifu katika uanzishwaji wa vuguvugu la kudai uhuru kwa pamoja kwa mataifa ya Kiafrika akiwa mjumbe wa Malawi katika mkutano uliozaa lile la nchi zilizo Afrika ya Mashariki na Kati (Pafmeca) kule Mwanza na baadaye Pafmecsa ukijumuisha na nchi za kusini.

Alikuwa miongoni mwa viongozi wa Kiafrika waliokutana mara kadhaa kwa ajili ya kuanzisha uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na mwaka 1964 katika mkutano uliofanyika Cairo Misri, hotuba kali ya kimapinduzi ndiyo iliyomkera rais wake Kamuzu Banda na kumjenga uhasama.

Nilipokutana naye kwa mara ya kwanza, Mzee Chiume alipata kunisimulia kuhusu mzozo mkali wa maneno uliozuka kati ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah ambao ulitishia uhai wa OAU.

Leo hii miaka takriban 10 tangu anieleze kuhusu tukio hilo alilolielezea kuwa ni baya kuliko yote katika uhai wa OAU, bado naweza nikakumbuka kwa ufasaha maneno aliyonieleza.

“Bado naikumbuka siku hiyo vyema kabisa. Ilikuwa ni siku ngumu kwetu. Viongozi wetu wawili, tuliokuwa tukiwaheshimu na kuwasikiliza, walizozana kweli kweli. Mwalimu alikuwa akipinga mtazamo. Sijapata kumuona Mwalimu akiwa amekasirika kama siku hiyo. Ugomvi ule ungeweza kuimega OAU,” alinieleza Chiume aliyekuwa akizungumza Kiswahili kwa ufasaha kabisa huku akivuta tukio moja baada ya jingine.

Katika mazungumzo yake siku zote, Chiume alikuwa akiiona Afrika kuwa moja na mipaka ya kikoloni haikuwa kikwazo cha kuwafanya Waafrika kupigana.

Ninapokumbuka maneno mengi mazito niliyoyasikia kutoka kwa Chiume miaka 1o iliyopita na kupekua pekuwa makabrasha ya historia ya bara hili, kwa mfano wa maneno ya Yohana Mbatizaji, napata shida kuwafunga kidamu za mzee huyo viongozi wa zama hizi wa Bara la Afrika.

Watoto wadogo na Watanzania wasioijua vyema historia ya mapambano ya uhuru wa Malawi na ile ya Afrika ya kati ya miaka ya 1950 hadi 1960 wanaweza wakashangaa, jina la mwanasiasa huyu likitajwa na kuwekwa katika mizania ya wanasiasa wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Chiume na wenzake wengine kadhaa akiwamo rafiki yake mkubwa Henry Chipembere na Orton Chirwa wanaweza wakatajwa kuwa ndiyo viongozi waasisi wa mapambano ya uhuru wa Malawi.

Chiume ambaye miaka ya mwanzoni mwa 1950 alikuwa na umri usiodizi miaka 25 na wenzake zama hizo wakijulikana kwa jina kwa jina la Kiingereza ‘The Young Turks’ (Vijana wasiodhibitika).

Nilipokutana naye katika kipindi cha kati ya mwaka 1996 wakati huo akija hapa nchini mara kadhaa baada ya kurejea Malawi miaka miwili iliyotangulia, nilipata fursa ya kujifunza mambo mengi kuhusu maisha ya mwanasiasa huyu na namna alivyoshirikiana na wenzake wengine katika vita ya mapambano ya ukombozi wa Afrika.

Mzee Chiume alinipa fursa ya kuijua historia ya Malawi, Tanzania na Afrika, nje ya ile tunayosoma katika vitabu na maandiko mabalimbali ya kihistoria.

Ndani ya akili yake, mzee huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 66, alikuwa na kumbukumbu sahihi ya matukio mbalimbali yaliyokuwa yakitokea zama za harakati za kudai uhuru wa nchi yake na ule wa Afrika.

Kwa hakika nikiwa mwanafunzi wa historia zama hizo, mzee huyu aliongeza ufahamu wangu kuhusu historia iliyopotoshwa ya harakati za ukombozi wa bara la Afrika.

Kupitia kwake nilimfahamu Kamuzu Banda, Rais wa kwanza wa Malawi ambaye miaka 30 ya utawala wake wa kiimla, aliiondoa nchi yake kuwa miongoni mwa mataifa ya mwanzo kabisa kudai na kupigania uhuru si wa taifa moja moja la Afrika bali la Afrika.

Kwa maneno yake mwenyewe Mzee Chiume aliniambia kuwa alikuwa akijutia uamuzi wake yeye na mwenzake Chipembere wa kusikia ushauri wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah wa kuwataka wao wamkubali Banda kuwa kiongozi wa harakati zao za ukombozi wa Malawi.

Wakiwa wadogo kiumri, Chiume na Chipembere waliheshimu maoni hayo ya Nkrumah wakihadaika na ushiriki wa Banda katika harakati za mwanzoni kabisa za mshikamano wa Waafrika (Pan African Movement).

Kama ilivyokuwa kwa Nkrumah na kwa vijana hao ambao walikuwa wameshaasisi mapambano ya uhuru wa nchi yao, Banda wa zama hizo, miaka ya 1940 na 1950 alibeba taswira ya kweli ya mwana wa Afrika, mpigania uhuru mwenye uchungu na nchi yake na bara lake.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba, uamuzi wa Banda kuhudhuria mkutano wa kwanza wa Mwamko wa Afrika (PanAfrican Congress) mwaka 1945 kule Manchester, Uingereza akiwa na Kenyatta na Nkrumah ulimfanya aonekane kuwa mmoja wa wanamapinduzi hodari na wa kuaminika wa Kiafrika. Ukweli haukuwa huo.

Mzee Chiume alinieleza namna Banda alivyoweza kutoka ndani ya gamba alilojificha kwa zaidi ya miaka 10, kwnai miezi isiyozidi mitatu tangu Malawi ipate uhuru wake mwaka 1964, ghafla alibadilika na akawa mpinzani mkubwa wa misingi ya ukombozi wa taifa lake na ule wa bara lake.

Akina Chiume walipigwa na butwaa kumuona Banda akitangaza kuutambua utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini ambao ulikuwa umetengwa na jumuiya ya kimataifa na miaka michache baadaye akaingia katika mzozo na Tanzania akigombea sehemu ya ardhi yetu.

Chiume, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje akiungwa mkono na mawaziri wenzake wengine watano, walikataa kumtii Banda, na matokeo yake wakafukuzwa kutoka serikalini.

Hali hii haikuishia hapo, Banda ambaye alishawatangaza kuwa ni wasaliti, akafanya jaribio la kuwakamata na kuwaua, tukio ambalo liliwanasa watu kadhaa na kumkosa Chiume ambaye kwa msaada wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alifanikiwa kutorokea Tanzania.

Kama ilivyokuwa kwa wana mapinduzi wengine kadhaa wa Kiafrika Chiume akarejea Tanzania ambako alisomea na kukulia na akaishi katika kipindi chake chote cha miaka 30 akiwa mkimbizi.

Nilipozungumza naye kuhusu matukio hayo, Chiume alikiri kufanya kosa kubwa la kumruhusu Banda kuziteka nyara harakati zao za mapambano ya uhuru wa Malawi nay ale ya Afrika.

Kwa hakika, kama si hulka yake ya kutopenda madaraka na kuwa tayari kusikiliza ushauri wa wanamapinduzi wenzake, Chiume alikuwa na nafasi kubwa ya kuwa Rais wa kwanza wa Malawi huru na mmoja wa viongozi ambao kifo chake kingewekwa katika daraja moja na akina Nyerere na Nkrumah hata na wale ambao hawakupata kumfahamu.

Wakati nikizungumza naye miaka 10 iliyopita, kulikuwa na maneno ya chinichini yalikuwa yakidai kuwa, Banda halisi aliyechukuliwa na Waingereza na kupelekwa Afrika Kusini na baadaye Uingereza hakuwa yule yule aliyerudi Malawi na kuwa Rais wa Kwanza wa Taifa hilo dogo lililo Kusini Mashariki mwa Afrika.

Nilipozungumza naye kuhusu tetesi hizo, Mzee Chiume alinihakikishia kuwa alikuwa ameshaanza kulifanyia uchunguzi suala hilo na kimsingi alitaka kuandika kitabu juu ya kile kilichotokea Malawi na hadaa ya Banda iliyomwezesha kuupata urais wa Malawi. Sikupata kujua iwapo alitimiza lengo lake hilo.




Amefariki akiwa na mapenzi makubwa kwa taifa lake na kwa Bara lake na ndiyo maana aliporejea nchini mwaka 1994, alianzisha chama cha upinzani akikiita Congress for Second Republic (CSR), akiamini kuwa taifa hili lilikuwa likihitaji uhuru wa kweli.

Tangu wakati huo akawa mstari wa mbele kupigania uimara ya mfumo wa vyama vingi na akatumia muda wake mwingi kuwaasa Wamalawi wenzake kutokubali tena kuirejesha nchi yake katika udikteta wa chama kimoja. Utawala wa mkono wa chumba wa Banda ukampa fundisho kubwa.


Tanzania

Chiume hawezi kutenganishwa na Tanzania. Historia yake ya maisha yake binafsi, kifamilia na kisiasa yanaungana moja kwa moja na taifa hili.

Mwandishi mwenzangu Maggid Mjengwa katika blogu yake ameonyesha kwa ufasaha namna Mzee huyu alivyo na uhusiano na taifa hili. Maggid anaanza kwa kusema;

Huyu mzee alisoma katika shule mbalimbali hapa nchini kuanzia elimu yake ya msingi hadi ile ya Sekondari kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Makerere alikosomea ualimu.

Aidha hata alipokuja kuishi ukimbizini, alioa mke wa Kitanzania akazaa watoto wake akina Nathan na ndugu zake wengine Tanzania. Wamesoma Tanzania na kimsingi wana Utanzania.

Akiwa ukimbizi hapa nchini, Chiume alikuwa akifanya kazi ya uandishia na makala zake za kimapinduzi zilikuwa zikichapwa katika magazeti mbalimbali kuanzia The Nationalist (baadaye Uhuru na Mzalendo) na katika gazeti la serikali la Daily News.


Si hayo tu, hata kabla ya uhuru wa Malawi, Chiume akiwa mjumbe wa Vuguvugu la Kudai Uhuru eneo la Afrika ya Mashariki na Kati (Pafmeca) alitumwa Zanzibar kujaribu kuvusuluhisha vyama vya ZNP na ASP vilivyokuwa katika mgogoro.

Sura ya mgogoro huo wa vyama viwili vya siasa vya Zanzibar ambavyo Chiume alitumwa kuja kuusuluhisha mwaka 1958, una sura inayofanana na ile ambayo leo hii inawaweka katika meza moja viongozi wa vyama vikuu viwili vya siasa CCM na CUF kwa tatizo la Zanzibar.

Mwanademokrasia wa Kweli


Wakati vuguvugu la kudai mfumo wa vyama vingi lilipopamba moto nchini mwake, akifanya kazi kutoka hapa nchini, Chiume hakulala hadi alipounda chama chake na hatimaye kurejea nchini.

Aliporejea nchini mwake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1994, vyombo vya habari vya huko vilikuwa vikimtaja kuwa Mmalawi maarufu kuliko wengine wote waliopata kuishi uhamishoni na mpinzani mkubwa kabisa wa Rais wa wakati huo wa Banda.

Chama chake cha upinzani alichokianzisha cha Congress for Second Republic na jitihada zake za kuviunganisha vyama kadhaa vidogo nchini huko mwaka 1996 ili kukabiliana na utawala wa aliyekuwa Rais wa Pili wa Malawi, Bakili Muluzi ni sehemu ya mambo yanayoonyesha namna alivyoheshimu misingi ya kidemokrasia.

Watanzania tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwa mzee wetu huyu ambaye kuondoka kwake kwa hakika kunaendelea kuwamaliza waasisi wa ukombozi wa mataifa yetu.

Leo hii serikali ya Rais Mbingu wa Mutharika wa Malawi inapokubali kumpa heshima zote za kitaifa Chiume katika mazishi yake, angalau pazia linaonekana kuanza kufunguka.

Hali ya matumaini inarejea na kwa kweli tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwa viongozi wa aina ya Chiume ambao hawakupata kulewa madaraka, ambao kwao Afrika ni taifa moja na ambao kwao uzalendo maana yake moja, kuwapigania, kuwatetea na kuwalinda watu wako.

Watanzania wanaoishi leo hii ni mashahidi wa namna viongozi wetu wengi wanavyofikiria zaidi matumbo yao na yale ya familia zao kuliko watu wanaowaongoza.

Kwa hakika tunapoyaangalia maisha binafsi na ya kisiasa ya wanasiasa wa kariba ya Chiume, tunapaswa kuyafanya kuwa masomo bora ya namna viongozi wetu wanavyopaswa kuishi leo na kesho ili huko tuendako waweke alama za uongozi uliotukuka na wa kuigwa.

Ingawa Chiume amefariki dunia, tunaamini kilio anacholiliwa, na Watanzania, Wamalawi, Waafrika wazalendo na ulimwengu mzima wa wapigania haki ni ushahidi kuwa mema aliyoyatenda yameacha alama ya aina yake.

Kwa hakika kifo chake kimethibitisha Chiume hapaswi kuliliwa kwa kusononeka na kwa kwikwi tu, bali tuna wajibu wa kulia kilio cha kumpoteza shujaa, mwana adhimu wa Afrika, mtetezi wa wanyonge, mpenda haki na shahidi wa mapambano yetu.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 9:27 AM | Webu Unganishi | Maoni 0
Thursday, July 05, 2007
JK, Makamba watuandalia matanga
Na Absalom Kibanda


NATAMANI Watanzania wenye mitazamo inayokinzana pamoja na mitazamo tofauti ya kiitikadi na kifalsafa wangekaa katika meza moja na kukubali kuwa mfumo madhubuti wa vyama vingi vya siasa, vyenye hazina ya wanasiasa wenye upeo, visheni, programu, kauli mbiu na hoja yakinifu, ndiyo siri kubwa kabisa ya kuondokana na wingu la kihistoria la udumavu wa kiakili na kimwelekeo unaolikabili taifa hivi sasa.

Mbali ya kulikubali hilo, Watanzania hao wangeamua kila mmoja kwa wakati wake, kufanya juhudi za dhati na za makusudi kuhakikisha kuwa, mfumo huo mchanga kabisa hapa nchini wenye umri utakaokuwa na umri wa miaka 15 kamili Julai mwaka huu unalindwa na kuimarishwa kwa nguvu zote.

Majukumu hayo matatu ya lazima ya kukubali, kulindwa na kuimarishwa kwa dhati kabisa yanapaswa kuwa ndiyo msingi, dhana na dira ya utawala bora ambao leo hii imebakia kuwa nadharia isiyofanyiwa kazi kivitendo.

Mwanasayansi ya Siasa ajulikanaye kwa jina la Anna Grzymaa-Busse anayendika katika jarida la kitaaluma la East European Politics and Societies la mwanzoni mwa mwaka huu anaandika kwa Kiingereza; Political party competition is critical to fostering good governance and preventing corruption. However, several aspects of competition—the number of parties, their vote share, or their specific ideology—have no demonstrable impact on corruption. In contrast, the robustness of competition is critical in constraining governments and monitoring policy.

Kwa maneno rahisi, msomi huyo anasema; “Ushindani ni jambo muhimu katika kuendeleza utawala bora na kuzuia ufisadi. Hata hivyo ili hilo liwezekane yapo mambo muhimu yanayopaswa kuwapo ili kukidhi ushindani huo- idadi ya vyama, mgawanyo wa kura zao au iwapo itikadi zao, hazina nguvu dhidi ya ufisadi. Kinyume chake, umadhubuti katika ushindani, ni jambo la msingi katika kuichunga serikali na kuzipima sera zake.

Maneno yenye maana hiyo na mchanganuo ulio na mwelekeo huo ndiyo msingi mkuu wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi zote duniani na ushahidi unaonyesha kitakwimu, namna nchi zilizo na mifumo imara ya vyama vingi isiyoingiliwa na nguvu nyingine za nje kama za kijeshi au za kidikteta zilivyofanikiwa kupiga hatua kubwa kabisa kimaendeleo kuliko zile za kiimla.

Kama hiyo haitoshi, mataifa mengi ambayo yameukubali mfumo huo kwa mikono miwili na kustawi kisiasa, kiutawala, kiuchumi na kijamii yameweza kufikia hatua hiyo chini ya mwavuli wa soko huria.

Mwenendo wa mambo katika kipindi cha miaka 15 hadi 20 iliyopita unaonyesha kwamba, hivi sasa chini ya mwavuli huo wa soko huria ndiyo silaha ambayo leo hii mataifa kama China, Korea Kaskazini na Urusi kwa mfano yaliyojiendesha kwa kufuata itikadi ya kidikteta ya kikomunisti yanaonyesha kupiga hatua za haraka kimaendeleo kuliko hata ilivyokuwa kipindi cha vita baridi.

Kwa upande mwingine, mataifa kama Italia, Ufaransa, Uingereza na Marekani ambayo kwa miaka nenda, miaka rudi yamekuwa yakiendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, leo hii yanaendelea kuwa mfano bora wa maendeleo ya katika kila nyanja kijamii, kiuchumi na hata kisayansi na kiteknolojia.

Wakati tukiutambua ukweli huo, Watanzania tukiongozwa na Rais wetu, Jakaya Kikwete tunakubali hata kufikia hatua ya kushangilia wakati taifa hili likipigwa ‘gia ya reverse’ ili tuzidi kuelekea kule walikotokea wenzetu hao miaka zaidi ya 100 na ushee iliyopita.

Kwa namna ya ajabu kabisa, huku tukijua kuwa, kudhoofisha mfumo wa vyama vingi ni jambo la hatari kabisa kwa ustawi wa taifa hili, viongozi wetu, wakitumia ufahamu mdogo wa mambo wa wananchi wanakubali kuhutubia mikutano ya hadhara na kutamba kuwarejesha katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanachama wanaokaribia 1,000 wa upinzani huko Dodoma.

Jambo hili la fedheha kabisa kwa bahati mbaya linafanywa na kusimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye saa chache tu baada ya kutangazwa kushinda uchaguzi mkuu Desemba mwaka jana alikiri kwamba, wengi wa waliompigia kura walikuwa wananchi wasio wanachama wa chama hicho tawala.

Kwa namna ya ajabu na isiyoelezeka kwa akili za kawaida, Rais, eti akitumia kofia yake ya uenyekiti wa taifa wa CCM, anasimama na kuwahutubia wananchi wa Kigoma katika moja ya majimbo machache kabisa ya upinzani na kukiponda hadharani chama hicho na mbunge wake kijana kwa lugha rahisi kabisa ya kukidhalilisha.

Kwa bahati mbaya, chama cha siasa kinachopondwa ni CHADEMA, na mwanasiasa anayejengewa hoja mbaya za kumalizwa tena na Rais kwa mfano wa tembo akimkanyaga sisimizi, ni Zitto Kabwe, mmoja wa wanasiasa wachache vijana wanaoweza kusimama hadharani wakajenga hoja za msingi.

Dhambi pekee ya CHADEMA ni ile jeuri yake ya kuifanya Kigoma kuwa ngome yake kuu, jambo ambalo kwa CCM na Serikali ya Kikwete na wale waliowatangulia kabla yao ni udhia usiopaswa kuvumilika.

Hiki anachokifanya leo hii Rais Kikwete akisaidiwa na akina Yussufu Makamba ndicho kilichofanywa na akina Benjamin Mkapa, Frederick Sumaye na wana CCM wengine ambao nao kwa staili hiyo hiyo waliwahi kuua baadhi ya ngome za upinzani kama mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa bahati njema, wakati ufa ukionekana kustawi kwa upande wa Tanzania Bara ambako makumi ya wanasiasa waliokuwa upande wa upinzani wameweka matumbo yao mbele na kujiunga na CCM, kule Zanzibar hali ni tofauti kabisa, kwani majemedari wa CUF wanao ubavu wa kutembea kifua mbele dhidi ya chama hicho tawala.

Fitna za kisiasa za akina Dk. Salmin Amour, marehemu Dk. Omar Ali Juma, Dk. Gharib Bilal, na baadaye Karume na wasaidizi wake wengine zimeshindwa kuubomoa mtandao imara wa CUF unaoongozwa na vinara wa siasa za upinzani visiwani akina Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohammed, Aboubakar Khamis, Haji Duni, Ismael Jussa na wengine wengi.

Kwa hakika msimamo usitetereka wa viongozi hao wa CUF na wafuasi wao ndiyo ambao leo hii umewafanya CCM tena wakiongozwa na Kikwete huyo huyo walazimike kukaa meza moja na wapinzani hao.

Kwa namna mambo yalivyo, huu moto wa viongozi wa serikali na CCM kuendeleza hulka ya kuvunja ngome za wapinzani, wakifanikiwa Bara na kukwama Zanzibar unaoneka kuchochewa na hulka ya chama hicho tawala kutopenda kukalishwa kwa shuruti katika meza moja na wapinzani kama wanavyofanyiwa sasa na CUF.

Leo hii matunda mabaya kabisa ya moto wa makada hao wa CCM ni kuiua hata kufikia hatua ya kukaribia kuizika ile jeuri ya akina Augustine Mrema, Mabere Marando, James Mbatia na wengine wengi ambao kipindi cha kati ya mwaka 1995 na 1997 walikuwa wanasiasa wanaoheshimika kwa kukitikisa vilivyo chama tawala na serikali yake.

Tunaweza tukasema kwa uhakika kuwa, iwapo majemedari wa CCM wa wakati huo wasingecheza faulo dhidi ya imara ya upinzani iliyoanza kujengwa wakati huo, leo hii kashfa za aina ya ANBEM, ununuzi wa rada na ndege za kifahari na sasa Richmond na mambo mengine yanayofanana na hayo yasingekuwa miongoni mwa matatizo yanayotutesa.

Hilo ndilo ambalo Watanzania tunapaswa kutambua kwamba wakati wakisherehekea kuvishwa skafu za kijani na njano na kupokea kwa mbwembwe kadi za uanachama wa CCM kwa ahahdi za uongozi ndani ya chama hicho tawala au serikalini nyuma ya pazia wanaruhusu kukithiri kwa vitendo vya rushwa na kuifanya serikali iendelee kuwa legelege na hata kupoteza mwelekeo.

Wakati fulani miaka kadhaa iliyopita, nilikuwa miongoni mwa watu niliokuwa nikikiona kitendo hiki cha wana CCM kufanya juhudi za kumaliza upinzani kuwa mchezo wa kawaida tu wa kisiasa ambao ulipaswa kufanywa pia na vyama vya upinzani dhidi ya chama hicho tawala.

Leo hii najiona mwenye bahati kulitambua hilo na kufahamu namna majemedari hawa wa CCM walivyo tayari kucheza rafu za kila aina kuwanyonga wapinzani wao wa kisiasa wanaotoka ndani ya vyama au wakati mwingine wakitokea katika asasi za kitaaluma kama HakiElimu na katika vyombo vya habari.

Je, ni nani aliyetuloga sisi Watanzania hata kuwa kama walivyokuwa Wagalatia ambao pamoja na ‘Mwana wa Mtu’kutupa kila ishara kuwa mfumo wa vyama vingi ndiyo msingi wa utawala bora na mkombozi wa kweli wa taifa hili, sisi bado tunapiga mbio kurudi kule kule tulikotoka.

Hivi ni kwa nini tunashindwa kukaa chini na kujiuliza, ni kwa sababu gani, viongozi wetu walio mabingwa wa kudai kwamba wataenzi falsafa zote za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere waamue kwa makusudi kuukana wito wake wa siku za mwisho za kutaka kuona upinzani wenye nguvu ukijengwa hapa nchini.

Acha historia inihukumu. Jitihada za viongozi wetu, akina Kikwete, Edward Lowassa, Makamba, Tambwe Hizza na makada wengine wa CCM kujaribu kuua upinzani au hata kuudhoofisha kwa kisingizio chochote ni mwelekeo wenye nia mbaya unaolenga kulihujumu taifa.

Baadhi yetu pamoja na ukweli kwamba si makada wala wanachama wa chama chochote kile cha siasa, tunaungana na wanazuoni wa aina ya akina Issa Shivji na wale wenye mawazo kama yake kufanya kila linalowezekana kuukubali, kuulinda, kuuimarisha na mfumo huu wa vyama vingi.

Tunafanya hivyo tukijua na tukiamini kwa dhati kabisa kuwa, tunazo sababu za msingi za kufanya hivyo, tuna nia ya dhati ya kulipigania hilo na mwisho tumeshaanza kujijengea uwezo kukabiliana na hulka mbaya ya majemedari wa vita wa CCM na serikali yake.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 11:14 PM | Webu Unganishi | Maoni 3
Huyu si Kikwete tuliyesimuliwa
Na Absalom Kibanda

MAJIRA kama haya, miaka miwili tu iliyopita taifa hili lilikuwa katika mchakato wa kumtafuta Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ingawa mchakato ulikuwa umeanza, machoni mwa wachambuzi wa mambo wa ndani ya nchi na hata wale wa nje, Kikwete ndiye aliyekuwa akionekana dhahiri kuwa; ‘President in Waiting.’ (yaani Rais Mtarajiwa).

Ingawa katika uchaguzi huo, wagombea wengine wawili wa urais, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema) walionekana kuamsha hisia mpya za kuungwa mkono na makundi kadha wa kadha, bado ukweli ulikuwa ukionekana kuwa walikuwa washindani wa kutoa changamoto na si wa kuchukua jahazi la uongozi, japo kwa wakati ule.

Zama hizo, vyombo mbalimbali vya habari, hususan magazeti takriban yote ya kila siku yalikuwa yakiimba wimbo mmoja zaidi katika kampeni; Kikwete, Kikwete, Kikwete.

Vichwa vya habari kama vile vilivyokuwa vikiandika; Kikwete shujaa!, Hakuna kama Kikwete! Kikwete we acha tu! Kikwete aiteka… na vingine vingi ambavyo kimantiki vilikuwa vikifanana na hivyo, vilipamba kurasa za habari na makala katika magazeti mbalimbali.

Waandishi na wahariri waliokuwa na jeuri ya kuandika kwa kina habari na makala za wagombea wengine wa urais na kufikia hatua ya kuwapamba kwa namna ile ya Kikwete walikuwa wakihesabika na idadi yao ilikuwa ikipungua kadri siku za uchaguzi zilivyokuwa zikikaribia.

Kile ambacho Kikwete mwenyewe hivi karibuni alipata kukiita maandalizi yake ya miaka 10 ya kuwa Rais wa Tanzania yalijipambanua kwa uwazi kabisa.

Kati ya mwezi Machi na Mei mwaka 2005 wakati CCM ikiwa katika mchakato wa kutafuta mgombea urais, wakiwa wamejitokeza wanasiasa 10 kusaka kiti hicho, niliandika safi za makala za kuwachambua wagombea hao wote nikieleza nguvu na udhaifu wa kila mmojawapo.

Kwa sababu ya mwelekeo wa makala yangu ya leo nitanukuu moja ya sehemu muhimu inayoendana na makala yangu ya leo inayomuelezea Kikwete niliyemuweka katika mizania ya wagombea wengine washindani wake. Niliandika hivi.

Ni jambo la wazi kwamba, watu ambao wamekuwa wakimuunga mkono Kikwete, tangu mwaka 1995 wamekuwa wakimuona kama mgombea anayewakilisha mawazo ya kizazi kipya cha Watanzania na mtu anayeweza akawa daraja la mahusiano kati ya wazee wastaafu na vijana wenye uchu wa kutaka kupewa nafasi ya kuongoza.

Pamoja na ukweli kwamba, Kikwete anapogombea hivi sasa ana umri wa miaka 55, vijana na wana CCM wanaoungana na falsafa ya Baba wa Taifa ya kuwataka wazee wang'atuke madarakani wanamuona kuwa ndiye chaguo lao sahihi kabisa la 'wakati huu' pamoja na ukweli kwamba, watu wa rika lake kama vile Frederick Sumaye (55) na Mark Mwandosya (57) wanaonekana kuwa ni wa kizazi kingine na tena waliochomoza kwa bahati mbaya tu.

…Swali moja hadi hivi sasa linaonekana kutojibiwa sawasawa: Ni kwa nini basi miaka 10 baada ya kugombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995, Kikwete bado anaonekana ndiye mwakilishi wa Watanzania wa kizazi hiki na mtu anayeonekana kufaa zaidi kuongoza taifa katika karne ya 21 zaidi kuliko ilivyo kwa wengine kama hao akina Sumaye, Mwandosya kwa upande mmoja na hata akina Malecela, Salim, Iddi Simba kwa upande mwingine.

Je ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya ujana aliyodumu nayo kwa miaka yote 10 tangu mwaka 1995? Ni upofu wa mashabiki zake? Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni mapungufu waliyonayo washindani wake? Ni kitu gani hasa? Watanzania wanapaswa kuliangalia hilo na kulitafutia majibu.

Hicho nilichokiandika Aprili mwaka 2005 ndicho ambacho kweli kilitokea ndani ya CCM. Benjamin Mkapa, akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM huku akiungwa mkono kwa siri siri na majemedari kama Kingunge Ngombale Mwiru, Ali Hassan Mwinyi na Rashid Kawawa (kwa kuwataja wachache) walitumia ajenda za namna hiyo hiyo kumpa ushindi Kikwete.

Siku ilipotoka makala yangu hiyo, rafiki mkubwa wa Kikwete, Rostam Aziz ambaye sasa ni Mweka Hazina wa CCM Taifa alinipigia simu na akaeleza kushangazwa kwake na hoja zangu hususan katika aya hiyo ya mwisho.

Kwa maneno yake mwenyewe; Rostam aliniuliza; “Hivi mdogo wangu Kibanda unaishi katika dunia gani? Kweli hujui ni kwa nini Kikwete ni mgombea maarufu na anayekubalika kuliko mwingine yeyote?.

Kwa bahati mbaya kwangu, hata Rostam mwenyewe hakunieleza ni kitu gani hasa kilichokuwa kikimfanya Kikwete atokee kuwa kipenzi cha Watanzania hata kufikia hatua ya baadhi ya wadadisi wa mambo kama akina Prince Bagenda kumuita Tumaini Lililorejea.

Hata hivyo, mwitikio mkubwa na wa kipekee wa wapiga kura na matokeo ya ushindi wa asilimia 80, yaliyopewa majina anuai, ushindi wa kishindo, kimbunga, el-nino na mengi mengine yaliendelea kumpamba, Kikwete aliyeonekana kuwa mtu wa watu.

Mmoja wa wasaidizi wakubwa wakati wa kampeni za urais wa CCM niliyezungumza naye wakati akiwa katika msafara wa Kikwete mkoani Ruvuma aliniambia kwamba, wengi wanaomuunga mkono Kikwete katika harakati zake, wanamuona kuwa ndiye kiongozi pekee atakayeleta mabadiliko makubwa ndani ya CCM na katika mfumo wa kiutawala.

Msaidizi huyo wa Kikwete huku akiwa amezingirwa na wapambe watu wengine kadhaa waliokuwa ndani ya timu ya ushindi wa mwanasiasa huyo alinieleza, nitamnukuu, ili nisipotoshe maana; “Kikwete ni mpinzani ndani ya CCM, wenzake wengi wanalijua hilo na ndiyo maana baadhi ya watu wanamuogopa wakijua akiingia madarakani atafanya mabadiliko makubwa.”

Leo hii ninaweza nikawaeleza Watanzania wenzangu kuwa, kwa kiwango fulani nilianza kushawishika kuwa JK alikuwa mtu wa mabadiliko na kiongozi ambaye angeweza kuleta mapinduzi makubwa kabisa ya kifikra katika mfumo wa kiutawala.

Ni bahati mbaya sana kwamba, miezi 18 sasa tangu aingie madarakani, matarajio makubwa waliyokuwa nayo watu wengi juu yake yanaonekana ama kutoweka au kutokwenda kama ilivyodhaniwa awali.

Ahadi zake kwamba ari, kasi na nguvu mpya vitakuwa chachu dhidi ya rushwa, uwajibikaji serikalini na hata katika mahusiano ya kisiasa na kijamii na vyama vingine vya siasa na nchi jirani ni mambo yanayoonekana kutokuwapo.

Tunapowauliza vijana wasio na ajira waliojitoa mhanga kumuunga mkono kwa kishindo, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu waliofikia hatua hata ya kumuona mtu aliyekuwa akifuata nyayo za Baba wa Taifa, wadadisi huru wa mambo na wasomi wa kada mbalimbali, jibu utakalopata ni rahisi kabisa; ‘tumeanza kukata tamaa’ ndivyo wanavyosema.

Si rahisi hivi sasa kusema kwa uhakika kabisa iwapo kasi, ari na nguvu inaonekana katika utendaji wa wizara moja moja au hata idara zake, hata baada ya kufanyika kwa milolongo ya semina elekezi na JK mwenyewe kutembelea wizara hizo na idara kadhaa nyeti.

Kile ambacho Waziri Mkuu, Edward Lowassa alipata kukielezea kuwa mwisho wa ‘business as usual’ serikali ndicho kinachoonekana kuendelea kubakia kikistawi serikalini.

Ukiacha tu kwamba, hivi sasa Rais ni Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu ni Edward Lowassa, kasi ya mambo serikalini inabakia ile ile ya zama za Benjamin Mkapa na Frederick Sumaye.

Jambo baya zaidi ni kwamba, kabla ya Mkapa hajaanza kusukwasukwa na jinamizi la maamuzi yake ya kibiashara akihusishwa na mikopo ya benki na kampuni ya ANBEM, midomo ya Watanzania ilishaanza kusema mara kwa mara; ‘ni afadhali serikali iliyopita.’

Ingawa ni kweli kwamba, Kikwete anaweza akatembea kifua mbele akijivunia mafanikio yake na Lowassa katika kuchochea ujenzi wa shule nyingi za msingi na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari katika kipindi chao kifupi madarakani bado sekta nyingine muhimu kama afya, miundombinu, maji, kilimo hazina mifano hai ya kuisemea.

Hivi sasa Watanzania hawawajui mawaziri na naibu mawaziri wa Kikwete kwa majina na kwa kazi za wazi za uwajibikaji wanazozifanya kwa namna tuliyopata kuiona zama akina John Magufuli, Augustine Mrema, Lowassa mwenyewe, Meghji (wa zama zile).

Hali hii ya mambo imetufanya baadhi yetu tuanze kujiuliza je huyu ndiye Kikwete yule yule aliyeungwa mkono kwa kishindo kwa hoja za ushawishi kwamba ataanzia pale alipoishia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere?

Baadhi yetu ambao tuliaminishwa tukubali kuwa Kikwete ni mpinzani wa kweli ndani ya CCM na ‘nabii’ aliyekuja kurejesha heshima iliyopotea ya chama hicho tawala na kuirejeshea msingi wake wa ‘mapinduzi’ leo hii tumeanza kuona ndivyo sivyo.

Wakati tukiona namna Kikwete anavyolemewa na mambo, tumeanza kujiuliza ni kitu gani hasa kinamzuia Kikwete kuchukua hatua dhidi ya mawaziri wake wengi wasindikizaji, wakuu wa mikoa wavivu na wakuu wa wilaya waliolala?

Hivi ni jambo gani hasa linalomfanya ashindwe kuwawajibisha makatibu wakuu na wakurugenzi wa taasisi na idara za serikali aliowateua walioshindwa kusimamia vyema maeneo yao ya kazi.

Ingawa mashahidi na manabii wa uongo wamekuwa wakijaribu kujenga hoja za kumlinda Kikwete na serikali yake kwa sababu wanazozijua wao, ukweli unabaki pale pale kwamba, matarajio makubwa waliyotujengea, yameanza kufifia na tuombe Mungu yasije yakatoweka kabisa.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 11:11 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Serikali ikubali lawama kujiepusha na fedheha
Na Absalom Kibanda

WATANZANIA tunaumwa magonjwa mengi ya kifikra na kisaikolojia ambayo kwa bahati mbaya, matokeo ya kuendelea kuugua huko kusikoisha yamekuwa ni mambo mengi mabaya.

Pamoja na kufanya mambo mengi ya msingi na yasiyo ya msingi, zaidi ya miaka 45 tangu tupate uhuru wetu, Tanzania bado imeendelea kubakia moja ya mataifa masikini kabisa duniani.

Juhudi za viongozi wetu kujaribu wakuu wanne kujaribu kulinasua taifa hili kutoka katika hali mbaya kabisa ya ufukura bado zimeendelea kugonga mwamba, pamoja na kuwapo kwa mafanikio ya hapa na pale.

Leo hii wakati Watanzania tukiwekwa katika majaribu ya kutakiwa kuingizwa kwa kasi zaidi (fast tracking) katika Shirikisho la Afrika Mashariki, sauti kubwa kutoka kwa watu walio wengi ni ile ya kupinga hatua hiyo, tukiwa na hofu ya wazi na kimsingi ya kweli.

Wale wanaopinga kuingia katika shirikisho kwa kasi, wanasema bayana namna wanavyohofia kile kinachoonekana kuwa ni hatari ya Tanzania kugeuzwa koloni la kiuchumi, kisiasa na kijamii la mataifa jirani, hususan Kenya.

Mbali ya hilo, wapinzani wa hoja hiyo hawaishii hapo, wanakwenda mbali zaidi na kueleza bayana kwamba, kuzorota kwa hali ya amani na usalama katika nchi majirani kama vile, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda nchi ambazo ndizo zilizo chini ya wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo siku moja itazaa shirikisho kunaweza kukailetea nchi yetu matatizo makubwa siku zijazo.

Watetezi wa hoja hiyo ambao kimsingi sipingani nao, wanasema bayana namna Watanzania tunavyopaswa kujivunia amani na utulivu tuliyojijengea kwa miaka yote tangu mwaka 1961 tulipopata uhuru wetu.

Tangu zama za uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere (1961-1985) na baadaye Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005) na sasa Jakaya Kikwete, amani na utulivu vimekuwa ni ajenda ya kujivunia na kimsingi ya kuilinda.

Mara kadhaa viongozi wetu wakuu wanapozungumza katika majukwaa ya kisiasa wamekuwa wakiwataka Watanzania kutambua kuwa amani (na utulivu) tunayojivunia leo hii tumeijenga kwa kutumia nguvu kubwa na kwa sababu hiyo basi tunao wajibu wa kuilinda kwa juhudi zote.

Wakati fulani wakati wa midahalo mikali ya hoja katika ukumbi maarufu wa Nkrumah mwanzoni mwa miaka ya 1990, msamiati huu, mara kadhaa ulipatwa kutundikwa msalabani hasa baada ya kundi moja la wanazuoni kuamua kuubatiza jina na kuutita ukondoo uliovishwa joho.

Leo hii wakati tafiti zikiwa zimeshathibitisha kuwa vijinchi kimoja kimoja kama ilivyo Tanzania (haya ni maneno ya Mwalimu Nyerere si yangu) bila ya kuungana na nyingine kichumi haziwezi zikasonga mbele au zikapiga hatua.

Uzoefu wa peke yetu wa miaka zaidi ya 40 ya kusimamia falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea tukijaribu kujenga viwanda vingi kabla ya kujihakikishia malighafi bora na ya kutosha na pasipo kuwa na masoko ya uhakika ya kuuzia mazao yetu na pengine kutokuwa na uwezo wa kuviboresha viwanda hivyo, umetufikisha hapa tulip oleo.

Ile jeuri tuliyokuwa nayo miaka ya kati ya 1961 na 1980 ya kutumia Tan Bond yetu, maziwa na nyama zetu wenyewe za kusindika, viwanda vyetu vya nguo na vitu vingi vingine vya namna hiyo vya kwetu wenyewe, hata kuweza kuonyesha jeuri dhidi ya nchi jirani kama Kenya ambayo tulikuwa tukiiona kuwa taifa kibaraka la mabepari (leo wawekezaji) wa kigeni imepotea na kutugeuka sisi wenyewe.

Wakati tukiwahofia Wakenya hao kuwa watakuja kuumeza uchumi wetu, ukitembea katika maduka yanayouza bidhaa mbalimbali za kutumia majumbani kwetu utashangaa kuona kwamba asilimia zaidi ya 70 ya vitu vinavyouzwa na kuuzika, vinatoka katika nchi hiyo jirani.

Blue Band ambayo miaka ya 1970 haikufua dafu kwa Tan Bond, leo hii imeshika chati na kuuzwa kila duka hata kule ambako kwa lugha ya mitaani leo hii tunakuita uswazi (yaani uswahilini).

Vyakula vya majumbani kuanzia maziwa ya unga kama Nido, vyakula vya watoto kama Celerac, na bidhaa nyingine nyingi zinazopamba maduka mengi zinatoka kati nchi hiyo ya Kenya huku zile zilizobakia zikitokea Afrika Kusini.

Matokeo ya Tanzania kugeuka kuwa soko la bidhaa za nchi hizo mbili, kwa kiwango kikubwa kikubwa yamesababisha Kenya kuishangaa Tanzania na kuiangalia kwa jicho la kutoiamini sana huku wasomi wake wengi wakionyesha waziwazi kuipinga sera ya serikali yetu kuikumbatia Afrika Kusini kwa kutumia mgongo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa mfano ule ule ambao mabepari walilazimika kuigombea Afrika hata kulazimika kuigawa vipande vipande ili kila mmoja apate koloni lake, ndivyo ilivyo sasa kwetu ambako mataifa hayo mawili kila moja kwa namna yake, yanaligombea soko Tanzania.

Mataifa hayo mawili yote mawili kwa namna na njia zinazofanana yamefikia hata hatua ya kufungua mabenki yao hapa nchini, Afrika Kusini ikijivunia kuongoza kwa kuwa nayo mengi kama Stanbic Bank, Barclays Bank na NBC huku Wakenya wao wakiwa na Kenya Commercial Bank.

Wachumi wa nchi hii bado tunawasubiri watupe majibu sahihi wakitufafanulia kwa kina ni wapi tulipoteza mwelekeo hata kufikia hatua ya leo hii kulazimika kukikubali kile ambacho wakati fulani zama za vuguvugu la vita baridi, walimu wa siasa wa zama hizo kama akina Kingunge Ngombale Mwiru walijenga desturi ya kukiita ukoloni mambo-leo.

Wakati tukiendelea kusubiri majibu ya kitaalam kutoka kwa wachumi wetu, bado tunayo nafasi ya kukiri kwamba, viongozi wetu ambao wamejenga hulka ya kutembea kifua mbele wakisema amani na utulivu ni tunda la juhudi zao, wanao wajibu wa kusimama na kuigeuza shilingi upande mwingine na kutamka kwamba, kuporomoka kwa mwelekeo wa mambo ni matunda ya kuweka mbele mustakabali wetu wa kisiasa na kusahau maeneo mengine.

Je, ni haki kwa viongozi wetu leo hii kutuita sisi tunaokosoa sera na falsafa zao kadha wa kadha kuwa ni wapinzani tusio na hoja na ambao hatulitakii mema taifa letu hili ambalo eti lina viongozi wanaofanya kazi usiku na mchana pasipo kuchoka?

Kwa namna yoyote ile, viongozi wa taifa hili, wakiwamo akina Kingunge ambao kwa nyakati tofauti walipata kutuambia kuwa tulikuwa tukipita katika kipindi cha mpito hata wakatuletea mikakati mingi yenye majina lukuki yaliyojaa misamiati yenye mbwembwe nyingi wanao wajibu wa kutueleza ni wapi tulipojikwaa hata tukaendelea kuanguka.

Hata hivyo wakati tukilazimika kugeuka nyuma na kuwanyoshea kidole viongozi wetu, sisi Watanzania pia tunao wajibu wa kujibebesha lawama wenyewe kwa kukubali kwetu kimsukule kuaminishwa kila tulichoambiwa na viongozi hao.

Mbali ya hilo, wakati tukilazimika kukiri kwamba, tulikuwa tumepotea njia hata kama mwelekeo ulikuwa ni sahihi, kila Mtanzania anao wajibu basi wa kuanza kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa ajili ya manufaa ya taifa hili.

Ingawa ni kweli kwamba, tunayo mambo mengi ya kufanya, moja ya mambo ya mwanzo kabisa ni kukubali kuacha ile hulka yetu ya miaka nenda miaka rudi ya kushangilia kila msamiati unaoonekana kusikika masikioni mwetu unaotolewa na viongozi.

Viongozi wetu wa sasa, wanapokuja na lugha za “Kwa Kasi Mpya, Ari Mpya na Nguvu Mpya, Tanzania yenye Neema Tena Inawezekana! Tunao wajibu wa kuipima kauli hiyo kwa kuangalia hali halisi iwapo inaendana na maneno hayo.

Kwa bahati mbaya, leo hii wanapoibuka wachambuzi wa mambo na kuwauliza akina Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu Edward Lowassa kuhusu utekezwaji wa kauli mbio za namna hiyo wanaanza kuonekana wasaliti na wapinzani wa dhamira njema ya viongozi wetu.

Baadhi ya watu katika nchi hii wanataka kutulazimisha tuache kuwakosoa viongozi wetu, wanataka tufikiri kwa namna na mwelekeo wanaoutaka wao na kimsingi wanataka kuendelea kuifanya nchi hii kuwa soko-koloni la mataifa rafiki na jirani.

Huku wakijua kwa hakika kabisa kwamba, viongozi wa CCM na kabla ya hapo wale wa Tanu wamekuwa ni mabingwa wa kutunga kauli mbiu ambazo zimeshindwa kuzaa matunda yaliyokusudiwa, bado wanakubali kuendelea kuukumbatia ujinga wa kushindwa kufikiri kwa kiwango cha ajabu kabisa.

Hulka yetu ya kushabikia kila tamathali za semi, tabia yetu ya kulewa ahadi zenye ladha tamu akililini na desturi zetu za kuwafanya viongozi wetu waungu watu, wasiokubali kukosolewa ilihali wakijua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya kuliongoza taifa hili ni mambo yaliyopitwa na wakati.

Kwa kutambua hilo, napenda kuweka bayana kwamba, tutaendelea kuhesabu na kuzichambua kauli nzito zinazotolewa na viongozi wetu wakuu na kama hiyo haitoshi, tunaziweka katika mizania ya hoja, kauli mbiu zao na falsafa wanazotumia huku tukiamini kuwa, kwa kuwa kwao madarakani, wao ni watumishi wa wananchi.

Viongozi wetu wakuu ambao walikuwa wanyenyekevu kweli kweli wakati wakiomba kura ama za ubunge, urais au zile za kuidhinisha uteuzi wao wanapaswa kutambua kuwa, wale ambao wanawakosoa kwa dhati leo hii wanawaepusha kukumbwa na fedheha siku watakapostaafu au kumaliza mihula yao ya uongozi ama kikatiba au kwa kulazimika. Heri lawama kuliko fedheha.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 11:10 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Lowassa; Kiepuke kikombe hiki
Na Absalom Kibanda


WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa amekalia kaa la moto. Ameshika moja ya nafasi za juu za kimadaraka katika nchi hiyo ambayo inabeba lawama nyingi.

Kwa namna mambo yanavyokwenda Lowassa sasa anaonekana ama ameanza kulitambua hilo kwani kiwango chake cha uvumilivu kwa tuhuma zinazoelekezwa kwake, kwa uwazi na wakati mwingine kwa siri, kinaonekana kuongezeka.

Kwa upande mwingine hicho kinachoonekana kuwa ni uvumilivu kinaweza kikawa pia aina ya ushauri anaopewa Waziri Mkuu unaofanana na ule waliowahi kupewa watangulizi wake.

Iwapo hali hii ya sasa inatokana na Lowassa kutambua ukweli kwamba kazi yake ni ya lawama kiasi kwamba anapaswa kwanza kutafakari kabla ya kufurukuta kwa kasi na kuanza kuchukua hatua, basi, hilo ni jambo jema na kimsingi linapaswa kupongezwa.

Ikiwa ukimya wa sasa wa Lowassa unatokana na ushauri wa wasaidizi wake wanaomtaka akae kimya na kuuacha upepo upulize hadi utakapochoka wenyewe, basi atakuwa anafanya makosa makubwa ambayo atakapoamua kuchukua hatua huenda akajikuta akiwa amechelewa sana na hivyo kukwama.

Hata hivyo wakati Lowassa akitafakari hayo anapaswa kutambua jambo moja la wazi kuwa, uwaziri mkuu, wadhifa alioubeba sasa, una historia ngumu kwa wateule wake.

Akiwa Waziri Mkuu wa tisa tangu uhuru na wa nane baada ya Tanganyika kuwa Jamhuri, Lowassa anapaswa kwenda katika rekodi na kuangalia mustakabali wa kikazi wa watangulizi wake.

Kati ya mawaziri wanane waliomtangulia kabla yake, ni watatu tu, Julius Kambarage Nyerere (1961-1962), Edward Moringe Sokoine na Dk. Salim Ahmed Salim ambao waliondoka serikalini wakiwa majina safi masikioni na machoni mwa wananchi wa kawaida.

Wengine wote waliobaki, Rashid Kawawa, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, John Malecela na Frederick Sumaye, wote kwa vipindi tofauti wakiwa mawaziri wakuu walipita katika hatua ngumu kabisa kiutendaji.

Lowassa akiwa wa mwisho katika mlolongo huo anapaswa kutambua na kimsingi naamini ameshaanza kuliona hilo kuwa, kiti alichokishika kina makali kila upande.

Akiwa mmoja wa wanasiasa ambao uchapakazi wao hautiliwi shaka hata kidogo, Lowassa anatakiwa kutambua kwamba, kina cha maji anachoogelea ni kirefu kuliko ujasiri wake binafsi.

Si hilo tu Lowassa anapaswa pia kutambua kuwa, ingawa yeye ni mteule wa Rais, utendaji wake wa kazi unapimwa si na rais tu, bali mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, wasomi wa kada mbalimbali, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida.

Lowassa anapaswa kutambua pia kwamba, majibu yatakayotokana na mizani itakayowekwa na makundi mbalimbali yanayoangalia utendaji wake ndiyo yatakayokuwa taswira halisi ya utendaji si wake tu bali pia wa serikali kwa ujumla.

Kama hiyo haitoshi, Lowassa anao wajibu wa kutambua kuwa, iwapo serikali ya Kikwete itaanguka katika maamuzi na katika utekelezaji wa programu zake, ndani ya serikali yenyewe na nje, basi lawama za kwanza zitaelekezwa kwake yeye hata kabla ya kufikishwa kwa Rais na mawaziri wengine.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana hata hivi sasa, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa ndani ya nje ya nchi, wakati wanapounyoshea kidole utendaji wa serikali ya awamu ya nne, jina la Lowassa ndilo linaloonekana kurushiwa mawe mengine na makali zaidi wakati mwingine kuliko hata yale anayorushiwa Kikwete.

Leo hii ukipita katika mitaa mbalimbali na ukakutana na wasomi, maafisa wa juu wa serikali, wabunge, wafanyabiashara wakubwa na watu wengi wengine ni jambo la kawaida kusikia jina la Lowassa likitajwa si kwa mema bali kwa lawama ambazo wakati mwingine ukizipima unaziona zisizo za msingi.

Ni jambo la ajabu na la kujiuliza hivi ni kwa nini basi kila maamuzi yenye utatanishi hivi sasa yaliyochukuliwa na serikali, yote tunaelezwa kuwa nyuma yake yuko Lowassa.

Kama ilivyopata kuwa zama za Sumaye, Msuya, Malecela na hata Warioba mwaka mmoja sasa tangu ashike kiti hicho muhimu kabisa, Lowassa ndiye anayebebeshwa mzigo wa lawama kwa kila baya linalotokea hapa nchini.

Leo hii, Lowassa ndiye anayehusishwa na kuchelewa kupatikana kwa mwekezaji anayefaa wa kuchimba chuma Liganga na kuendeleza makaa ya mawe ya Mchuchuma.

Hata Rais Jakaya Kikwete alipofanya mabadiliko ya kumuondoa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa, NDC, taasisi ya umma iliyokuwa ikishughulikia miradi hiyo miwili ya chuma na makaa yam awe, Lowassa ndiye aliyenyoshewa kidole na baadhi ya watu kuwa mtu aliyekuwa nyuma ya mabadiliko hayo ambayo baadhi hayakuwafurahisha.

Ni Lowassa huyo huyo ambaye hivi sasa anahusishwa pia na kuwapo kwa jitihada zenye walakini za kubomolewa kwa baadhi ya majengo yaliyo katikati ya jiji la Dar es Salaam ambayo awali yalikuwa yametengwa kwa sababu za kihistoria.

Naamini baadhi ya watu wanakumbuka vyema namna Mbunge wa Moshi, Philemon Ndesamburo alivyomhusisha Lowassa katika sakata la mgogoro kati ya Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) na Reginald Mengi, ugomvi ambao sasa umechukua sura tofauti kabisa kiasi cha kulifanya suala hilo lichukue sura ya kitaifa.

Ukiunganisha na hilo, ni Lowassa huyo huyo ambaye baadhi ya wabunge wanamtaja kuwa nyuma ya Malima aliyeamua kulihamisha suala lake kutoka katika mtiririko wa masuala ya Bunge na kulipeleka CCM.

Watu wanaomhusisha Lowassa na hilo wanasema mahusiano yake mabaya ya kikazi na Spika wa Bunge, Samwel Sitta ndiyo sababu kuu ya yeye kuamua kuungana na Malima katika jitihada za kumshughulikia mbaya wake. Falsafa rahisi. ‘Adui wa adui yako ni rafiki.’

Tunapowauliza baadhi ya wanasiasa, mawaziri, wabunge wanasiasa ndani na nje ya CCM na wanamtandao wengine, sababu hasa za Lowassa na Sitta kuhitilafiana nje ya genge lao lililomuandalia ushindi Kikwete majibu tunayoelezwa ni ya ajabu kweli kweli.

Lakini kikubwa kinachotajwa kuwa kiini cha mzozo huo ambao hakuna yeyote kati yao wawili amewahi kuuweka bayana ni kile kinachoelezwa kuwa ni ‘Urais baada ya Kikwete.’

Jibu hili wakati mwingine haliniingii akilini, ingawa kwa bahati mbaya huwa nakataa kulipinga, hasa ninapoangalia historia ya utendaji wa kazi wa wanasiasa hao wawili ambao wote kwa miaka 10 iliyopita walipitia hatua mbalimbali za kumuandaa Kikwete kuwa Rais wa Nne wa Tanzania.

Kimsingi jibu hili ndilo ambalo limewahi kumfanya hivi karibuni kabisa mwandishi mwenzangu wa habari, Deodatus Balile kuhoji, iweje nchi hii watu washindwe kufanya kazi kwa sababu ya kuogopa kuhusishwa na ‘urais baada ya Kikwete.’

Hayo ni sehemu tu ya mambo ambayo baadhi ya watu wanayahusisha na Lowassa. Kwa bahati mbaya mengi miongoni mwake ni yaliyo na harufu mbaya.

Nimepata kuyazungumza haya na marafiki zangu na wakati fulani nilipata kuandika makala nikihoji ni siri gani mbaya iliyojificha nyuma ya uwaziri mkuu.

Lowassa anapaswa kulitambua hilo na kimsingi anao wajibu wa kukisafisha kiti hicho alichokalia kwa kukataa kuhusishwa na kila aina ya takataka. Anapaswa kufanya hivyo akitambua kuwa uongo akisemwa sana hugeuka ukweli.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 11:03 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Majungu; Falsafa ya ushindi CCM!
Na Absalom Kibanda

HUU ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kimsingi huu ni msimu wa kuibuka kwa mambo mengi makubwa na madogo yasiyo na kichwa wala miguu.

Waswahili wanao msemo mzuri kabisa unaokwenda sambamba na majira au nyakati. Msemo huu si mwingine bali ule usemao; ‘dalili za mvua ni mawingu.’

Kwa CCM ya zama hizi, limekuwa ni jambo la kawaida kila ukaribiapo msimu kama huu kuanza kusikika na kuonekana kwa matukio ya ajabu ajabu yanayoambatana na vituko vya hapa na pale miongoni mwa wanasiasa wa kada mbalimbali ndani ya nchi hii.

Kwa hakika dalili za msimu mbaya kabisa za ‘wanasiasa kuanza kuvuna kile walichopanda na kupanda kile wanachotarajia kukivuna zimeanza kuonekana waziwazi.

Kwa maneno rahisi kabisa, kupitia katika vyombo vya habari, huu sasa ni wakati ambapo CCM hujipambanua kuwa chama ambacho wanasiasa wake, wakiwamo wale wanaoonekana kuwa hodari kabisa kuanza kushikana mashati, kushambuliana, kukashifiana na kupeana sifa nzuri na mbaya. Kimsingi hapo ndipo tulipo sasa, tukijiandaa kufika tuendako.

Kwa lugha rahisi kabisa, chama tawala kinaingia katika kipindi kigumu kingine kigumu kabisa kinachotawaliwa na majungu mepesi na mazito ya kisiasa ambayo yanaendelea kuyathibitisha maneno ya Profesa Issa Shivji ya hulka ya siku zote ya wanasiasa kupenda madaraka, kuliko kuipenda siasa yenyewe.

Leo hii tunaposoma habari zinazomhusu Amina Chifupa, baadhi yetu tunaishia kuangalia pale alipoangukia mwanasiasa huyo, huku tukisahau kabisa kutupa macho yetu kule alikojikwaa.

Kwa hakika Amina anapita katika tanuri lenye moto mkali kabisa, lililopata kuwakaanga wanasiasa wengi wakongwe katika nchi hii kama akina John Samuel Malecela, Dk. Salim Ahmed Salim, Dk. Abdallah Kigoda, John Pombe Magufuli, Frederick Sumaye, Prof. Mark Mwandosya na wengine wengi wengine.

Amina Chifupa mwanasiasa mwepesi kiumri na mtu anayeonekana kukosa uangalifu katika mambo yake mengi binafsi, pamoja na kutambua kuwa amekuwa ‘target’ safari ametumbukia ndani ya maji ya kina kirefu yaliyopata kuwazoa na kuwamaliza kisiasa kila mmoja kwa kiboko chake wanasiasa hao.

Hakuna shaka kabisa kwamba, watu anaokabiliana nao, wameamua kwa dhati kabisa kumvua joho la ufahari wake kisiasa na kimsingi makosa yake binafsi yanaweza yakagharimu kwa kiwango kikubwa nafasi yake ya kisiasa iwapo hatakuwa makini kukabiliana nao sawasawa.

Amina na wanasiasa wengine wachanga ndani ya CCM wanaojiandaa kwa ajili ya nafasi nyeti za kiuongozi wanapaswa kulifahamu hilo na kutambua kuwa, jitihada za kuwakata miguu ili kuwazuia wapoteze nguvu za kusimama mchuano wakati utakapowadia, ndiyo azma kuu ya wapishi wa fitna hizo.

Ingawa mbele ya macho yetu tunamuona Amina Chifupa, ukweli ni kwamba, katika suala lake la sasa, yeye ni kivuli tu cha mwenendo wa mambo machafu, siasa za kuvutana mashati na falsafa kuu kuu ya majungu na yenye mafanikio makubwa kabisa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

‘Fitna’ mbaya kabisa kisiasa anayojaribu kukabiliana nayo leo na ambayo sasa imempotezea mume huku ikijaribu kusonga mbele na kumpokonya ubunge wake na baadaye kumnyima matunda mengine ya kisiasa inaweza ikamfanya abakie kuwa majeruhi kwa kipindi kingine kirefu kijacho.

Kwa namna yoyote ile magwiji wa mtandao wanaokabiliana na Chifupa wanaoungwa mkono kisirisiri na genge kubwa la maadui wa mwanasiasa huyo wanaomtuhumu yeye kwa kuwahusisha na biashara za dawa za kulevya.

Kwa bahati mbaya sana, miongoni mwa wale ambao wanapinga harakati za kujijenga za mwanasiasa huyo ni wabunge wenzake na wengine ni wanachama wenye madaraka ndani ya CCM wakiwa ama wabunge au wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho tawala.

Kile ambacho kimekuwa kikionekana kuwa ni jitihada za Amina kujijengea jina na kujipatia umaarufu mkubwa hata kuwashangaza baadhi ya watu waliokuwa wakimdharau wakati alipoingia bungeni kwa ‘mlango wa nyuma’ akizishinda jitihada za viongozi wake kadhaa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, sasa kinageuka haraka haraka na kuonekana kuwa uchafu usiopaswa kutetewa.

Jitihada za kumjengea taswira chafu mwanasiasa huyo, inafanana na kile kilichoitwa uziro wa Sumaye, uarabu wa Salim Ahmed Salim, ukabila wa Mwandosya, ukarani wa Mangula, ubadhirifu wa Kigoda na uzee wa Malecela.

Kwetu sisi, watawaliwa, walipakodi, wananchi wa kawaida na umma wa Watanzania tatizo tunalopaswa kuliangalia sasa, si kile kinachoweza kuonekana leo kuwa ni ufuska wa Amina Chifupa unaoweza ukafananishwa na sifa mbaya wanazojaribu kubebeshana wana CCM.

Kimsingi tatizo ni CCM. Mfumo wake wa uongozi na staili ya viongozi wa zama hizi wa chama hicho kukubali kuliongoza taifa hili kwa njia haramu kabisa ya kupikiana majungu.

Iwapo Amina Chifupa anastahili kuvuna kile alichopanda kwa sababu ya kukosa kwake uaminifu katika ndoa yake au hata katika chama chake, bado hilo halitoshi kulifanya taifa hili liwe la watu wanaosubiri mabaya ya wengine kama kigezo cha kuanza kuchafuana.

Wenzetu Wamarekani ambao tumenyofoa mambo kadhaa muhimu katika mfumo wa vyama vingi vya siasa wamefikia hatua ya kuwapima viongozi wao kwa kuangalia rekodi zao za utendaji wa kazi za kisiasa kabla hawajaingia katika nafasi ya uongozi.

Ingawa mfumo wetu wa siasa ya vyama vingi bado ni mchanga kabisa, binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba, CCM, chama kikongwe kuliko vyote, kilipaswa kujijengea mfumo madhubuti wa kuwapata viongozi wake, ambao ungekuwa na uwezo wa kuwaandaa makada, wasomi katika ngazi mbalimbali.

Hii tabia ya chama hicho tawala kujijengea desturi ya kukusanya wanachama kwa mfano wa kokoro linalovua samaki, pasipo kuangalia rekodi za siku za nyuma kisiasa, kijamii na hata kiuchumi za wanachama wake eti tu kwa sababu ya kuwaonyesha jeuri wapinzani, ni moja ya chachu kuu za kujengeka na kushamiri kwa hulka mbaya za majungu yasiyokoma ndani ya chama hicho.

Kile chama chenye heshima ambacho Baba wa Taifa alijaribu kukijenga chini ya mwavuli wa kauli mbiu ya ‘huyu ni mwenzetu’ iliyokuja kubadili maana yake halisi ya awali na kuwa kitovu cha kuwakataa baadhi ya watu makini, leo hii inakitafuna polepole chama hicho.

Taifa linalojaribu kujitoa katika tatizo lililoota mizizi la ufisadi, kamwe haliwezi kupata nafasi ya kujinasua katika jinamizi hilo, iwapo nyufa za namna hii zitaendelea kustawi na kuboreshwa.

Leo hii unaposikia taarifa kwamba, viongozi wa juu kabisa wa kiserikali, wakijiingiza katika mitandao ya kuwabomoa baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara kwa sababu zisizo na maslahi ya kitaifa, unapata picha halisi ya mahali tulipo Watanzania na pengine mwelekeo wetu wa siku za usoni.

Si rahisi kujua ni vikao vingapi vya CCM au Bunge vitakaa na kulijadili suala hili la Chifupa ambalo kwa namna ambayo si rahisi kabisa kuielezea, limepenyezwa kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa njia ya barua ambayo nakala yake anayo Katibu Mkuu wa CCM.

Hivi kweli, viongozi wetu wakuu, wanazo sababu za msingi za kukubali kuingizwa katika mtandao wa majungu ambayo wakati mwingine huwa tunaambiwa huwa yana baraka za viongozi ambao ukiambiwa majina yao na kuangalia nyadhifa tulizowapa unapigwa na butwaa.

Je; baada ya sakata la Reginald Mengi na Mbunge Adam Malima ambalo chimbuko na hitimisho lake ni majungu lililogharimu takriban shilingi bilioni 100 bado Bunge hilo hilo na chama kile kile tawala vina sababu ya kuendelea kujiingiza katika masuala ya kijinga yasiyo na tija?

Hivi kweli tunamtendea haki spika wetu ambaye hivi sasa yuko katika kipindi kigumu cha kulijengea Bunge heshima kwa kuwa na meno ya kujadili mambo yenye tija kitaifa, kuendelea kumuingiza katika masuala ya ufuska ya wabunge wake?

Je, ni sahihi kwa Yussuf Makamba, kumuingiza katika mjadala mwingine wa ugomvi wa Amina Chifupa na mumewe na akaacha kukiandaa chama chake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa ndani baadaye mwaka huu, au hata akaweka kando mazungumzo muhimu anayoyaongoza kati ya chama hicho na kile cha CUF.

Je, ni haki kwa Watanzania wote kujiingiza katika mtego mwingine wa kuwa washangiliaji wa ugomvi wa Mpakanjia na Amina au ufuska wa Mheshimiwa Kabwe na Amina hata kusahau masuala mengine mazito na ya msingi tunayokabiliana nayo?

Kwa namna yeyote ile, Watanzania tunapaswa kuachana na hulka ya kuendekeza majungu kama kweli tunataka kujenga mustakabali mwema wa taifa hili wa siku zijazo. CCM inapaswa sasa kurejea masomo ya maadili kwa viongozi wake ambayo hatimaye yatawarudisha katika mstari wa kusudio la kuasisiwa kwake. Wanahabari tunao wajibu wa kukwepa kuingia katika mtego wa habari za kashfa za ngono kila kukicha wakati nchi hii ikiwa na masuala mengi mengine ya kijamii ya kuyaandikia.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 11:01 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Tuna njaa na kiu ya migomo ya kifikra
Na Absalom Kibanda

LAITI kama Rais Jakaya Kikwete angelijua, asingekwenda katu kuonana na wanafunzi wa vyuo vikuu Diomond Jubilee mwanzoni mwa mwaka huu kwa lengo la kuwapooza na kuwapa ahadi ya matumaini.

Kutokwenda kwake kungetoa fursa kwa wanafunzi hao waliokuwa wamegoma, uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Wizara ya Sayansi, Tekinolojia na Elimu ya Juu na Bodi ya Mikopo kutafakari upya madai ya wanafunzi hao na kuyatafutia majibu yakinifu.

Kwa kuthubutu kwake kwenda, Kikwete alionyesha ujasiri ambao uliwashinda watangulizi wake kadhaa miaka kadhaa iliyopita.

Hata hivyo mkutano wake huo na wanafunzi kwa upande mwingine ulibadili kabisa sura ya mzozo kutoka kuwa wa kitaaluma na kuchukua taswira ya kisiasa.

Kimsingi mkutano wa Kikwete na wanafunzi hao, ambao awali ulionekana kuwapa matumaini makubwa wanafunzi hao, sasa umegeuka na kuchukua sura fadhaa kwa wasomi hao na serikali.

Zaidi ya miezi miwili sasa tangu Kikwete atoe ahadi kwamba serikali yake isingekuwa tayari kuona mwanafunzi yeyote akifukuzwa shule kwa sababu ya umaskini wa wazazi wake, hakuna kilichoonekana kufanyika bayana katika macho ya wanafunzi hao ambao kwa maneno yao wenyewe wanasema aliwaeleza kuwa jibu lao lingekuwa tayari katika kipindi cha mwezi mmoja tangu hiyo Februari 3 alipozungumza nao.

Kushindwa huko kwa serikali kutoa jibu la mapema kwa wanafunzi limetoa matokeo mabaya kabisa, kwani subira ya vijana hao wasomi imekoma na badala ya kuelekeza lawama zao dhidi ya sera mbaya ya mikopo, wamejikuta wakirukia hoja mpya kabisa za uendeshaji wa serikali na hata kuingiza siasa za vyama katika malalamiko yao.

Mabango waliyoyabeba siku moja kabla ya kusimamishwa masomo yao, yote yakidhihaki uundwaji wa serikali, utendaji wake wa kazi na hata kufikia hatua ya kuomba msaada kutoka kwa viongozi wa upinzani, yalikuwa ni matokeo ya mkutano ulioshindwa kuzaa matunda kati yao na Rais Kikwete.

Mabango hayo yamezua maoni tofauti miongoni mwa watu mbalimbali. Wako wanaowaona wanafunzi hao kuwa ni watovu wa nidhamu kutokana na kitendo chao hicho cha kuwakebehi viongozi wakuu wa kitaifa na serikali yake na wako wengine wanaowaona wanafunzi hao kama wasemaji wa kweli wa sura halisi ya serikali yetu.

Watangazaji wawili wa kituo maarufu cha utangazaji cha Clouds FM, Fina Mango na Masoud Kipanya wao wamekuwa wakikielezea kitendo hicho cha wasomi kuwa kinachoonyesha dharau na kinachotoa sura mbaya kabisa kwa viongozi wao.

Hata hivyo walichokifanya wanafunzi hao hakikuwa kipya. Wamefanya kile ambacho kinafanywa na vyuo vikuu vyote duniani hadi hivi sasa.

Ukiangalia katika rekodi mbalimbali, wanafunzi wa vyuo vikuu wanatatizwa na ugonjwa unaotokana na msongamano wa kifikra unajengwa na masomo anuai wanayosoma, ukianzia na falsafa, historia, haki za binadamu na mengi mengine.

Mchanganyiko huo huzaa tafakuri kwa kila kinachopita mbele yake. Hufungua milango ya kupima kila jambo, kulalamikia kila aina ya maumivu, yawe ni madogo au makubwa.

Kwa wanafunzi wa vyuo vikuu duniani. Uvumilivu dhidi ya hujuma ya aina yoyote ni ukondoo na hata subira dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote ni ujinga na kimsingi ni mambo yanayokwenda kinyume kabisa na hadidu za rejea zinazotokana na usomi wao.

Ukifungua katika mitandao ya kompyuta leo, utashangaa utakapoona migomo ya chuo kikuu ikiwa imesambaa katika mataifa mbalimbali duniani ukianzia na yale ambayo ni maskini hadi nchi tajiri kupindukia.

Wingi wa migomo inayotokea katika vyuo vikuu mbalimbali duniani inakwenda sambamba na wingi wa hoja zinazosababisha migomo hiyo.

Kwa sababu hiyo basi serikali inapaswa kutambua jambo moja kwamba, wanafunzi wa vyuo vikuu hawezi kamwe kukosa sababu ya kugoma katika kipindi chochote wakiwa masomoni.

Naamini kwa dhati kabisa kwamba, serikali inapaswa kushukuru kwamba, hivi sasa wanafunzi katika vyuo vikuu vyetu wanasumbuliwa na njaa katika matumbo yao, wanakabiliwa na ukata katika mifuko yao na kimsingi wanaishi maisha magumu kabisa wakiwa vyuoni kuliko walivyopata kuishi ndugu, jamaa na Watanzania wenzao waliowatangulia.

Ufukara wa kimaisha unaowakabili wanafunzi wa vyuo vyetu vikuu, uliochangiwa kwa kiwango kikubwa na sera batili ya uchangiaji wa elimu ya juu, ndiyo msingi mkuu wa malalamiko ya sasa ya wasomi wetu hao.

Lakini jambo baya kabisa ni kwamba, hivi sasa wanafunzi hao wanalalamikia kiu na njaa za matumbo yao, tofauti na ilivyokuwa zama zile ambazo kiu ya fikra ndiyo iliyokuwa chagizo kuu la migomo ya wanafunzi.

Wakati wanafunzi wakijenga desturi ya kugoma wakidai posho zao au kuongezewa fedha katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, wenzao wa zama zile walikuwa wakigoma kupinga sera za uchumi na kijamii za

Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa. Mwaka 1978/79 wanafunzi wa Chuo Kikuu walipogomea masomo walikuwa wakipinga uamuzi wa wabunge kujiongezea mishahara wakati taifa likiwa ndiyo kwanza limetoka kukabiliana na vita iliyogharimu uchumi wa nchi hii.

Miaka ya mwanzo ya 1990, wanafunzi wa chuo hicho hicho, tena wakiungwa mkono na maprofesa wao, waligoma kupinga maamuzi ya serikali ya kutaka kuwahamisha wahadhiri kadhaa waliokuwa wakionekana kuwa chachu kuu ya migogoro katika chuo kikuu hicho.

Walichokuwa wakikigomea wanafunzi hao ni kiu yao ya kitaaluma na ‘kiitikadi’ ya kukataa kuondokewa na wahadhiri wao wanamapinduzi akiwa Profesa Mwesiga Baregu, Issa Shivji na Chachage S Chachage.

Leo hii ni nadra sana kuikuta migomo ya namna hii ikifanyika katika vyuo vikuu vyetu. Njaa ya matumbo imebadili kabisa ile kiu ya kifikra ambayo kimsingi ndiyo iliyozaa viongozi makini wa migomo wa zama zile, akina Samuel Sitta, Andrew Chenge, na marehemu Wlifred Mwabulambo.

Migomo ya kifikra ya namna hiyo hiyo ndiyo ambayo baadaye ilizaa wasomi wa aina ya Zitto Kabwe, John Mnyika na wengine wengi ambao unaweza ukawatofautisha na wagomaji waliokuwa wakiangalia mustakabali wa matumbo yao.

Leo hii wanafunzi kwa makosa yasiyo yao, wanaishia kugomea chakula duni na ukata wa mifukoni, ilhali nchi hii ikiwa imebeba orodha ya majinamizi ya ubadhirifu ambayo kelele zake zinapigwa na vyombo vya habari na viongozi wachache wa vyama vya kisiasa na kijamii.

Wanafunzi wa vyuo vikuu ambao leo hii wamegomea haki yao ya msingi kabisa, tunawaasa kugeuka upande mwingine kwa kuangalia mienendo isiyoridhisha ya maamuzi mabovu kabisa ya kiserikali na kuandaa maandamano kwa ajili yake.

Wakati huu tunapokaa na kutafakari, tunajikuta tukilazimika kujiuliza hivi wanafunzi wa vyuo vikuu, wamewahi kufikiria kuongoza maandamano ya nchi nzima kupinga kashfa kama zile za rada, matumizi yaliyokithiri serikalini, mikataba yenye utata kama ile ya madini na Richmond?

Huko ndiko ambako wanafunzi wanapaswa kuelekea. Wanapaswa kutambua kuwa wao wakiwa vijana wanaopaswa kuwa tanuri la kifikra wanao wajibu pia wa kuhakikisha kuwa wanaliongoza taifa katika kuimarisha maamuzi ya kisera na kisheria ambayo hatimaye yataliondoa taifa hili katika umaskini uliokosa dawa.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:59 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Huu ni mwanzo wa mwisho wa matumaini
Na Absalom Kibanda

‘Sema unachomaanisha, maanisha unachosema;’ huu ni moja ya misemo maarufu kabisa na iliyozoeleka na wengi. Msemo huu umetafsiriwa neno kwa neno kutoka katika msemo wa Kiingereza; ‘Say what you mean, mean what you say’.

Ingawa si rahisi kusema kwa hakika ni nani aliubuni msemo huu au ni kitu gani hasa kilisababisha ukaibuka, ni ukweli wa wazi kabisa kwamba, hivi sasa umegeuka kuwa moja ya semi maarufu inayoandikiwa vitabu, inayofundishwa mashuleni na kufanyiwa tafiti na wasomi wa fani mbalimbali.

Katika mataifa yaliyoendelea na hususan katika medani ya siasa, msemo huu umekuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa wengi wanaosaka nafasi za kuchaguliwa.

Kauli wanaozotoa katika majukwaa ya kisiasa aghalab zimekuwa kipimo kikubwa cha kupima utekelezwaji wao mara tu wanapoingia madarakani na wakati mwingine wanapomaliza mihula yao wau wanapotafuta fursa za kugombea uongozi kwa mara nyingine tena.

Hali hiyo ni tofauti kubwa kwa nchi maskini za Kiafrika kama zetu ambazo wanasiasa husema maneno mengi, wakijua hakuna anayeweza akaja siku moja akawapima kwa kuyaangalia maneno yao kwa dhati kabisa.

Matokeo ya hulka hii, ndiyo hasa iliyosababisha baadhi ya watu kuwakejeli wanasiasa na hata kufikia hatua wa kuiponda dhana nzima ya (uana) siasa hata ikaonekana kuwa ni sawa na mchezo wa kuigiza.

Ni jambo la kawaida hivi sasa kwa wananchi wa kawaida kuwaelezea wanasiasa kuwa watu wa mzaha, waongo na mabingwa wa kusema kile wasichomaanisha.

Matokeo ya hali hii yamekuwa ni ya kukatisha tamaa kabisa, kwani maana halisi ya siasa katika nchi maskini kama Tanzania imebadilika na kuwa ‘si-hasa’ (not real) badala ya siasa ambayo katika nchi za wenzetu ni dhana inayotumika kutoa changamoto muhimu kabisa za kimaendeleo.

Hali hii ya kusikitisha imesababisha basi, wanasiasa wetu kuitumia siasa kama mwanya na daraja la kutafutia madaraka ya kuongoza, wakitambua kuwa kwao wao, uongozi ni ulaji na si utumishi wa watu.

Mwenendo huo wa mambo ndiyo ambao wakati fulani ulimfanya Profesa Issa Shivji atamke maneno ambayo leo hii huenda yana maana kubwa kuliko ilivyopata kuwa miaka michache tu iliyopita pale aliposema; ‘Wasomi wanapenda siasa. Wanasiasa hawapendi siasa, wanapenda madaraka’.

Ukiyatafakari maneno ya msomi huyu, jibu utakalopata ni rahisi kabisa kwamba. Wanasiasa wetu wameamua kuweka kando maana halisi ya siasa kuwa dhana ya uongozi inayompa wajibu mtu kuwaongoza wenzake kisheria na kisera na kuwa dira na kioo cha mwelekeo wa kikundi, taasisi, nchi au jumuiya ya kimataifa.

Hicho alichokisema Shivji kimechukua maana halisi leo hii, wakati serikali ya awamu ya nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ndiyo kwanza iko madarakani kwa miezi 16.

Maneno hayo ya Shivji na mwenendo wa mambo hapa nchini unatoa jibu moja rahisi kwamba, maneno matamu tuliyoyasikia kwa viongozi wa awamu hii tangu wakati wa kampeni yameanza kuchukua mwelekeo ule ule wa kusemwa kwa kile kisichomaanishwa.

Ni jambo la fedheha na kukatisha tamaa kwamba, hadi hivi leo, viongozi wetu wakuu wangali wakitumia misamiati ya ‘wakati ujao’ ya tuta..fanya, tuta..tekeleza, tuta..timiza, tutaendeleza wakati kipindi cha kufanya hivyo kilikwishapita.

Ni jambo lisiloingia akilini hata kidogo leo hii kwa Rais Kikwete na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa kuamua kuitisha kile kinachoitwa kikao cha watendaji serikalini na kuwapa maelekezo ya nini cha kufanya siku zijazo.

Kwa maneno mengine ni kichekesho kuwaona viongozi hao wakiwaita kwa mara nyingine tena wakuu wa mikoa na wilaya wakiwa na makatibu tawala wao kwenda Dodoma eti kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambayo imeonyesha hulka ya kudumu ya serikali ya CCM ya kutumia fedha isivyopaswa kila mwaka.

Ninasema ni kichekesho na hata kuufananisha na mchezo wa kuigiza kwa sababu Kikwete anafanya hivyo leo wakati akijua fika kuwa mwanzoni mwa mwaka jana alitoa tamko zito wakati alipotembelea Wizara ya fedha pale aliposema wale wote ambao watabainika kutumia fedha isivyo watawajibika kwa kupelekwa mbele ya vyombo vya habari.

Mwaka mmoja baada ya kutoa tamko hilo, Kikwete huyo huyo tena eti anaitisha kikao cha watendaji cha kuijadili ripoti nyingine ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na halafu anaahidi kitu kingine kwa ajili ya siku zijazo. Jina la kitendo hiki sinalo.

Maamuzi ya namna hii yanafanana kabisa na yale yaliyolalamikiwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na kimsingi yanaongeza gharama ambazo zingeweza kuepukwa.

Huku akijua kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inahusu matumizi yaliyokwishapita, kwa makusudi kabisa Rais Kikwete anajaribu eti kutoa tahadhari ya nini kinapaswa kufanywa kuanzia sasa ili kuepuka makosa yaliyopita.

Hivi iwapo Rais Kikwete angeamua kusambaza waraka maalum kwa watendaji nchi nzima akitoa maelekezo ya nini kifanywe kuhusu ripoti hiyo ni fedha kiasi gani zingeweza kuokolewa?

Iweje leo hii siku chache tu baada ya Bunge kuelezwa kuwa mikutano ya siku moja moja ya Waziri Mkuu na watendaji wa mikoa 10 ya mwanzoni mwa mwaka huu kujadili namna ya kuboresha elimu, ilitumia kiasi cha shilingi milioi 160, serikali iamue kuwakutanisha watendaji wakuu wa mikoa yote nchini?

Hivi ni lini serikali yetu hii ambayo daima imejenga hulka ya kudai kuwa gharama kubwa za mikutano kama hiyo ni ndogo kuliko faida ya mikutano yenyewe itaacha kutudanganya Watanzania kwa maneno ambayo hayawezi kupimwa kwa vigezo vya kitakwimu?

Hivi Rais Kikwete na Waziri Mkuu Lowassa wanataka kutuambia kwamba, hoja kuhusu matumizi bora serikalini haikuwa sehemu ya mada wakati wa semina elekezi za mapema mwaka jana za watendaji wa mikoa na wilaya ambazo gharama zake bado hazijawekwa bayana?

Kwa hakika huku si kuziba ufa nyumbani, bali ni staili rahisi ya viongozi wetu wakuu kuendelea kutupa matumaini Watanzania kila kunapokucha ili tuaamini kuwa serikalini yetu inakerwa na mabaya yanayotokea na kwamba huo ni mwanzo wa kuelekea kule walikokuita; ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’.

Wakati mwingine ninapoziangalia mbwembwe hizi za viongozi wetu huwa nashindwa kutuelewa Watanzania namna tulivyoshindwa kuwawajibisha hawa viongozi wetu ambao kwa miaka zaidi ya 45 wameendelea kuyaahirisha matatizo yetu hata kuufanya umaskini ndiyo uzishinde zile zinazoitwa sera za kuukabili.

Leo hii Watanzania ambao mara kadhaa Baba wa Taifa alipata kutusifu kwa kusema si wajinga, katika kutambua kile tunachokitaka, tumegeuka na wajinga kwelikweli ambao tumeendelea kusahaulishwa matatizo yetu wakati wa kampeni kabla ya kuanza kunungunika baada ya sura mpya ndani ya CCM ile ile kuingia madarakani.

Leo hii ukiwasikiliza wale waliokuwa mashabiki wa falsafa za kuahirisha matatizo za Kikwete wakati wa kampeni na baadaye siku za mwanzo za utawala wake unaweza ukawashangaa.

Wao ndiyo wamekuwa watu wa kwanza kulalamika. Wao ndiyo ambao leo wanasema hakuna kinachokwenda mbele, wao ndiyo ambao wameanza kuikebehi serikali.

Ni juzi tu wasomi wa chuo kikuu ambao waliendesha kampeni za wazi za kumshabikia Kikwete, walibeba mabango ya kudhihaki matumizi yasiyomithilika ya serikali hii tofauti kabisa na ilipokuwa wakati wa kampeni.

Ukisikiliza michango ya waziwazi ya wabunge wa CCM wenye uchungu wa kweli kweli wa nchi yao, katikati ya mistari ya hoja zao utasikia namna walivyo na wasiwasi na namna nchi hii inavyoendeshwa.

Jibu la mwenendo huu wa mambo ni rahisi kabisa. Matumaini makubwa ambayo Kikwete aliwajengea Watanzania tangu siku alipotangaza kugombea urais kule Kibaha yameanza kupungua.

Waraka wa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein wa kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kuchukua hatua za mara moja, nao unaonekana kubakia katika makabrasha.

Ile ahadi ya Lowassa aliyotoa siku alipopitishwa na Bunge kwa kusema atawapa Watanzania utumishi mahiri na makini inaanza kuonekana kuwa ni simulizi ya kufikirika, hasa kiongozi huyo anapowekwa katika mizania na watangulizi wake kadhaa waliowahi kushika wadhifa huo.

Lakini kikubwa ambacho kimeanza kuwafikisha Watanzania huko wanakokwenda sasa, ni hii hulka ya viongozi wetu hao, kuanza kuonekana kuwa ni watu wanaopenda kusema yale wasiyomaanisha na kuziweka viporo ahadi lukuki walizopata kuzitoa.

Kwa hakika Serikali ya Kikwete inaonekana dhahiri kuendeleza yale yale yanayoitwa mema ya serikali zilizotangulia za CCM, ambazo kwa bahati mbaya, rekodi ya kipekee inayowatembeza kifua mbele ni amani na utulivu.

Leo hii Kikwete ambaye baadhi ya wapambe wake wa zama za kampeni walipata kumuita mpinzani aliye ndani ya CCM anaonekana wazi kuanza kuwaangusha wasomi wa vyuo vikuu, wawekezaji wazalendo wanaogombea miradi na wawekezaji wa nje na wakashindwa, wabunge wa CCM, waandishi wa habari na makundi mengine aliyoyapa matumaini mengi yasiyomithilika.

Kwa hakika baadhi yetu sasa tumeanza kuamini kwa dhati kabisa kuwa, tabasamu lisilokwisha la Kikwete si suala la maumbile tu kama alivyopata kusema yeye mwenyewe, bali ni kielelezo halisi ya undani wake, upole wake na pengine kushindwa kwake kuchukua maamuzi magumu pale inapobidi.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:57 PM | Webu Unganishi | Maoni 0
Tuko zama za udikteta mamboleo
LEO nawaandikia Watanzania wenzangu, wenye mtazamo kama wangu, ujumbe unaokusudia kutufungua macho kutoka katika usingizi wa pono tuliolazwa na viongozi wetu na sisi wenyewe tukajifunika mablanketi mazito tukiridhia ubembelezwaji haramu wa ‘mtoto lala’.

Ujumbe wa leo ni rahisi kabisa na ambao kimsingi unaiendeleza hoja yangu ya wiki iliyopita ambayo ilikuwa ikilenga kuamsha hisia na fikra zitakazotuwezesha kutambua kuwa, mfumo unaofungua milango kwa ajili ya soko huria- kiuchumi, demokrasia ya vyama vingi- kisiasa na utawala bora- kijamii ndiyo njia pekee sahihi ambayo hatimaye itatuondoa hapa tulipo leo.

Watanzania, tupende tusipende, tukubali au tukatae, ahadi na mbwembwe nyingi za viongozi wetu wanaotembea kifua mbele wakitamba kwamba, wamelifanyia mema mengi taifa hili, hata kustahili kuenziwa kwa maneno, kalamu na kura ni mambo ambayo yanafurahisha genge zaidi kuliko kujenga misingi ya kuondokana na umaskini ulioota mizizi.

Ushahidi wa hayo ni rahisi kabisa. Miaka 45 na ushee baada ya uhuru majigambo ya viongozi wetu kutamba kujenga kilomita nyingi tu za barabara za lami na za kokoto, kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu na sifa nyingi nyingine zinazofanana na hizo ni mambo ambayo yameshindwa kulinusuru taifa hili na fedheha ya ufukara uliokithiri, maradhi yasiyokoma na ujinga usiomithilika.

Mambo makuu matatu ambayo Serikali ya Kwanza ya Tanzania (1961-1985) iliyaainisha kuwa maadui wakuu watatu wa maendeleo; ujinga, maradhi na umaskini yameendelea kubakia vidonda ndugu kwa taifa hili.

Leo hii Kikwete anapolieleza jarida la NewAfrican (soma toleo la Juni mwaka huu) kuhusu dhamira ya serikali yake kufanikisha mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE) baada ya kubaini kuporomoka kwa maelezo yanayoonyesha kuwa suala hilo ni jipya sana hapa nchini.

Watu makini wanafahamu kuwa, wakati Kikwete akisema chini ya UPE ya zama zake hizi imeingiza masomoni asilimia 96 ya watoto wote wanaopaswa kuwa darasani, ukweli ni kwamba kiwango kama hicho au zaidi yake kilipata kufikiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwishoni mwa miaka ya 1970.

Ukiuweka kando ujinga, adui mwingine maradhi naye pia amekuwa tatizo kubwa kabisa linalokuwa. Ukiuweka kando ukimwi, maradhi kama kifua kikuu, malaria na kipindupindu ambayo leo hii yanaundiwa mikakati mipya na ya kila jina kukabiliana nayo, yamekuwa katika kuta za maandishi maeneo mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35 sasa pasipo kupatiwa ufumbuzi. Nani halijui hilo!

Wakati ukimwi ukiwa sababu mojawapo ya kurejea kwa kasi kwa kifua kikuu, ukweli wa kitakwimu unaonyesha kwamba, ugonjwa huo kama yalivyo hayo mengine (malaria na kipindupindu) yameendelea kuwa sugu yakichagizwa na umaskini mkubwa unaolikabili taifa hili.

Leo wakati viongozi wetu wakipiga mbinje kujivunia matunda ya utawala wao, kwa miaka hiyo yote baada ya kuambiwa kuwa tuko vitani tukikabiliana na umaskini, Watanzania tunaendelea kuwa miongoni mwa mataifa sita maskini zaidi duniani. Kwa maelezo yoyote yale hii ni aibu na fedheha.

Kwa bahati mbaya sana, wakati baadhi yetu tukitambua kuwa Watanzania, kuanzia kwa viongozi wao hadi kwetu wananchi wa kawaida, tunao wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya, baadhi ya wenzetu, kwa sababu wanazozijua wao wameamua kutudhihaki hata kutupiga mkwara tena wa kimaandishi wakitaka eti tuache kuwafuatafuata, vigogo serikalini. Tunasubiri tuone nani atamuacha mwenzake.

Uamuzi wetu wa kuwakosoa viongozi, kuwakumbusha wajibu wao, na kukemea inapobidi kwa lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora tukitumia kalamu zetu, unaonekana kuwa ni wa kisaliti na unaofananishwa na ukibaraka tunaotumwa na wale wanaowaita ‘mabwana’ zetu.

Viongozi wa serikali wanaokosolewa kwa makali na uzito unaolingana na ukubwa wa makosa yao, wameanza kugeuka mbogo. Wanashambulia kila mmoja anayeonekana kujaribu kuhatarisha madaraka yao ambayo, badala ya kuyaona kuwa dhamana na wajibu wa kuwatumikia wananchi wameyageuza kuwa mtaji wa ulaji wa aina ile ambayo Augustine Mrema alipata kuuita ‘ya kula bila kunawa.’

Kile ambacho, mchambuzi wa habari, Ansbert Ngurumo alipata kukiandika akiwataja baadhi ya wanahabari wenzake kuwa ni mamluki wa viongozi wa dola, ndicho kinachoonekana kutokea hivi sasa.

Ukimsoma Ngurumo, ndani ya makala yake utawabaini mbwa wanaowaita watu, mbwa. Wasaliti wanaojivika joho la ushujaa na kuwaita wapambanani vibaraka. Hii ni jeuri ya ajabu kabisa.

Baadhi ya viongozi walio katika serikali hii ya Rais Kikwete hivi sasa wameanza kuhusishwa na magenge ya ‘kimafia’ yanayoundwa na baadhi ya watu tukiwamo wanahabari ambao pengine kwa ahadi za kupata nafasi za kiuongozi au kimaslahi wanayoyajua wao, wameamua kuanza kutumia vyombo vya habari kuwalinda majemedari wao hao kwa gharama zozote zile.

Maelfu ya Watanzania wanaosoma safu hii, wanapaswa kutambua kuwa, huko tuendako, kalamu kali dhidi ya ukiukwaji wa uongozi bora unaofanywa na baadhi ya watu wenye madaraka ndani ya CCM na katika serikali zake zinaweza kukabiliana na dhoruba kutoka kwa wanahabari mamluki wanaojulikana na ambao wameamua ama kujibebesha au kubebeshwa ukibaraka wa kifikra.

Lakini pia, viongozi hao hao kwa kadri inavyoonekana, wameshaanza kujipanga tayari kukabiliana na jambo lolote lile linaloelekea kufanana na wimbi la upinzani kutoka miongoni mwa wafanyabiashara na wanasiasa makini kutoka kambi ya upinzani.

Hiki ambacho wapinzani wa vyama vinne vya siasa, NCCR-mageuzi, TLP, Chadema na CUF wanataka kukiita ushirikiano unaotarajia kuzaa umoja wenye nguvu wa vyama hivyo, tayari umeshaanza kuonyesha dalili za kukisumbua chama tawala na serikali yake.

Ukisoma katikati ya mistari, baadhi ya tahariri, ukasadifu viponzo kadha wa kadha na ukazitafakari makala nyingi tu za kichambuzi ndani ya magazeti utayaona mashambulizi makali dhidi ya muungano huo wa upinzani na namna ulivyoshindwa kabla ya wakati.

Kwa kweli ni jambo la bahati mbaya kwamba, kauli mbiu za Kikwete za Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya zimegeuka na kuwa falsafa na muongozo wa kazi za wanataaluma wa kada mbalimbali wakiwamo wana habari.

Jukumu la wanahabari limegeuka kabisa kutoka katika kundi la wachokozi wa mada, wakosoaji kupitia katika tahariri na makala za kiuchambuzi na kuwa washangiliaji na walinzi wa status quo.

Kile ambacho Jenerali Ulimwengu amekuwa akikielezea kuwa ni ‘urafiki wa hatari na uliovuka mipaka kati ya wanahabari na wanasiasa’ ndicho ambacho leo hii tusipokuwa macho, kinaweza kikaivuruga taaluma ya habari yenye wajibu wa kuongoza njia.

Leo hii, Kwame Nkrumah angeamka kutoka kaburini na kufanya tathmini ya kile kinachoonekana kuwa mafanikio ya sera za soko huria na mfumo wa vyama vingi ninao uhakika jina la kitabu chake lisingelikuwa tena; ‘New Colonialism The Highest Stage of Imperialism’ (Ukoloni mambo leo ni hatua ya mwisho ya ubeberu).

Badala yake mwanasiasa na mwanazuoni huyo kwa namna yeyote ile Neo Colonialism ingebadilika na kuwa Neo Liberalism kwa maana ya Udikteta mambo leo ambao watawala wanaoshinda uchaguzi chini ya mfumo haramu wa vyama vingi uliojaa mizengwe iliyokithiri wanavyojaribu kutumia ushindi wao huo kuminya uhuru wa habari, uhuru wa vyama vingi, uhuru wa kufikiri na dhana nyingine za namna hiyo.

Nkrumah angeshangaa kubaini kuwa ubeberu umebadilika. Angestaajabu kuona watawala wa wa Kiafrika wakiwa wamejenga mtandao wa mahusiano ya ajabu kabisa na mabeberu walioupa jina la utandawazi. Mahusiano haya ndiyo yaliyowapa jeuri watawala wetu hata kuwa na jeuri ya kutumia udikteta mambo leo.

Kwa hakika udikteta mambo leo wa watawala wengi wa Kiafrika, umefanikiwa kuihadaa dunia kuwa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa habari, soko huria la kishindani ni mambo yanayofanya kazi pasipo shida yoyote, ilhali hali ikiwa tofauti.

Siyo jambo la siri kwa Watanzania wachambuzi wa mambo kutambua kuwa, udikteta mambo leo wa watawala wetu wanaojivunia ushindi wa kishindo ni matokeo ya wazi ya kazi kubwa iliyofanywa ya kuwanyonga wapinzani kwa fitina za uzushi, sheria ngumu na kandamizi zikiwamo zile 40 ambazo Tume ya Jaji Nyalali ilipata kupendekeza zifutwe.

Ni ukweli unaojulikana wazi kwamba, ushindi wa asilimia 80 ni matokeo ya kazi batili itakayobakia kuwa historia ya nchi hii ambayo ilivigeuza vyombo vyetu vya habari na na baadhi ya sisi wanahabari (Watanzania watusamehe) kuwa taasisi mahususi za uenezi za CCM.

Ni jambo la ajabu kabisa kwamba, leo hii, ushindi huo wa kishindo wa asilimia 80 ambao badala ya kuwa mzigo na dhamana isiyobebeka ya wajibu wa kuwatumikia wapigakura umegeuka na kuwa jeuri ya kuwasakama na kuwazulia mambo wakosoaji wengi ninaoamini wanafanya hivyo kwa nia njema kabisa.

Ujinga wa sisi Watanzania tulio wengi kuendelea kuuona mfumo wa vyama vingi kuwa eti msingi wa kusambaratika kwa umoja wetu, na dalili mbaya za kutoweka kwa amani na utulivu, tukitahadharishwa kuwa makini tusije tukafikwa na yale yaliyowahi kuwafika wenzetu wa Rwanda, Burundi, Kongo, Sierra Leone na kwingineko una sehemu kubwa katika ushindi huo wa asilimia 80.

Hivi Watanzania tumesahau kwamba, asilimia 80 ya watu ambao walipiga kura ya maoni wakitaka mfumo wa chama kimoja uendelee mbele ya Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1991 na 1992 ndiyo matunda ya ushindi wa CCM leo hii ambayo viongozi wake wanapita kifua mbele wakiwakebehi wachambuzi wa mambo wanaoikosoa serikali leo hii.

Kwangu mimi, CCM na serikali yake wanafanya makosa kuutumia ujinga wetu wa kuvinyanyapaa vyama vya upinzani na kukishabikia chama hicho tawala kwa staili ya zimwi likujualo, kuwa ndiyo jambo la kuwatembeza kifua mbele.

Ninasema ni makosa kwa sababu, viongozi hao na mashujaa wao wanaowatumia kuwadhihaki na kuwatukana wachambuzi wanaoikosoa serikali ikiwa ni pamoja na kuwashusha hadhi wanasiasa wa kambi ya upinzani hawajui wanafanya hivyo kwa sababu ya matumbo yao na wala si kwa maslahi na uzalendo wenye manufaa ya leo na kesho ya taifa hili. Hakika huu ni udikteta mambo leo. Tunaelekea kubaya.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:56 PM | Webu Unganishi | Maoni 2
Tumeangushwa na manabii wa uongo, tuanze upya
Tunakabiliwa na tatizo kubwa la kiuongozi katika nchi hii. Kimsingi tupo katika tanuru la uongozi uliolipotezea mwelekeo taifa, kiasi kwamba hivi sasa ni jambo gumu kwelikweli kutofautisha baina ya pumba na mchele.

Leo hii umaarufu wa kiongozi mmoja binafsi umechukua nafasi ile ile ya uwezo wa kiuongozi au hata kiutawala wa kiongozi huyo huyo.

Ubora wa kiongozi hivi sasa unapimwa kwa maneno rahisi kabisa; ‘Je, akubalika!?’ Kukubalika kunakozungumzwa hapa ni kule kunakojengwa na uwezo wa ushawishi wa kiongozi mhusika ama wapambe wake au mawakala wake rasmi na wasio rasmi.

Ukianzia na uongozi katika vyuo vya elimu ya juu, vyama vya michezo, klabu za kijamii, uongozi wa kidini na hata ule wa kisiasa, hoja kubwa imekuwa ni hiyo hiyo; anakubalika?

Kwa bahati mbaya sana, kukubalika huko hakujengwi na historia yeyote ile ya kutukuka ya kiongozi mhusika, mabadiliko aliyowahi kuyafanya huko nyuma au rekodi ya kipekee ya utendaji wake, bali haiba yake binafsi na namna alivyoweza kuwa karibu na watu wengi wanaomuunga mkono.

Kile ambacho kwa kimombo kimekuwa kikijulikana kama ‘charisma’ ndicho hicho ambacho sasa kimekuwa kigezo kikuu na sifa ya uongozi.

Tumefikishwa hapa na historia yetu. Tumefikishwa hapa na urithi mbaya kabisa tulioachiwa na waasisi wa taifa hili. Tumefikishwa hapa na ulafi wa watu wachache ambao kwa makusudi kabisa wamefanikiwa kuipa rushwa jina jema, wale ambao wamebariki ufisadi.

Matokeo ya kufikishwa kwetu hapo ndiyo yaliyotufanya tuwaite ‘wajanja’, ‘mashujaa’, ‘wenye akili’, ‘wanaoona mbele’, maafisa wa serikali waliojenga makasri katika maeneo mbalimbali nchini kwa fedha ambazo haziwezi kulinganishwa hata kwa chembe ya haradali na mapato yao halali yanayojuolikana.

Hatima ya kupelekwa hadi huko ndiyo ambayo leo hii imetufikisha hatua ya kuwacheka na kuwadharau viongozi waadilifu wa kweli kweli (ukiwaacha walevi, mafuska na wale wenye tabia zinazofanana na hizo) ambao wanastaafu serikalini wakiishi maisha ya kawaida yasiyo na makuu.

Leo hii, taifa hili limefikishwa mahali ambapo wajasiriamali wa kwelikweli wasiofungamana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) au serikali yake kimtazamo wanafinyangwa na kukamuliwa kwelikweli kimapato na serikali huku matapeli makada wa chama hicho tawala wanaofanya biashara kwa njia haramu zenye maswali mengi, wakilindwa na kuheshimiwa kwa kiwango cha kuabudiwa.

Hayo ndiyo matunda ya miaka 45 ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi kilichoingia madarakani madarakani mwaka 1961 kwa jina la Tanganyika African National Union (TANU) kwa Tanzania Bara na kuanzia mwaka 1964 kikijulikana kwa jina la Afro Shiraz Party (ASP) kule Zanzibar.

Hayo ndiyo matokeo ya urithi mbaya tuliogawana wakati wa zama za vita baridi ambayo upepo wa mabadiliko yake umewakamata pabaya Watanzania.

Msingi wa mambo hayo ni maamuzi ya kimaono ya kiongozi mkuu wa kwanza wa chama hicho tawala, Julius Kambarage Nyerere, aliyeamua kulipeleka taifa hili maskini katika kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1960 baada ya kutambua kuwa tulikuwa hatuna ubavu wa ama kushikamana na mataifa ya kibepari ya kimagharibi au kuungana na yale ya kisoshalisti ya mashariki.

Mwalimu, akitumia maono yake binafsi na taaluma yake ya masomo ya historia akaona namna ilivyokuwa vigumu kwa kijinchi maskini kama hiki kujitwisha ubepari au ukomunisti na badala yake akaifanya kile walichofanya viongozi wenzake kadhaa wa Kiafrika.

Yeye na wenzake kadhaa ambao leo wanaitwa mashujaa wa Afrika wakaja na kile walichokiita Ujamaa wa Afrika (Africa Socialism), wakisema huo ndiyo mfumo unaotokana na mazingira ya kihistoria ya bara hili.

Ujamaa huo wa Afrika ulichukua sura tofauti katika nchi mbalimbali za Kiafrika. Kwame Nkrumah shujaa nambari wani, yeye akaunda wake, Milton Obote naye akaja na wake, hivyo hivyo Leopold Senghor wa Senegal, baadaye Muamara Gaddafi wa Libya na hata Jomo Kenyatta wa Kenya.

Mwalimu yeye akaja na ujamaa. Akautaja kwa mara ya kwanza mwaka 1962 na miaka mitano baadaye akaja na Azimio la Arusha.

Huo ukawa mwanzo wa Tanzania kuanza kuzalisha orodha ndefu ya manabii wa kisiasa, wengi wao wakiwa ni wanafunzi waliopata masomo yao katika nchi za kisoshalisti duniani zikiongozwa na lililokuwa Shirikisho la Kisoshalisti la Kisovieti (USSR), iliyokuwa Ujerumani Mashariki, Cuba na kwingineko.

Leo hii miaka mingi baadaye, mafundisho ya unabii huo, ambao kiongozi na mwasisi wake alikuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Tanzania imezalisha viongozi mahodari wa kusema kile wasichoamini na kuamini kile ambacho hawakisemi.

Kwa bahati mbaya sana, orodha ya viongozi wa namna hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi ambayo inapaswa kudhibitiwa, kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Karibu miaka 22 sasa tangu Mwalimu ang’atuke kutoka madarakani, Tanzania imepata jina jipya ikijulikana kama ‘Bongoland’ ambalo wakati fulani Mkapa alipata kuonyesha hisia ya kukerwa na maana yake ya sasa.

Wakati wa zama za Mwalimu na baadaye enzi za Mzee Ali Hassan Mwinyi, neno Bongoland likimaanisha watu wanaoishi kiujanjaujanja, lilikuwa ni neno lililokuwa likiwagusa watu wa daraja la chini kabisa, waliokuwa hawana mbele au nyuma na waliokuwa wakiishi kwa utapeli, leo hii neno na tafsiri halisi ya neno hilo vimepanda daraja.

Upandaji wa daraja kwa maana na matumizi ya neno hilo yalikwenda sambamba na mabadiliko ya serikali tangu zama za Mwalimu, na baadaye Mwinyi kabla ya kujistawishi wakati wa uongozi wa Benjamin Mkapa na hatimaye kuchukua kabisa madaraka mwaka 2005.

Kundi lililompa ushindi Rais Jakaya Kikwete lililojumuisha watu kama, Bernard Membe, Edward Lowassa, Mohammed Abdulaziz, Rostam Aziz, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri na wengine ambalo miaka takriban 10 iliyopita lilipewa majina mengi ya utani yaliyokuwa yakiendana na haiba zao enzi hizo kama; ‘watoto wa mjini’, ‘Boyz 2 Men’ na mengine mengi leo hii limefanikiwa kushika madaraka ya juu kabisa ya nchi.

Wanachama wa kundi hilo ambalo kabla ya kupanda ngazi hata kuingia katika viunga vya ikulu na wengine kukalia makazi ya waziri mkuu na kusindikizwa kwa mbwembwe za ving’ora lilikuwa likisifiwa kwa namna lilivyokuwa na uwezo wa kujichanganya na watu wa aina mbalimbali, leo hii ni nadra kuwaona katika hali kama ile tena.

Urithi wa kundi hili haukuanza nao, bali ulirudi nyuma zaidi zama za Mkapa mwenyewe ambaye naye zama zake za kabla ya ikulu alikuwa mtu wa kariba hiyo hiyo ya kujichanganya, japo yeye kundi lake lilihusisha wasomi vijana wa zama zao, miaka ile ile ya 1970, 1980 na 1990.

Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa. Mtazame Mkapa, angalia mbwembwe za uvaaji wake, utanashati wake, mapenzi yake kwa vidani, pete kubwa kidoleni chain pana shingoni na salamu yake maarufu ya; ‘mambo!!!’ vyote vilikuwa vikionyesha jitihada zake za kujaribu kuwasiliana na vijana wenzake aliojichanganya nao zama akiwa hajagusa zulia jekundu la ikulu.

Ukimwacha Mkapa warejee wadogo zake aliowarithisha ikulu, madaraka na mamlaka. Anza na Kikwete na baadaye wachunguze akina Lowassa, Membe, Nao utaona mambo mengi yanayowafanya wajaribu kila mara kuwasiliana japo kwa haiba na kundi lile waliloliacha. Hii inaweza ikawa falsafa ngumu kuielewa haraka. Itafakari.

Matokeo haya ya malezi mchanganyiko ndiyo ambayo leo hii yanauweka uongozi wetu hivi sasa katika zama tofauti kabisa na zile za akina Mwinyi na Nyerere ambao malezi yao yaliwanyima fursa ya kuchamana na makundi yaliyo nje na haiba za kiuongozi.

Ingawa ni kweli kwamba, viongozi wa zama za Mkapa na hawa wa Kikwete wanazo fursa fursa za kulijua vyema kundi lililowazunguka linalowakilishwa na vijana wa mitaani, au vijana wa zamani kama wanavyojulikana baadhi yao hivi sasa, bado wamerithi hulka mbaya ambazo wanapaswa kukabiliana nazo.

Ingawa hulka hizo walizorithi ni nyingi, kubwa ambayo nitaanza kuizungumzia wiki hii na kuendelea nayo wiki ijayo ni hii ya unabii wa uongo wa viongozi wetu ulioanza tangu zama za Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Watanzania wenye umri wa zaidi ya miaka 40 sasa wanakumbuka namna taifa hili mwaka 1980 lilipoahidiwa kuanza kupata neema ya kukua kwa uchumi katika kipindi cha miezi 18 baada ya kumalizika kwa vita ya Uganda ambayo iligharimu mamilioni ya fedha.

Leo hii miaka 27 baadaye hali ya uchumi bado haijatengemaa na unabii wa kwanza wa kuikomboa nchi hii kiuchumi umekwama hadi hivi leo.

Kukwama kwa unabii huo wa kiuchumi kulikuja miaka zaidi ya 10 baada ya kukwama kwa unabii wa Azimio la Arusha ambalo Baba wa Taifa alilisimamia na akalipigania kwa nguvu zake zote.

Huku akidhani kwamba, alikuwa amefanikiwa kurithisha ajenda yake kwa manabii wake, Mwalimu alipigwa na butwa baada ya kubaini kuwa takriban manabii wake wote walikuwa wamemsaliti. Walihubiri Ujamaa mchana na jioni wakakiuka misingi ya falsafa hiyo.

Kuzorota kwa Azimio la Arusha na baadaye kukwama kwa programu ya miezi 18 ya kujinasua kiuchumu kulifuatiwa na kuzorota na baadaye kuendelea kushindwa kabisa kwa mipango mingine ya kiuchumi ya taifa hili iliyoasisiwa na serikali za awamu za pili na tatu.

Ukiuliza leo ni kwa nini unabii wa akina Nyerere, Rashid Kawawa uliorithishwa kwa akina Mwinyi na baadaye kwa Mkapa wa kukabiliana na maadui wakuu watatu, umaskini, ujinga na maradhi umeishia wapi? Hautapa jibu la moja kwa moja.

Leo hii hotuba aliyowahi kutoa rais wa zamani wa Marekani, Ronald Reagan Novemba 2 mwaka 1988 kuhusu mapambano dhidi ya umaskini unaweza ukapata jibu rahisi kabisa.

Reagan mmoja wa marais wa taifa hilo kubwa siku hiyo alisema bayana akiilenga nchi yake pale aliposema umaskini ndiyo ulioshinda vita ya kuukabili.

Hakuna anayeweza akabisha kuwa hata hapa nchini, umaskini umeushinda nguvu unabii wa akina Nyerere, Mwinyi, Mkapa na sasa Kikwete naye akiwa na unabii ule ule uliopambwa kwa maneno totauti; “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania” umeanza kuonyesha dalili zile zile za kukwama.

Leo hii vita anavyoongoza Lowassa vya kuhamasisha ujenzi wa shule za msingi na sekondari nyingi zaidi katika kila kata inapiganwa kama vile nchi hii haijawahi kuwa na programu maarufu ya enzi za Mwalimu Nyerere ya Elimu kwa Wote (UPE) ambayo tafsiri yake ilibadika na kuwa Elimu Pasipo na Elimu (UPE).

Unabii wetu kuhusu maradhi ndiyo mbaya zaidi kuliko mwingine wowote kwani, kwa zaidi ya miaka 40 tangu tutangaze vita dhidi yake, tumeshindwa kuyamaliza baadhi ya magonjwa sugu huku mengine mapya yakiendelea kuibuka kila kukicha.

Leo hii taifa linashindwa kukabiliana na maradhi kama kipindupindu, malaria, kifua kikuu, Homa ya Bonde la Ufa na mengine mengi kwa sababu unabii wake ulijengwa katika misingi mibaya.

Umefika wakati wa kugeuka Kaskazini na kuachana na unabii na manabii wa uongo. Tukiendelea kuwa mafundi wa kujidai tunaanzisha programu mpya za kumaliza matatizo yetu kila kukicha, taifa hili litaendelea kupiga maktaimu wakati wenzetu wakiruka na kutuacha tukiwa pale pale. Tunapaswa kuanza upya.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:53 PM | Webu Unganishi | Maoni 1
Je huu ndiyo ushupavu wa uongozi?
Na Absalom Kibanda

AGOSTI 25 mwaka 2004, takriban mwaka mmoja na ushee kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete na wanamtandao wenzake madarakani, Benjamin Mkapa wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alitoa moja ya hotuba ambazo kwangu itaendelea kubakia kuwa ya kihistoria.
Mkapa alitoa hotoba hiyo iliyokuwa ikibeba ujumbe mzito wakati alipokuwa akiwahutubia wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma.
Siku hiyo hiyo baada ya Mkapa kumaliza hotuba yake hiyo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula aliielezea hotuba hiyo kuwa ya kihistoria na akatamka kwamba ndiyo itakayotumika kama dira ya chama hicho kitakapokuwa kikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Kimsingi Mkapa aliibadilisha hotuba yake na ikachukua sura ya mada ya kisiasa na kwa maneno yake mwenyewe, akaipa kichwa cha habari kisemacho, ‘Ushupavu wa Uongozi’ au kwa Kiingereza, ‘The Courage of Leadership’.
“Leo nimeamua kutoa hotuba, tena iliyoandikwa, maana jambo nitakalo kulizungumza ni zito na nimelitafakari kwa muda sasa. Napenda kuzungumza nanyi kuhusu ushupavu wa uongozi, kwa Kiingereza: “The Courage of Leadership.
“Nafanya hivyo kwa vile tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani (2005).” Hayo yalikuwa ndiyo maneno ya utangulizi katika hotuba hiyo aliyokuwa akiitoa huku akisoma.
Hakuishia hapo Ben; bali alikwenda mbele zaidi na akahoji kwa kujiamini kabisa akisema: “Napenda leo tujiulize swali la msingi kabisa. Sisi Chama Cha Mapinduzi tunataka uongozi; vema, lakini je, chama chetu kinao ushupavu wa uongozi unaohitajika katika mazingira ya karne ya 21? Wagombea wetu watarajiwa nao je?”
Huo ulikuwa ni utangulizi wa maneno mazito. Kwa hakika ni dhahiri kwamba Mkapa alijenga hoja kwa kauli nzito.
Nikiwa miongoni mwa waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia moja kwa moja hotuba hiyo, niliguswa na msingi wa ujumbe wake na leo hii miaka karibu mitatu baada ya kutoa hotuba yake hiyo, bado maneno hayo ya Mkapa yameendelea kubakia chachu ya tafakuri zangu kuhusu mwenendo wa siasa zetu na mustakabali wa taifa letu.
Hotuba hiyo ya Mkapa ilibadili kwa kiwango kikubwa mwelekeo wa kifikra wa wanasiasa wengi, na kwa mara ya kwanza akawajengea Watanzania subira ya kuwapo kwa matumaini mema.
Kwangu hiyo ilikuwa ni hotuba ya nne bora kabisa iliyowahi kutolewa na Mkapa. Iliingia katika kumbukumbu ya hotuba nyingine tatu alizopata kuzitoa awali.
Kwanza alinikumbusha ujasiri na kujiamini aliotuonyesha Watanzania wakati wa mdahalo wa wagombea urais wa Tanzania mwaka 1995, alipowafunika wenzake akiwamo Augustine Mrema, ambaye alikuwa akionekana chaguo la wengi, nje ya CCM.
Pili, alirejesha nyuma kumbukumbu zangu hadi Oktoba 10 mwaka 2001 alipotoa hotuba nzito siku vyama vya CCM na CUF vilipotia saini muafaka wa kisiasa uliopanga kumaliza mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
Tatu, alirejesha hisia zangu hadi Oktoba ya mwaka 1999, alipotoa hotuba nyingine nzito wakati wa mazishi ya Baba wa Taifa, hata baadhi ya watu kudiriki kusema, ‘mzimu’ wa Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa umemgusa.
Kwa maneno mengine yoyote yale, hotuba ile ya Mkapa ya ‘Ushupavu wa Uongozi’ ilipaswa na kimsingi inapaswa iendelee kuwa moja ya hotuba za kukumbukwa miaka mingi baadaye.
Kama zingekuwa zikipangwa katika madaraja, basi hotuba hiyo ya Mkapa ingeweza kushika nafasi ya pili kwa kuwa na mawazo ya kimapinduzi baada ya ile aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete bungeni, Desemba 31 mwaka 2005, siku chache tu baada ya kuingia Ikulu.
Mkapa katika hotuba yake hiyo ndipo alipotangaza kwa mara ya kwanza, haja ya CCM kuwa na wagombea kuanzia wa urais, ubunge na hadi udiwani wenye uwezo wa kutenda pasipo kutegemea nguvu za chama.
Ni katika hotuba hiyo, Mkapa alionyesha kutambua kuwapo kwa uwezekano wa chama hicho kuwa na kapu la viongozi aliowaita wa hovyo, ambao ushindi wao ungetegemea tu nguvu ya CCM.
“Na zipo njia mbili kubwa za mtu kushinda uchaguzi. Moja ni kuhakikisha unakuwa mgombea wa chama chenye nguvu na mvuto, kama ilivyo CCM hivi sasa. Maana yake ni kuwa hata wewe mgombea ungekuwa hovyo kiasi gani, utabebwa na chama, na utachaguliwa kuwa diwani, mbunge au rais, kwa sababu tu ya chama.
“Njia nyingine na ya pili, ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi wampigie kura, sio chini ya kivuli cha chama chake. Napenda leo tujikumbushe kuwa yote haya mawili ni muhimu: Chama imara, chenye ushupavu wa uongozi; na wagombea imara, wenye sifa, uwezo na ushupavu. Na kuhakikisha kabisa, yote mawili ni muhimu na ni vema yaambatane,” alisema Mkapa.
Hicho alichokisema ndicho kinachoonekana leo. CCM imeendelea kama alivyopata kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa dodoki au kokoro lililobeba uchafu wa kila namna ndani yake.
Si jambo la siri kwamba wanasiasa kadhaa wa hovyo kabisa (kama alivyotanabaisha Mkapa) wameweza kupenya na kushinda ubunge na baadhi yao wameukwaa hata uwaziri kwa sababu tu ya dhamira ya rais kuwianisha uwakilishi wa kimikoa na kikanda.
Kwa sababu hiyo basi, msingi mbaya uliojengwa na CCM umesababisha wanasiasa wa hovyo wafanikiwe kukitumia chama hicho kama maficho ya ama udhaifu wao wa kupindukia au madhambi yao mengi mengine.
Matokeo ya hili ni ya wazi kabisa. Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, wanalazimika kufanya kazi za mawaziri, naibu mawaziri, wabunge na hata madiwani.
Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa. Kikwete ndiye anayeongoza hamasa katika michezo, ndiye anayetoa muongozo katika sekta ya ardhi na ndiye huyo huyo anayekwenda kufungua shule na kuagiza TANESCO waipelekee umeme. Unajiuliza mawaziri, makatibu wakuu, watendaji mbalimbali wako wapi?
Edward Lowassa, ndiye anayelazimika kurudiarudia harakati za rais wake kuchochea ari ya ujenzi wa madarasa katika mikoa, hata kufikia hatua ya kuwaita watendaji wa mikoa kwa zamu wakati nchi hii ikiwa na wizara mbili zinazoshughulikia maendeleo ya elimu.
Ni Lowassa huyo huyo anayeratibu mapambano dhidi ya homa ya bonde la ufa na kipindupindu ilhali kuna mawaziri, watendaji na mawaziri katika wizara za afya, kilimo, mifugo na taasisi nyingine za kitaalam zikiwamo.
Mbaya zaidi ni kwamba, Waziri Mkuu anakwenda nje ya nchi, kama alivyokuwa New Zealand hivi karibuni, na anajikuta akilazimika kufanya ziara ya kutembelea mashamba ya kabeji na kujionea ukulima wa kisasa, akiwa ameongozana na viongozi wengine kadhaa isipokuwa Waziri wa Kilimo. Hili nalo ni jambo la kushangaza.
Kwa maneno rahisi kabisa, matendo haya yanayofanywa na viongozi wetu wakuu hayatokani na ushupavu wao kiuongozi, bali ni udhaifu mkubwa wa kiutawala unaotokana na CCM kuruhusu kuwa na jeshi kubwa la viongozi wasio na uwezo.
Haya ndiyo matokeo ya kuendeleza kasumba inayodai kuwa, nafasi za uwaziri, ukuu wa mikoa na wilaya ni za kisiasa wakati tukijua kuwa matatizo yanayotokea katika maeneo wanayofanyia kazi yanatakiwa kupatiwa majibu ama ya kimenejimenti, kisaikolojia au hata kisayansi. Huku kwa hakika ni kucheza mchezo wa kujificha na mwenzi wetu umaskini.
Kila mara ninapopata fursa ya kuzungumza na wasaidizi wa Rais Kikwete na Waziri Mkuu Lowassa, huwa napata jibu moja kutoka kwa watu hao, la kunitaka nitambue kuwa eti viongozi wetu hao wawili wanatumia muda wao mwingi kuhangaikia matatizo ya watu kwa maslahi ya taifa.
Majibu hayo hugeuka kichekesho kikubwa kabisa kwangu, kwani wakati nikikubali kwa dhati kabisa kwamba viongozi wetu hao wawili hutumia muda mwingi kufanya kazi hizo, natambua vile vile kuwa wanafanya kazi ambazo si zao.
Kikwete na Lowassa wanapaswa kutambua kuwa, wakati wakiwa na wajibu wa kufuatilia utendaji wa kazi kitaifa, wanao wajibu pia wa kuwaamini wasaidizi ambao wengi wao wameteuliwa na wao wenyewe.
Hii tabia ya Rais na Waziri Mkuu kuzikimbia kabisa ofisi zao, mwaka mmoja na ushee sasa, eti wakitafuta kuonekana kuwa wao ni watu wa ‘field’, hata kufikia hatua za wao kugeuka na kuwa madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, naibu mawaziri na hata mawaziri, inakinzana na misingi ya utawala bora.
Kama wanabisha hebu wawaangalie viongozi wakuu wa mataifa yaliyoendelea kama Marekani, yenye uwezo mkubwa kifedha kuliko sisi, wenye miundombinu bora kabisa kama barabara kuliko sisi, na waangalie muda ambao rais na makamu wake wanatumia nje ya ofisi zao ndani ya nchi yao.
Ni nadra na kimsingi hakuna kitu kinachoweza kikafanana na uzururaji kwa Rais wa Marekani, George Bush ndani ya Marekani na kila anaposikika akisafiri kutoka Washington yaliko makao yake makuu, kwenda katika jimbo jingine, basi ni ama anafanya hivyo yanapotokea maafa kama yale ya Katrina au anadhuria mkutano muhimu.
Leo hii hapa nyumbani, kasi ya Rais Kikwete kushughulikia masuala madogo madogo ya ndani ya nchi au yale yanayohusu mahusiano ya kimataifa, inaonekana kuwa ni kubwa kuliko hata alipokuwa Mbunge wa Chalinze na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kikwete anakaribia kufanya makosa yale yale ya mtangulizi wake, ambaye hata alipokuwa Rais wa Jamhuri kwa miaka 10, bado alikataa kabisa kuiacha nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje, akitumia kisingizio kile kile kinachotumika leo, kuwavuta wawekezaji na kurejesha imani ya mataifa makubwa.
Kwa sababu hiyo basi, nikitumia maneno ya Mkapa; “The Courage of Leadership”, napenda kutumia fursa hii kuwaasa viongozi wangu wakuu wawili; Kikwete na Lowassa, kutafakari upya matumizi mabaya ya fursa waliyopewa na Watanzania, kwa kujenga mtandao imara wa wasaidizi kuanzia ngazi za chini kabisa ili kujipunguzia mzigo mzito wa madaraka wanayojaribu kujitwisha.
 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 10:48 PM | Webu Unganishi | Maoni 1
Thursday, January 25, 2007
Zanzibar inadai Mapinduzi mengine
Zanzibar inadai mapinduzi mengine!


Na Absalom Kibanda

Vyama viwili vya siasa, vyenye ushawishi unaowiana
Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha
Wananchi (CUF) vimewarejesha tena Watanzania na
hususan Wazanzibari kule walikotoka.

Vyama hivyo vimeanzisha tena kile kinachoitwa
mazungumzo ya kuponya jinamizi lililobadili jina la
awali la ‘mgogoro’ na ambalo hivi sasa limebatizwa
jina tofauti; ‘mpasuko.’

Jemedari mkuu anayeongoza mapambano ya kukabiliana na
jinamizi mpasuko safari hii ni mpya, naye si mwingine
bali Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Nne wa Tanzania.

Kikwete anaingia katika pambano hilo la Zanzibar
akikabiliana na kinara wa siasa za visiwani kwa zaidi
ya
miongo miwili na ushee, Seif Sharif Hamad, al- maarufu
‘Maalim’ miongoni mwa Wazanzibari na hususan watu
wanaohusudu sera zake na za chama chake cha CUF.

Ingawa ajenda ya sasa ya kutafuta suluhu dhidi ya
mpasuko wa Zanzibar ilijengwa na Kikwete siku chache
tu baada ya kutwaa madaraka ya urais Desemba mwaka
juzi, ukweli uko wazi kwamba hicho alichokisema
kilikwisha kuwapo na kwa hakika alikuwa akilazimika
kutafuta maneno yaliyokuwa na mwelekeo wa kutoa tiba.

Kuanza tena kwa mazungumzo kati ya vyama hivyo vya CCM
na CUF wiki iliyopita, vikiongozwa na Katibu Mkuu wa
chama tawala, Yussuf Makamba kwa upande mmoja na
Maalim Seif kwa upande mwingine, kumelirejesha taifa
kule kule lilikoshinwa miaka kadhaa iliyopita.

Ingawa CCM katika kipindi chote tangu Uchaguzi Mkuu wa
kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 imekuwa ikibadilisha
majemedari wakuu na wasaidizi wake wa kukabiliana na
mzozo wa kisiasa wa Zanzibar, kutoka kwa Ali Hassan
Mwinyi (1994-95), Dk. Salmin Amour Juma (1995-2000) na
Benjamin Mkapa (1995-2005), CUF wao kwa miaka hiyo
yote wamekuwa wakimuweka mbele Maalim Seif katika
makabiliano hayo.

Kwa maneno mengine, mwenendo huu wa mambo ambao
hauendi mbele zaidi ya kurudi nyuma na kuongeza hali
ya wasiwasi, umemwacha Maalim Seif kuwa ndiye nguzo
kuu ya kubadilika kwa mwelekeo wa mambo katika siasa
za Zanzibar.

Japo mwenyewe Kikwete, hajatoa kauli yoyote
akimwelekezea Maalim Seif, anaonekana kutambua ukweli
wa mambo ulivyo huko Zanzibar ambao nyuma ya jinamizi
mpasuko yuko huyo mwanasiasa huyo.

Ingawa CCM na CUF wameanzisha tena mazungumzo ya aina
ile ile yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1998 na
baadaye tena yakarejewa mwaka 2001, bado kuna
uwezekano kuwa majibu ya mazungumzo ya sasa yakazaa
mazungumzo mengine baada ya mwaka 2010.

Vyama hivyo vinaingia katika mazungumzo, wakati hali
ya kisiasa ya Zanzibar ikiwa iko bayana kabisa machoni
mwa wadadisi wa masuala ya kisiasa na kiutawala.

Majibu ya tatizo la Zanzibar ni mengi na rahisi kwani
katika kipindi cha miaka 15 kilichopita yamekuwa
yakibainishwa na watu mashuhuri, yakafanyiwa utafiti
na taasisi za kisomi na matokeo yakaonekana pia katika
chaguzi tatu zilizopita.

Hayati Abdulrahaman Babu mmoja wa Wazanzibari wasomi
alipata kutafakari kuhusu namna bora kabisa ya
kumaliza tatizo la Zanzibar ambalo wakati fulani huko
nyuma liliwahi kushuhudia uhasama mkali kati ya
wanachama wa vyama viwili vya CCM na CUF.

Profesa Babu, mmoja wa wanaharakati wa mwanzo wa siasa
za Zanzibar alikufa akiamini kwamba suluhu ya kudumu
visiwani humo itakapitakana iwapo tu itajengwa nguvu
kubwa ya tatu, itakayovilazimisha vyama vikuu hivyo
viwili vya CCM na CUF kupoteza ushawishi.

Kwa bahati mbaya, si Babu mwenyewe wala waumini wa
ajenda yake hiyo wakiwamo wanasiasa kama Sultan Sultan
na Naila Jiddawi walifanikiwa kuiweka mezani na
ikapata visheni ya mafanikio ambayo alikuwa
akiyafikiria. Hilo likawa moja ya majibu ya kupatikana
kwa suluhu ya kudumu Zanzibar.

Mwaka 1995 muda mfupi tu baada ya kupata taarifa
kwamba, Dk. Salmin Amour Juma aliyekuwa mgombea urais
wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM alikuwa ndiye mshindi
kwa kupata asilimia 50.2 ya kura zote zilizopigwa,
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitoa kauli
ambayo chama alichokiasisi kimeendelea kuikataa na
kuifumbia macho.

Mwalimu ambaye wakati huo alikuwa Morogoro akimpigia
kampeni Benjamin Mkapa aliyekuwa mgombea wa urais wa
Tanzania, aliwataka wana CCM wa Zanzibar kukubali
kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo
ingekishirikisha chama cha CUF ambacho mgombea wake,
Maalim Seif alipata asilimia 49.8 ya kura zote.

Jibu la CCM na la Salmin ambalo lilikuja kuungwa mkono
na viongozi wenzake wote wa CCM (ukimwacha Mwalimu)
zama hizo, akiwamo Mkapa aliyekuja kuwa Rais wa
Tanzania, lilikuwa rahisi kabisa; “ushindi ni ushindi
hata ukiwa ni wa kura moja.”

Jibu hili lilikwenda sambamba na uamuzi wa chama hicho
tawala kuamua kuchukua kilichokuwa chake na ambacho
hakikuwa chake, kikafanya ubabe kuwatawala hata wale
waliokuwa wakikipinga dhahiri.

CCM kimefanya hivyo wakati kikijua bayana kwamba,
uhalali wake wa kuitawala Zanzibar yenye visiwa viwili
ulikuwa ukikomea katika eneo moja tu la Unguja.

Jeuri ya CCM kukataa kukubali ukweli mchungu kwamba
hakina uhalali Pemba, leo hii umelifikisha Taifa hili
hapa lilipo na kimsingi imezaa kile ambacho mwenyekiti
wake wa sasa, Kikwete amekiita mpasuko.

Jitihada za chama hicho tawala za miaka 12 iliyopita
za kujaribu kugeuza mioyo ya Wapemba ikigeukie
zimekwama na kimsingi zimeendelea kupoteza mwelekeo na
kudharauliwa.

Wapemba wa CCM wa aina ya marehemu, Dk Omar Ali Juma,
Dk. Ali Mohammed Shein, Mohammed Aboud na wengine
wachache wameendelea kuonekana kuwa ni wasaliti wa
wenzao wa kwao.

Mpemba pekee anayebakia kipenzi cha watu wake na
shujaa wa kisiwa hicho, ni Maalim Seif. Mwanasiasa
huyo hivi sasa amepoteza uhuru wake binafsi ndani ya
chama chake, amefanywa kuwa taasisi inayojitegemea.

Watu wa kisiwa hicho anachotoka wamekataa kumsahau,
tangu alipotimuliwa kutoka ndani ya CCM mwaka 1988,
karibu miaka 20 iliyopita.

Kile ambacho alikifanyia kisiwa hicho tangu akiwa
ofisa wa juu serikalini kabla hajapanda na kuwa Waziri
wa Elimu na baadaye Waziri Kiongozi kwa marais watatu,
Aboud Jumbe Mwinyi, Dk Abdul Wakil Nombe na baadaye
Ali Hassan Mwinyi hakijasahaulika.

Ingawa CCM haipendi kuyasikia maneno haya, wala
kuukubali ukweli huu, Maalim Seif bado anabakia kuwa
kiongozi aliye ndani ya mioyo ya Wazanzibari
wasiyoikubali CCM kihistoria na kisera huko visiwani.

Nilipofanya mahojiano na Rais Jakaya Kikwete, mjini
Dodoma siku chache tu kabla hajashinda urais, Desemba
mwaka 2005, na kumuuliza iwapo CCM ilikuwa ikijutia
uamuzi wake wa mwaka 1988 wa kumfukuza Maalim Seif na
wenzake 17 ndani ya chama hicho tawala, hakuwa tayari
kuukubali ukweli huo.

Ingawa Kikwete kama walivyo wana CCM wenzake wameamua
kuukataa ukweli, historia itaendelea kubakia pale pale
kwamba, dhambi ya chama hicho tawala ya kuwanyima
Wapemba dhamana ya kuviongoza visiwa hivyo ndiyo
inayowatafuna hadi leo.

Wazanzibari, hususan wale wenye asili ya Pemba,
tofauti na Wabara wamejengwa katika kuheshimu na
kuikubali historia ya visiwa hivyo.

CCM ipende isipende inapaswa kutambua kuwa, Wapemba
wanakumbuka namna Mapinduzi ya mwaka 1964
yalivyokisahau kisiwa hicho kutokana na udhaifu mkubwa
wa kimuundo ambao chama cha Afro Shiraz Party (ASP)
ilikuwa nao.

Inapaswa kufahamu pia kwamba, Maalim Seif ni miongoni
mwa vijana wasomi wa mwanzo wa baada ya Mapinduzi hayo
ambao kuingia kwao serikalini, mwanzoni mwa miaka ya
1970, kulianza kufufua matumaini mapya ya Wapemba
kutambulika na kukubalika.

Kikwete na wana CCM wenzake wa sasa wanapaswa kutambua
na kukubali kuwa, kupanda haraka haraka kisiasa kwa
watu kama Maalim Seif na vijana wenzake wa zama hizo,
akina Hamad Rashid Mohammed halikuwa suala la bahati
mbaya.

Aidha, Kikwete, Rais Amani Abeid Karume na wahafidhina
wengine wa CCM Zanzibar wanapaswa kutambua kuwa,
mchango mkubwa wa Maalim Seif na uwezo wake binafsi wa
kiuongozi tangu akiwa serikalini ndiyo sababu kuu
iliyomjengea heshima na kukubalika hata kufikia
kiwango cha kuabudiwa kisiasa na wale wanaomuenzi leo
hii.

Kama hiyo haitoshi; CCM inapaswa kutamka bayana ama
ndani ya vikao vyake na ikibidi hadharani kwamba,
uamuzi wa kibaguzi na wa kimizengwe uliompokonya
Maalim Seif haki yake ya kukubalika ya kuwa Rais wa
Zanzibar, baada ya Mzee Mwinyi kuwa Rais wa Tanzania,
ni sehemu ya dhambi zinazoitafuna Zanzibar leo hii.

Ingawa CCM ilifanya hivyo ikimlenga Maalim Seif,
matokeo ya uamuzi huo wa hovyo, yaligusa hisia za
Wapemba na vijana wapenda maendeleo wa zama hizo wa
aina ya akina Juma Duni Haji (Muunguja), Hamad Rashid
Mohammed, Aboubakar Hamisi na wengine wengi.

Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa. Vijana wengi
machachari na wapenda mabadiliko waliamua kufungamana
na Maalim, tangu wakati huo wakaunda mtandao wa
kuihujumu CCM Zanzibar iliyoamua kwa makusudi
kuendesha ubaguzi ule ule ambao ulizaa mapinduzi mwaka
1964.

Kikwete na wana CCM wenzake wanapaswa kutambua kwamba,
Zanzibar inadai Mapinduzi mengine na kimsingi
mapinduzi hayo yanakuja. Yatakuja kwa CCM kupenda au
kutopenda.

Watanzania, Wazanzibari na dunia ya wapenda mageuzi
inatakiwa kulifahamu, kulikubali na kujiandaa kwa
tukio hilo linaloweza kuja wakati wowote na kuundoa
usultani wa ‘CCM Zanzibar kukubali kubeba dhamana ya
makosa yake.

Mapinduzi mengine Zanzibar yanakuja. Yatakuja wakati
huu wakati akina Kikwete, Karume, Maalim Seif na
wenzake wa CCM na CUF wakiwa hai au hata watakapokuwa
wamekufa.

Zanzibar inahitaji mapinduzi yatakayoiondolea CCM
ukiritimba na dhana ya mapinduzi daima. Zanzibar
inadai mapinduzi yatakayoondoa udikteta wa CUF Pemba.
Zanzibar inadai mapinduzi yatakayoondoa ubaguzi wa
Wazanzibari dhidi ya Watanganyika, Wapemba dhidi ya
Waunguja.

Zanzibar inadai mapinduzi ya fikra yatakayoondoa
ubaguzi wa rangi wa sisi weusi, wale Waarabu, sisi
Wangazija wale Wanyamwezi na kadhalika.

Zanzibar inadai mapinduzi yatakayomaliza urithi wa
hovyo kabisa wa kibaguzi wa sisi ndiyo CCM- ASP wale
ni wabuguzi wa Ki-Hizbu.

Zanzibar inadai mapinduzi yatakayoondoa uhalali wa
Waaunguja kuendelea kuwatawala Wapemba. Mapinduzi ya
kuondoa uhalali usio halali wa CCM kujipa dhamana ya
kuvitawala visiwa hivyo kimabavu.

Iwapo CCM Zanzibar inadhani kwamba, tatizo la Zanzibar
ni Maalim Seif, itakuwa ikifanya makosa ya Marekani
inayofanya katika dunia ya sasa.

Wakati fulani, Taifa hilo kubwa duniani lilidhani kuwa
kifo cha kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Il Sun
alipofariki dunia na ikadhaniwa kwamba huo ndiyo
ungekuwa mwisho wa sera za kikomunisti za Juche.
Ilikosea alikuwapo Kim Jong Ill.

Ni kosa hilo hilo ambalo taifa hilo kubwa limekuwa
likilifanya Irak leo, inakodhani kuuawa kwa watoto wa
Saddam na baadaye baba yao na jamaa wengine wa
kiongozi huyo wa zamani wa Irak kungemaliza mambo.
Maafa yanayotokea Irak leo yanatisha.

Si huko tu, hivi sasa taifa hilo kubwa linafuatilia
kwa karibu hali ya afya ya Rais Fidel Castro wa Cuba
ambaye ni mgonjwa, likidhani kuwa kifo chake
kitamaliza sera za kikomunisti za nchi hiyo ya
Marekani Kusini. Hata katika hilo inajidanganya.

Kwa hakika CCM Zanzibar inapaswa kutambua kwamba,
Maalim Seif ameshafika hatua ya kujijenga na kuwa
taasisi na kwa bahati kwao alipata kuwa kada mwaminifu
wa chama hicho tawala ambacho kimsingi kuondoka kwake
kulikuwa ni kwa kulazimika kama si kwa kulazimishwa.

Kwa sababu hiyo basi, Maalim Seif ndiye mtu wanayeweza
kukaa naye meza moja wakazungumza kutokana na kuwa
kwake na chembe chembe za damu ya CCM, tofauti na
ilivyo kwa vijana Wazanzibari wanaokiunga mkono CUF
waliosambaa dunia nzima na ambao hawajahai kunusa
harufu ya U-CCM.

Viongozi wetu wa kisiasa na kiserikali wanapaswa
kutambua kuwa, vijana hao walio ndani ya nje ya
Zanzibar, ndani na nje ya Tanzania, wana hasira kubwa
na CCM. Wao ndiyo waliopiga kura ambazo wanaamini
ziliibwa mwaka 1995, 2000 na 2005.

Watakapobaki wenyewe bila ya kuwapo kwa Maalim Seif,
mwanasiasa mliberali, vijana hao ambao miongoni mwao
wako wale waliochinja polisi mwaka 2001 na
kuvishambulia kwa mawe vituo vya polisi wakijaribu
kuzifikia silaha na wengine kukimbilia nje ya nchi
wanaweza wakaamua kufanya lolote litakalofanana na
Mapinduzi ya mwaka 1964.

Ingawa juhudi za sasa za CCM na mwenyekiti wake
Kikwete zinaweza zikawa na lengo kama lile la akina
Mkapa la kutaka kuwaridhisha wafadhili badala ya
kuutazama mustakabali wa Zanzibar ki kweli kweli,
mtazamo wa namna hiyo unaweza ukaja kuliweka taifa
hili katika wakati mgumu ujao siku zijazo.

Mwisho

Labels:

 
Muandishi: Absalom Kibanda Saa: 2:32 AM | Webu Unganishi | Maoni 1